BARD AI
JF-Expert Member
- Jul 24, 2018
- 3,591
- 8,826
Siku chache baada ya uongozi wa Hospitali ya Bugando Mwanza kuelezea kadhia wanayoipata kutokana na vijana kuulizia iwapo wananunua figo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa Dk Alphonce Chandika naye leo Jumatatu Machi 13, 203 ameeleza kuwepo na wimbi la vijana wanaopiga simu hospitalini hapo kuuliza ikiwa wanaweza kuuza figo zao.
Dk Chandika amesema hadi sasa amepokea simu zisizopungua nne kutoka kwa vijana hao wakidai kutaka kuuza figo hali aliyoieleza kuwa ni kutokana na changamoto za maisha.
"Hili suala lipo unakuta vijana maisha yana changamoto halafu anajua Benjamin Mkapa wanapandikiza figo, wamekuwa wakipiga simu. Niwaombe huo utaratibu haupo na sheria zetu haziruhusu biashara ya uuzaji wa viungo na hata tukigundua kuna biashara imefanyika tunasitisha mara moja," alisema Chandika.
Dk Chandika ameyasema hayo leo Machi 13, 2023 wakati akizungumza kwenye hafla ya maadhimisho ya miaka mitano ya huduma ya upandikizaji figo iliyoanza kutolewa hospitalini hapo mwaka 2018.
Aidha Chandika amesema katika kipindi hicho wamekutana na changamoto ya ukosefu wa elimu kwa baadhi ya ndugu na kushindwa kutoa figo wakihofia kufariki dunia.
Akizungumzia huduma hiyo Faraji Shabani aliyepandikizwa figo aliyopewa na mtoto wake amesema huduma hiyo imesaidia kuokoa maisha yake kutokana na kuugua muda mrefu.
Aidha Shabani amewaasa wananchi kujiunga na huduma ya Bima ya Afya kwa Wote kwani baadhi ya huduma katika upandikizaji wa figo hufidiwa kwa mgonjwa mwenye bima.
Naye Neema Sweti aliyempa figo kaka yake alisema alipata ujasiri huo baada ya kupata semina ya huduma hiyo mara kwa mara na sasa anaendelea vizuri baada ya miaka mitano tangu atoe figo yake.
MWANANCHI