Viongozi wapya wa serikali ya wanafunzi UDOSO 2026/27 waapishwa

Viongozi wapya wa serikali ya wanafunzi UDOSO 2026/27 waapishwa

University of Dodoma (UDOM)

Public Institution
Joined
Feb 24, 2024
Posts
50
Reaction score
55
WhatsApp Image 2026-06-01 at 16.20.07 (1).jpeg


Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) leo, tarehe 1 Juni 2026, kimewaapisha viongozi wapya waliochaguliwa kuiongoza Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOSO) kwa mwaka wa uongozi 2026/27. Hafla hiyo fupi ya kuapishwa imefanyika katika Ukumbi wa Seneti Jengo la Benjamin Mkapa ( Utawala Mkuu).

Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Lughano Kusiluka, amewapongeza viongozi wapya waliochaguliwa pamoja na wale wanaomaliza muda wao wa uongozi. Amesema ana matarajio makubwa kwa uongozi mpya kutokana na mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi uliopita, ikiwemo kuanzishwa kwa Mfuko wa Masomo (UDOSO Scholarship).

Prof. Kusiluka amewahimiza viongozi hao kuendelea kubuni miradi ya maendeleo yenye tija kwa wanafunzi, ikiwemo kuanzisha kampuni zitakazoweza kushiriki katika zabuni mbalimbali zinazotolewa chuoni.

"Natamani muanze kufikiria kuanzisha kampuni ambazo, baada ya kusajiliwa, zitaweza kupata zabuni na hivyo kuzalisha mapato yatakayosaidia kukuza mfuko wa UDOSO na kuwasaidia wanafunzi wengi zaidi," aliongeza Prof. Kusiluka.

Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Tafiti na Ushauri Elekezi, Prof. Razack Lokina, amewasihi viongozi hao kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wa msingi wa kuhudhuria vipindi na kufanya vizuri katika masomo yao. Aidha, amewapongeza kwa kuthubutu kugombea nafasi za uongozi, akisema hatua hiyo ni mwanzo mzuri wa kujenga viongozi bora wa taifa katika siku zijazo.

Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Jefta Sunzu, amewataka viongozi hao kuwa na mwenendo mzuri, kuzingatia maadili ya uongozi na kuwa mfano wa kuigwa katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya UDOSO, Bi, Najma Mdee, amesema mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa UDOSO 2026/27 haukuwa rahisi, lakini kutokana na ushirikiano mzuri kati ya Tume na Menejimenti ya Chuo, zoezi hilo lilifanyika kwa ufanisi mkubwa. Amewataka viongozi waliochaguliwa kutekeleza kwa vitendo ahadi walizozitoa wakati wa kampeni.

Kwa upande wake, Rais anayemaliza muda wake wa uongozi,Bi. Jackline Humbaro, amewasisitiza viongozi hao kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano uliopo chuoni, pamoja na kuzingatia kanuni, taratibu na miongozo yote ya Chuo.

WhatsApp Image 2026-06-01 at 16.20.06.jpeg


Naye Rais Mteule wa UDOSO, Gilberto Bulali, amesema uongozi wake utaendelea kusimamia maendeleo ya wanafunzi na kulinda hadhi na sifa ya Chuo Kikuu cha Dodoma. Aidha, amewataka viongozi wote walioapishwa kuwa waadilifu, kuwajibika ipasavyo na kushirikiana katika kuleta mafanikio chanya kwa wanafunzi na chuo kwa ujumla.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chuo, wakiwemo Rasi wa Ndaki, Maamidi wa Shule Kuu, Wakuu wa Taasisi, Walezi wa Wanafunzi, wawakilishi kutoka Kitengo cha Ulinzi na Usalama, pamoja na wanafunzi.
 
Back
Top Bottom