KERO Viongozi wachunguze Kituo cha Afya Kadashi, Wilaya ya Kwimba – Mwanza. Utendaji unatukwaza Watumishi

KERO Viongozi wachunguze Kituo cha Afya Kadashi, Wilaya ya Kwimba – Mwanza. Utendaji unatukwaza Watumishi

Hii ni kero ambayo mwananchi ameiwasilisha JF akitaka wahusika kuchukua hatua
A

Anonymous

Guest
photo_2026-07-24_09-55-12.jpg
Kituo cha Afya Kadashi kipo Wilaya ya Kwimba, Mkoa wa Mwanza, Kata ya Maligisu Kijiji cha Kadashi kina Watumishi 12 ambao ni Co 3, NO 1, ANO 3, EN 2, MAT 2 na CA 1.

Mimi ni mmoja wao, nimeamua kueleza changamoto tunazopitia kwa sababu hali iliyopo imekuwa ngumu kwetu watumishi na inaweza kuathiri hata huduma tunazowapa wananchi,

Pamoja na juhudi zetu za kuwahudumia wananchi, tumekuwa tukikumbana na changamoto kubwa ya uongozi. Changamoto kubwa tunayoiona ni namna kituo kinavyoendeshwa na Mganga Mfawidhi ambaye pia ni Daktari (Medical Officer).
photo_2026-07-24_09-55-11.jpg
photo_2026-07-24_09-55-11 (2).jpg
Kwa muda tumekuwa tukiona maamuzi mengi yakifanyika bila kuwashirikisha watumishi wengine. Kwa sababu yeye ndiye mkuu wa kituo, mara nyingi tunahisi mamlaka yake yanatumika bila kuzingatia maoni ya wengine. Hali hii imesababisha baadhi ya watumishi kujiona hawana nafasi ya kueleza changamoto zao au kushiriki katika maamuzi yanayohusu kituo.

Kinachotuumiza zaidi ni pale tunapomhudumia mgonjwa kwa kufuata taaluma zetu, lakini baadaye anapofika daktari mfawidhi anakagua matibabu yaliyotolewa na wakati mwingine kuyakosoa mbele ya mgonjwa.

Hali hiyo humfanya mgonjwa kupoteza imani na mtumishi aliyemhudumia, kana kwamba hana uelewa wa kazi yake, jambo ambalo linaathiri heshima na morali ya watumishi.

Pia tumekuwa tukipata changamoto pale tunapohitaji msaada wa daktari kwa wagonjwa wenye hali ngumu. Wakati mwingine tunapomuita aje kumuona mgonjwa, badala ya kufika moja kwa moja tunapewa maelekezo kwa simu akiwa ofisini au akiwa katika shughuli nyingine. Sisi tunahitaji ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bora kwa wakati.

Kuna pia changamoto kwenye usimamizi wa dawa. Tumekuwa tukizuiwa kuingia stoo ya dawa isipokuwa watu wachache waliowekwa. Hali hii imekuwa ikizua maswali kuhusu uwazi wa usimamizi wa dawa.

Wakati huohuo, kila mara tunasikia taarifa za dawa kupotea, jambo ambalo linahitaji uchunguzi wa kina.

Kuhusu malipo ya kazi za ziada na huduma za dharura (on call), tumekuwa tukiona changamoto katika mgawanyo wake. Wakati mwingine fedha ambazo ni stahiki ya mtumishi zinakatwa kwa ajili ya kununua dawa bila kuwa na mwongozo unaoeleweka. Mtumishi anayestahili kulipwa kiasi fulani anaweza kuishia kupata kiasi kidogo bila maelezo ya wazi.
photo_2026-07-24_09-55-10.jpg
Pia, tumekuwa tukiumizwa na namna baadhi ya mawasiliano yanavyofanyika. Baada ya vikao au kutokea kwa tofauti za kimawazo, wakati mwingine tunaona ujumbe wa vijembe kwenye mitandao ya kijamii kutoka kwa kiongozi ambaye tunategemea awe mfano wa kuunganisha watumishi. Hali hiyo inatengeneza mazingira ya hofu na kutokuaminiana.

Gari la wagonjwa ambalo limekaa takribani miezi sita bila kufanya kazi
Kwa upande wa huduma, kituo chetu kina changamoto za miundombinu. Tuna gari la wagonjwa ambalo limekaa takribani miezi sita bila kufanya kazi kwa sababu ya matatizo ya matairi na betri, licha ya kituo kuwa na uwezo wa kufanya matengenezo.

Tuna jengo la upasuaji lililokamilika lakini halitumiki ipasavyo, pamoja na chumba cha kuhifadhi maiti ambacho hakifanyi kazi tangu kujengwa.

Vyoo vya wazazi pia vina changamoto kubwa. Wakati mwingine vinapoziba, baadhi ya wazazi hulazimika kutoka nje ya jengo kutafuta sehemu nyingine ya kujisaidia, jambo ambalo si salama wala la heshima kwa huduma za afya.

Sisi hatupingi uongozi wala hatutaki kuvunja heshima ya kiongozi wetu. Tunachotaka ni mazingira bora ya kazi, ushirikiano na uongozi unaosikiliza watumishi. Tunaomba CHMT, Ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya na mamlaka husika zifike kituoni kwetu zione hali halisi na kuchukua hatua.

Tunaomba tupate kiongozi ambaye ataweza kushirikiana na watumishi, kusikiliza changamoto zetu na kuweka mbele maslahi ya wagonjwa na jamii. Tunataka kufanya kazi kwa amani na kutoa huduma bora kwa wananchi wa Kadashi.
 
Back
Top Bottom