Mdogo wangu Shomari Salehe Kacheuka mtoto wa Salehe Shomari Kacheuka ambaye alikuwa akifanya kazi katika kampuni ya GS Group Limited inayoingiza na kuuza pikipiki aina ya Haujue eneo lake la kazi likiwa mtaa Nyamwezi na Msimbazi ameuawa na polisi siku ya Jumatano, Desemba 27. Shomari nilikuwa naye katika eneo la kazi mpaka ofisi ilipofungwa mida ya saa kumi na mbili kama na robo hivi. Aliondoka Kariakoo majira ya hayo kuelekea nyumbani kwake Vingunguti Kiembembuzi. Muda wa kama dakika 40 baadae kaka yake anaietwa Omary Salehe Kacheuka alipiga simu kusema Shomari anashambuliwa na Polisi. Kwa maelezo ni kwamba Shomari alipaki pikipiki akaingia ndani na kutoka muda huohuo. Alipotoka akakutana na watu waliojitambulisha kama askari waliotaka kuondoka naye. Alipowauliza kulikoni wakamtolea bastola. Punde kuna kijana wa Car wash ya jirani anaejishughulisha na kuosha pikipiki alikuwa akipita. Akahoji kulikoni wakampiga risasi ya mguu. Katika hali ya sintofahamu na taharuki wakampiga risasi ya goti Shomari. Wakawaburuza kutoka nyumbani mpaka barabarani. Barabarani wakaendelea kumshambulia Shomari na kumfyatulia risasi kadhaa. Wakamburuta mpaka kwenye defender na yule waliempiga risasi ya mguu wakampakiza kwenye IST na kutokomea kusikojulikana.
Kama familia tulianza kumtafuta kuanzia majira hayo. Tunaruhusu kufuatilia mawasiliano yetu yote kuanzia saa moja ya siku mpaka sasa. Tulifika vituo vyote vya polisi bila mafanikio. Tulimpigia mkuu wa kituo Buguruni kwenye namba yake hii 0787668306 tuliyopatiwa na msamalia mida ya saa mbili usiku. Akasema bado hajapata taarifa ila ataifanyia kazi. Tuluripoti vituo kadhaa vya polisi ikiwemo Tabata, Vingunguti, Stakishari, Msimbazi, Central, lakini tuliambiwa hata taarifa hizo hazijawafikia. Tulifika Buguruni polisi usiku ule na alfajiri hakukuwa na taarifa. Tukaenda Selander Bridge tulipotoka Buguruni na kufuatilia Muhimbili bila mafanikio. Tukipotoka Muhimbili tukapita Msimbazi na kwenda Amana hospital. Amana hakukuwa na rekodi za kupata majeruhi wala miili ya watu wa tukio aina hiyo. Hivyo kama familia tukaamua kurudi Buguruni kufungua jalada. Buguruni tukakabidhiwa Askari aliejulikana kwa jina la Sylvanus baada ya kuzunguushwa mara kadhaa ili atufungulie jalada. Namba ya Afande Sylvanus ni hii 0755329211. Afande Sylvanus akatuambia kwasababu tukio limetokea majira ya saa moja kasoro usiku inatubidi tuvute subira yafike masaa 24 ndio tufungue jalada. Mimi nikamwambia hatukuja kufungua jalada la kupotelewa na ndugu. Tumekuja kufungua jalada la ndugu kutekwa na wasiojulikana. Tena wakiwa wamepigwa risasi miguuni. Na pamoja na jitihada zetu kama familia kufika sehemu zote ambazo tungesaidia mmeshindwa kutusaidia kutuma hata askari kwenda eneo la tukio. Lakini akiongozwa na askari mwenzake mwenye kama suzua kadhaa ukubwa wa zabibu na ndimu changa kichwani walitugomea kabisa kutufungulia jalada. Ikabidi tutoke nje tuanze kujadiliana. Pembeni yetu tukiwa na askari wawili wanaosikiliza maongezi yetu ambapo tukisema maadamu Polisi wameshindwa kutusaidia basi twende kwa Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama wa Mkoa ambaye pia ni mkuu wa mkoa. Tukaachana ambapo wengine wakarudi kwanza nyumbani. Tunafika nyumbani tunakutana na Mwenyekiti wa serikali ya mtaa nadhani ambaye anasema amepigiwa simu kuwa vijana wale wawili wapo Amana hospital hali zao ni mbaya. Baadhi ya wana familia wakarudi Amana ambako bado wakasema hakuna majeruhi wa risali wala maiti zilizoingia. Mwishoni tukajaribu kwenda moja kwa moja Mortuary kuulizia. Ndio mtu wa Mortuary akasema leo asubuhi kuna miili miwili ililetwa na askari imeokotwa maeneo ya Vingunguti labda mkaangalie. Kuangalia ndio tukatambua kuwa ni wale vijana wetu tuliokesha tukiwatafuta bila mafanikio zikiwa na majaraha mengi ya risasi.
Sisi kama familia tuliamini labda kijana alipita eneo lisilo sahihi katika muda huo na kupelekea kufananishwa na mtu fulani. Tuliamua kumshitakia Mungu tukampumzisha Marehemu ili maisha yasonge. Mengine tumemwachia Mungu. Lakini kilichotusikitisha ni ripoti iliyotolewa na Kamanda Murilo kwa kuwabatiza uhalifu na kuwahusisha na tukio la panya road lililotokea majira ya saa mbili huko Vingunguti huku likiwahusisha vijana hao. Bila haya wala hofu ya Mungu akawabatiza na majina mabaya. Kama familia tunatoa ruhusa kwa mamlaka kufuatilia mawasiliano yetu wote wana familia kuanzia saa moja usiku ili kuonesha ni namna gani jeshi letu lilivyowafanyia udhalimu vijana hawa. Pia tunaomba serikali ifuatilie mtaani alipoishi Shomari nyumba kwa nyumba kujua alikuwa na tabia zipi na kama ashawahi hata kulala ndani kwa kukaa tu kijiweni ama kuzurula. NB. Hakuna jirani anaemjua Marehemu kwa jina la Shomari. Toka mchanga anajulikana kwa jina moja tu la Babuu. Shomari ni jina analotumia kwenye documents tu na shuleni.
Naomba taarifa hii imfikie Mheshimiwa Raisi huenda akatia mkono wake na ukweli ukabainika na ikawa faraja kwa familia.
Natanguliza shukran.
Mungu asimame na wote wenye kuisimamia na kuiishi Haki
🙏🏿🙏🏿🙏🏿🙏🏿