Huu ni mwaka wa 30 tangu China ilipoanza kupeleka vikosi vya kulinda amani kwa nchi za nje. Ikiwa moja ya nchi kubwa zaidi duniani, katika miaka 30 iliyopita, China imetekeleza kikamilifu wajibu wake wa kimataifa, na kutoa mchango muhimu katika kudumisha amani na utulivu duniani, hasa barani Afrika, kwa vitendo halisi.
Tarehe 16 Aprili mwaka 1992, kwa mara ya kwanza China ilipeleka kikosi cha kulinda amani nchini Cambodia kupitia operesheni ya ulinzi wa amani ya Umoja wa Mataifa. Katika miaka 30 iliyopita, China imeshiriki katika operesheni 25 za kulinda amani za Umoja wa Mataifa, na kutuma takriban askari 50,000 wa kulinda amani katika nchi zaidi ya 20 duniani.
Bara la Afrika ni sehemu muhimu kwa China kushiriki katika ulinzi wa amani. Mwaka 2015 rais Xi Jinping wa China alipohudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani, aliahidi kuongeza msaada kwa Afrika ili bara hilo liweze kudumisha amani na usalama. Katika miaka 30 iliyopita, China imeshiriki katika zaidi ya operesheni 20 za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa, na nyingi zikiwa barani Afrika.
Mwaka 2013, China ilituma kikosi cha kulinda amani nchini Mali. Kikosi hicho kiliundwa na wahandisi, wafanyakazi wa afya na walinzi wa usalama, na ilikuwa mara ya kwanza kwa China kutuma kikosi cha usalama tangu iliposhiriki katika operesheni ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa. Mwaka 2015, China ilituma kikosi cha askari 700 wa kulinda amani nchini Sudan Kusini, na hii ilikuwa mara ya kwanza kwa jeshi la China kutuma kikosi cha askari wa miguu kushiriki katika operesheni ya Umoja wa Mataifa. Mwaka wa 2017, China ilituma kikosi cha kwanza cha helikopta cha kulinda amani huko Darfur, Sudan, ili kutoa msaada muhimu kwa operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa katika eneo hilo.
Hivi sasa, China ina zaidi ya wanajeshi 2,000 wa kulinda amani barani Afrika, ambao ni zaidi ya asilimia 75 ya walinda amani wote wa Umoja wa Mataifa barani Afrika, na zaidi ya asilimia 80 ya walinda amani wa China walio nje ya nchi. Askari hao wa kulinda amani wa China wanalinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Liberia, Sudan, Sudan Kusini, Mali, Libya na Jamhuri ya Afrika ya Kati na nchi nyingine za Afrika zinazokumbwa na vita na migogoro.
Kwa sasa, China ni nchi iliyotuma walinzi wengi zaidi wa amani kati ya nchi wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na pia ni nchi ya pili katika utoaji wa fedha kwa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa. China siku zote imekuwa mjenzi wa amani ya dunia, mchangiaji wa maendeleo ya kimataifa, na mtetezi wa utaratibu wa kimataifa. Katika siku zijazo, wanajeshi wengi zaidi wa China watajitolea kuchangia katika kudumisha amani na utulivu duniani, haswa barani Afrika.