Visa hivi ni vya kuvipa muda

Visa hivi ni vya kuvipa muda

SteveMollel

JF-Expert Member
Joined
Jul 12, 2015
Posts
8,797
Reaction score
25,177
Katika muda huu wa mchana, bwana Cllint, mmiliki wa kampuni ya ujenzi, yuko kazini kama kawaida.

Anapopata nafasi anampigia simu mkewe, Joanna, na kumweleza ya kwamba leo atawahi kurudi nyumbani ili wawe pamoja kwasababu mwanamke huyo hatokuwepo weekend.

Haipiti muda Clint anampokea mgeni, wanaongea kidogo na kumalizana. Baadae Clint anajipaki kwenye gari na kuanza safari ya kwenda nyumbani.

Njiani anakutana na afande Sam. Wanazungumza kidogo na wanakubaliana waonane baadae kwa ajili ya kwenda kuvua samaki na Clint anaona si tabu kwani atakuwa na muda hivyo si mbaya.

Screenshot_20241006-163320.png


Clint anapofika nyumbani anakuta mbwa wake, Duke, anabweka sana sabababu hajafunguliwa, basi anamfungulia na kuingia ndani.

Humo anakutana na Joanna, mkewe, ambaye haonyeshi kafurahia kumwona mumewe hapa nyumbani muda huu.

Mwanamke huyo anasema inabidi aondoke kwasababu ana 'appointment' na daktari, lakini kabla hajaondoka, Clint anamshirikisha habari za mgeni alompokea leo hii kazini.

Mgeni huyo anataka kununua kampuni yake kwa 'mamilioni' ya hela lakini yeye hayuko tayari kwani hajui akiuza kampuni yake atafanya shughuli gani.

Swala hili linamkasirisha mkewe, Joanna, ambaye yeye anaona hela hiyo ni kubwa na hawatakiwi kuiacha.

Mwanamke huyo anamwambia Clint, kwanini wasiuze tu alafu warudi zao jiji la New York, jiji la maraha? Clint anamwambia wametoka huko kuja huku kutafuta maisha bora hivyo wabaki kwenye lengo lao.

Joanna ananuna na kuondoka kwa hasira. Anapanda gari na kutokomea kwenda kuonana na daktari wake, bwana Cortland.

Kumbe daktari huyo ni mchepuko wa Joanna.

Na hiyo appointment walonayo si ya tiba unazozijua wewe mwanetu.

AH-AH!

Sio tiba za panadol ya Kenya wala paracetamol za India.

Hizi ni tiba maalum.

Tiba mbadala.

Tiba za raha.

Raha maamumu.

Screenshot_20241006-170040.png


Joanna anatoa vitu vya uvunguni ambavyo hata mumewe hapati. Wanapomaliza wanaanza kusuka mipango ya kummaliza Clint ili wajilie raha zao vizuri.

Dokta anampatia Joanna sumu aliyoivuna kwenye mayai ya samaki. Anamwambia akamuwekee mumewe kwenye chakula na bwana huyo atakufa kwa shambulizi la moyo. Akishakufa wataiuza kampuni yake ya ujenzi alafu watakula raha milele.

Dokta anamwambia Joanna cha kuhakikisha ni bwana Clint anakula na kumaliza sumu yote ili kazi iwe nyepesi.

Screenshot_20241006-170222.png


Joanna anapofika nyumbani anapukutisha mkoba wake kutoa sumu. Chupa inaangukia mezani na kuvuja kiasi.

Anaichukua chupa na kuiweka kwenye ndoo ya nguo kisha anaanza mchakato wa kuandaa chakula.

Muda kidogo mumewe anarejea nyumbani. Wanasalimiana na kisha mume anaenda kumalizia viporo vyake vya kazi.

Wakati huo Joanna anaona fursa ya kuweka sumu kwenye glasi ya wine ya mumewe, bwana Clint.

Ghafla mume anarudi jikoni na kukwapua glasi zote mbili na kwenda nazo kwenye meza ya chakula. Joanna anapata hofu kama glasi atakayochukua mumewe ndo yenye sumu au lah.

