Elias Msuya
Platinum Member
- Dec 23, 2011
- 267
- 1,014
Serikali imeahidi kuendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi kupitia upatikanaji wa mitaji, zabuni za umma, mafunzo ya ujuzi na maboresho ya sera na sheria mbalimbali.
Hayo yameelezwa leo Julai 5 jijini Dar es Salaam na Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan katika hafla ya kuwatunuku washindi wa shindano la ubunifu kwa vijana.Ameeleza kuwa Serikali kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeweka mkakati wa kujenga uchumi imara unaotegemea nguvu ya vijana, ambao kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ni zaidi ya milioni 21.3, sawa na asilimia 34.5 ya Watanzania.
Aidha, alisema Serikali imeunda Wizara ya Maendeleo ya Vijana ili kuratibu sera na programu zinazolenga kuwawezesha vijana kupata ajira, ujuzi, ubunifu na mitaji ya kuanzisha biashara.
Katika maboresho yaliyofanywa, alisema Sheria ya Ununuzi wa Umma imeendelea kutenga asilimia 30 ya zabuni kwa makundi maalumu, huku asilimia 10 ya zabuni hizo zikitengwa mahsusi kwa vijana. Alibainisha kuwa hadi mwaka 2026, vikundi 299 vya vijana vyenye wanachama zaidi ya 2,226 tayari vimesajiliwa katika mfumo wa manunuzi ya umma na vinaendelea kushiriki katika zabuni mbalimbali.
Serikali pia imeongeza sehemu ya fedha za mikopo ya halmashauri itakayolenga kujenga miundombinu ya biashara kwa vijana, hatua inayolenga kutatua changamoto ya maeneo ya kufanyia biashara ambayo imekuwa ikiwakabili wajasiriamali wengi.
Kwa upande wa sera za kodi, alisema katika mwaka wa fedha 2026/2027 Serikali imeanzisha msamaha wa kodi ya mapato kwa wafanyabiashara wapya kwa kipindi cha mwaka mmoja ili kuwapa nafasi ya kuimarisha biashara zao kabla ya kuanza kulipa kodi.
Dk Mwigulu ameeleza pia kuwa Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya biashara kupitia utekelezaji wa mapendekezo ya "Mkumbi Namba Mbili", pamoja na kuanzisha mfumo wa dhamana kupitia Benki Kuu ya Tanzania utakaorahisisha wafanyabiashara wadogo na wa kati kupata mikopo.
Amesema Serikali pia inakusudia kuanzisha mfumo wa matumizi ya dhamana zinazohamishika, ikiwemo vyeti vya taaluma, stakabadhi za mazao na mali nyingine, ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo kwa vijana na makundi mengine ya uzalishaji.
"Tunataka vijana wenye elimu na ujuzi waweze kutumia uwezo wao kupata mitaji badala ya kuzuiwa na ukosefu wa dhamana za kawaida. Hili litafungua fursa kubwa zaidi za uzalishaji na ajira," amesema.
Awali akimkaribisha Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, alisema awali waliwachuja vijana na kupata washindi 100, ambao walipewa mafunzo maalum, ambapo kati yao vijana 10 waliteuliwa kushindanishwa ili kupata washindi watatu.
Mshindi katika shindano hilo alitangazwa kuwa ni Geoffrey Sanga aliyejichukulia kitita cha Sh50 milioni, akifuatiwa na Jacob Lugwisha aliyechukua Sh30 milioni na watatu ni Robert Malonga aliyepata Sh20 milioni.