Viongozi na kuhangaika kurekebisha mambo wanapotembelewa na viongozi ngazi za Juu

Viongozi na kuhangaika kurekebisha mambo wanapotembelewa na viongozi ngazi za Juu

Nyendo

JF-Expert Member
Joined
Jun 4, 2017
Posts
1,336
Reaction score
4,731
Ukistaajabu ya Mussa utaona ya viongozi wakiwa na hekaheka za kurekebisha mambo yao wakijua watatembelewa na viongozi ngazi ya juu, utajionea vituko vya mahangaiko yao wakati siku zote walikuwa wamekaa kama hawaoni kuna kasoro au hawahusiki na kurekebisha.

Utapigwa butwaa kama ni barabara zitachongwa sehemu anazopita Kiongozi huyo wa ngazi za juu, nyasi, mashimo na takataka zitazolewa, kama ni ofisi ilikuwa imekaa kama zizi la ng'ombe la watani zangu wagogo utaona inapangwa na kama rangi imechakaa hawatasita kupaka rangi mpya ilimradi tu mgeni wao akifika akute mambo yako shwari, kuta zenye nyufa zitarekebishwa na tandabui watatolewa kwenye ofisi kwa nyakati za ujio wa mgeni wao.

Hapo ndipo ule usemi wa mgeni njoo mwenyeji apone unapokamilishwa kwa wananchi kupatiwa maji siku hiyo iwapo mgeno wao huyo atakuwa na ratiba ya kuwafikia wananchi wa eneo fulani basi watu hao kama walikuwa wanaona mabomba tu bila maji kwa wakati huo yatatoka maji mpaka unajiuliza haya maji siku zote yalikuwa wapi au wameyanyesha wao kwa mvua zao wenyewe?

Uwajibikaji kwa Tanzania kwa viongozi wa chini haupo ila huigiza mambo kwa muda kwa kumuogopa aliyewateua au kuwajibika kwa ajili ya kutafuta kuchaguliwa tena kinapokaribia kipindi cha uchaguzi, lakini asipokuwepo karibu aliyewateua hawana muda na wananchi wala miundombinu inaowazunguka waanchi kwa ajili ya ustawi wa maisha yao, na kama ni wa kuchaguliwa basi wakishaingia madarakani hakuna uwajibikaji mpaka pale watakapo taka tena kuchaguliwa ndipo huigiza kuwajibika.

Ndio maana unakuta barabara zina mashimo kama hawaoni au hawahusiki, maji hayatoki wanaendelea na maisha yao tu kisa kwao yanatoka, hakuna huduma muhimu za kijamii hawajali kwa kuwa mwananchi kwa wakati huo hana cha kuwafanya, ila kiongozi anayeweza kuwawajibisha wale walioteuliwa ndio huanza kuhangaika kutwa kucha kufukia mashimo mpaka usiku ili waonekane wanawajibika au hawana kasoro waendelee kuaminika na kuteuliwa tena wakati mwingine.

Jifunzeni kutimiza wajibu wenu hata kama wanaoweza kuwawajibisha wako mbali nanyi, juweni mpo kwa ajili ya wananchi na si kuwaonesha waliowateua, kama mnaweza kurekebisha makosa wanapokuja viongozi kwa nini msirekebisha kabla ili mazingira yawe salama kwa wananchi wanaoishi maeneo hayo?
 
Back
Top Bottom