Ila bahati kwake, Clint anapokunywa fundo kadhaa za wine, anashikwa na maumivu makali ya moyo.

b45066a9e77a2bac568a4ab417106479.png


Analia akishika kifua.

Anaanguka chini akimwomba mkewe amsaidie lakini Joanna hajigusi kwa lolote. Anamtazama Clint akihangaika huku akiomba afe upesi yeye aendelee na maisha yake.

Na kweli baada ya muda, Clint anakufa.

Cha kwanza Joanna anapiga simu kwa dokta Cortland kumwambia kazi ameifanya vema. Hivi anapoongea, maiti ipo chini inangoja shimo.

Dokta anampongeza kwa kazi kubwa alofanya.

Baada ya dakika kadhaa afande Sam na daktari Cortland wanafika eneo la tukio. Afande anashangaa kilichomkuta Clint kwani alikuwa naye muda si mrefu akiwa na afya njema.

Anapendekeza mwili wa Clint ufanyiwe 'post-mortem' ili kujua sababu ya kifo chake ila dokta Cortland anamuwahi kwa kumwambia haina haja.

Bwana huyu amekufa kwa mshtuko wa moyo, kufanya post-mortem ni kupoteza tu muda na pesa kwani kifo hakina utata wowote.

771ed29adb6bc9dd4255fa6af4b6c0bf.png


Mwili wa Clint unapelekwa mochwari, na kesho yake dokta Cortland anapiga simu mochwari kusema mke wa Clint anautaka mwili wa mumewe uzikwe upesi pasipo kuguswa.

Hivyo mwili unaandaliwa na kuhifadhiwa tena kwenye jeneza la bei chee.

Baadae watu wanaibuka kwenye mazishi ya Clint wakiongozwa na mkewe, Joanna. Mwanamke huyo amevalia nguo, kofia na miwani meusi.

Na kama ilivyo ada ya mnafki mbele za macho ya watu, analia kwa uchungu mpaka anabembelezwa.

Screenshot_20241006-170356.png


Watu wanajua ameumia kumpoteza mume, kumbe yeye anaona anachelewa kwenda kupata raha za dokta Kumpeneka.

Wakati huo wote, mbwa (Duke), anabweka sana hapa msibani kana kwamba ameona kitu cha hatari.

Baadae usiku, hata mwili ukiwa bado haujapoa huko ardhini, Joanna anakutana na dokta Cortland tena ndani ya nyumba ya marehemu. Bafu la marehemu. Kitanda cha marehemu.

Wanakutana kupeana pongezi kwa kumaliza kazi nzito. Kazi ya kung'oa kisiki.

Screenshot_20241006-170431.png


Mabusu kilo mbili.

Baby papasa huku. Usisahau na hapa. Baby aaah ... baby eeeh ...

Wakati huo mbwa anabweka sana huko nje. Hamna mtu wa kumfungulia.

Anabweka mpaka Joanna anakasirika. Anaona sasa inatosha. Anachukua gobore aende kummaliza Duke ili amfuate bwana Clint hukohuko kaburini.

Anafyatua risasi ila kwa bahati mbaya inaufungua mlango wa banda na Duke anakimbilia kizani.

Anajaribu kumfyatulia risasi lakini mbwa anapona.

Anakimbilia moja kwa moja kaburini kwa Clint. Anakaa pembeni ya kaburi hilo kwa huzuni kana kwamba anamngojea marehemu arudi.

Ajabu, kule kaburini, ndani ya jeneza, Clint anafungua macho. Kumbe ni mzima. Sumu alokuwa nayo mwilini sasa imekwisha nguvu na amerejea kwenye uhai wake.

Si bure dokta alimwambia Joanna ahakikishe mumewe amekunywa sumu yote, lakini ndo' hivyo haikuwezekana.

Sumu ilivuja pale chupa ilipoanguka chini.

Sasa Clint anajikuta ana kibarua kigumu cha kujinusuru humu kaburini tena ndani ya jeneza.

Anatokaje?

Na je akifanikiwa, atakabiliana vipi na balaa linalomngoja nyumbani kwake, mbele ya wauaji wawili walokula njama?


Mzigo unaitwa BURIED ALIVE.

37a66254f4c8de82753e5d9a8a97c60d.png
 
Katikati ya usiku wa manane, mtoto Sophia anaamka baada ya kusikia sauti ya ajabu.

c7d1211c35f3dc7930784aaa2a0bf5e8.png


Anatazama na kuona kabati la chumbani mwake likiwa wazi.

Kwa uoga anamuita mama yake bila mafanikio. Anashuka kitandani kwenda kuangalia kuna nini lakini mara kidogo anasikia sauti ya mama yake ikipiga yowe.

Hivyo upesi anashika korido kwenda kutazama nini kinaendelea chumbani kwa wazazi wake.

Kadiri anavyopiga hatua kusogea ndivyo na kelele inazidi kuongezeka.

Anapofika kabla hajashika kitasa, mlango unafunguka na mara anamwona mama yake akiwa anapayuka kama mwehu huku mwili wa baba yake ukiwa umelala mfu kitandani!

Masaa kadhaa mbele, mwanasaikolojia (bi. Kate) anawasili eneo la tukio na kupokelewa na mpelelezi (McCathy) anayemweleza kisa kilichotokea.

Mpelelezi anasema bi. Hellen, yaani mama yake na Sophia, amemuua mumewe na hivyo sasa wana kazi ya kutazama kama mwanamke huyo anapaswa kupelekwa mahakamani kama mhalifu ama aende milembe kama mgonjwa wa akili.

5127479bb35fe7d8596ff0259ce8d13b.png


Bi. Kate anaingia ndani kutazama na anapoona mwili wa marehemu anashtuka sana.

Mwili huo umekaa kwa namna ya ajabu.

Anapoangaza humu ndani anakutana na karatasi iloandikwa neno moja 'TAKAHASH' na hajui neno hili lina maana gani.

Anaonana na binti Sophia ambaye bado hali yake si shwari sababu ya kushuhudia tukio lile la kutisha.

Binti huyu amejificha chini ya uvungu wa kitanda.

Hataki kutoka huko.

Kate inabidi amfuate Sophia uvunguni ili wapate kuongea.

Kate anajaribu kumuuliza Sophia nini kilitokea usiku.

Anamuuliza ni nani alimuumiza baba, binti anajibu kitu kipya. Anasema aliyefanya hivyo ni MARA.

MARA ni nani?

Kate anamfuata Hellen, mama yake na Sophia, lakini anapomuuliza mwanamke huyo MARA ni nani, ajabu anaishia kupiga ukunga kama mama wa kinyakyusa aliyefiwa na first born.

Ni baadae, hali ikiwa imetulia, Kate anajaribu tena kufanya mahojiano na Hellen ili apate kufahamu,

Nini kilitokea usiku ule wa manane?

Hellen anasema alikuwa kwenye ugomvi na mumewe kwasababu ya usaliti. Bwana huyo alikuwa anachenguliwa na kiuno kichanga cha mtoto wa 2000, na jambo hilo likamuumiza sana Hellen.

Zile habari za wanaume wote ni mbwa zikaanzia hapa.

Ulikosa nini kwangu we mwanaume? Nini ulitaka sijakupatia?

Japo bwana alipambana kuomba msamaha, Hellen hakusikia. Alisisitiza kitu pekee anachotaka ni talaka yake tu.

Sasa usiku huo wakiwa wamelala, Hellen alishangaa kujikuta yu macho, anaona kila kinachoendelea, lakini mwili wake ukiwa bado usingizini!

4b28c6903a79e2db4caf494dcabdded4.png


Hawezi kuusogeza mkono wala mguu. Ni macho tu ndo' yanazunguka huku na kule.

Akiwa katika hali hii ya kupooza, alisikia sauti ya ajabu kisha akamwona pepo aliyemuita MARA akiwa katika umbo lake halisi.

Ushawahi kulala ukahisi kitu kinakukaba shingoni, unatamani kupiga kelele, lakini sauti haitoki?

Unatamani kujiokoa ila mikono imelegea kama tambi, na kila ukijitahidi haujiwezi abadan?

Basi ndo' kazi za huyu mtaalam.

Hellen anasema, kwa macho yake ya nyama, alimwona MARA akikwea kifuani mwa mumewe kisha akamuua kwa kumnyonga na kumvunja shingo kama ufito wa kuni.

Haya maelezo haya-make sense kwa bi. Kate. Anaona mwanamke huyu amechanganyikiwa si bure!

Anaafiki mama huyu ana kesi ya kujibu kama mtuhumiwa wa mauaji ya mumewe na yote ni kwasababu ya wivu wa mapenzi.

Japo Hellen anasisitiza hana makosa. Hajamuua mumewe katukatu. Hamna anayemuelewa.

Anatiwa nguvuni na anatenganishwa na mwanae Sophia kwasababu za usalama.

Baadae usiku, katikati ya usingizi mzito, ghafla afisa Kate anajikuta akiwa macho.

Anajaribu kujisogeza mwili.

Hawezi!

Anajaribu kufurukuta kwanguvu zote ila hamna kitu. Mwili umelala kama maiti inayongoja mwoshaji.

Ni macho pekee ndo' yanayosogea huku na kule. BASI!

Kidogo anamwona kiumbe cha ajabu kimemsimamia kizani.

Akiwa amepaliwa na hofu, anagutuka kwanguvu na kuketi kitako.

Anayatoa macho. Anahema pumzi ya woga.

Kiumbe kile hakipo, kimeshapotea kufumba na kufumbua.

Baadae anatazama karatasi za binti Sophia, karatasi alizozikusanya kule kwenye eneo la tukio la mauaji, anaona mchoro wa kiumbe cha ajabu ukiwa na maneno 'TAKAHASHI KNOWS MORE', yani Takahashi anafahamu zaidi kisha kuna anwani ya makazi fulani ambayo anapanga kwenda kuyatembelea.

Anapofika huko anakuta nyumba pweke.

ed314e6f5f634f680735db2bc4661796.png


Anaita ila hamna mtu anayejibu. Anaingia ndani kutazama, anakutana na mazingira hayaeleweki.

Anapoingia chumbani kukagua, anakutana na mwili ulokufa muda mrefu.

Anashtuka nusura moyo utokee mdomoni.

Polisi wanapofika na kuchunguza, mpelelezi anasema mwili huo haupo kwenye rekodi yeyote ya usajili.

Lakini Kate anajiuliza mbona majeraha ya marehemu huyu ni ya mtindo sawa sawa na yule mume wake Hellen?

Baadae Kate anazungumza na Hellen na mwanamke huyo anamwambia mumewe alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa kupooza usingizini na tatizo hilo lilimfanya ahangaike huku na kule kumsaidia ili apate tiba.

Huko ndo' akakutana na Takahashi na Dougie ambao nao walikuwa wagonjwa kwenye group moja linalosimamiwa na Dokta Ellis.

Hellen anasema siku moja mumewe aliamka akiwa na alama nyekundu jichoni na tangu hapo hakuchukua muda mrefu kuja kupooza na kuuawa na 'Sleep Demon', yani MARA, huku akishuhudia kila kitu.

Hellen anaonyesha jicho lake la kushoto.

Screenshot_20240924-234638.png


Jicho lina alama nyekundu.

Anasema kuwa na yeye ashawekewa alama ya kifo hivyo muda si mrefu MARA atakuja kumuangamiza.

Mbele ya macho ya Kate, mambo haya ni kama miujiza, ni kama hekaya za Abunuwasi, ila kadiri muda unavyozidi kwenda maisha yake yanabadilika katika namna ya kutisha.

Kila siku afadhali ya jana.

Anaanza kuona kiumbe cha ajabu kila akipitiwa na usingizi, na siku moja anapokuja kutazama kwenye kioo, anaikuta alama nyekundu kwenye jicho.

Alama kama ya Hellen!

Sasa anapanick na mbio za kunusuru maisha yake zinaanza kwa kasi.

MARA ni nani na anataka nini kwake?

Na kwanini yeye si watu wengine?

f07787dee53fd440acfbdc8db160290a.png


Wakati huo anapambana kuyasaka majibu ili apate kujiokoa, Kate inabidi akae mbali na usingizi.

Kwani kwake usingizi si kupumzika.

Bali usingizi NI KIFO.

Mzigo unaitwa MARA.

faad96b24379aa4ec0a3039de3491091.png
 
Back
Top Bottom