VITA: Kazi Vs Pesa! Nani ataibuka mshindi?

VITA: Kazi Vs Pesa! Nani ataibuka mshindi?

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Joined
Mar 24, 2018
Posts
28,297
Reaction score
68,017
VITA VYA KAZI DHIDI YA PESA. KAZI Vs PESA

Kwa Mkono wa Robert Heriel

Kazi ni shughuli aifanyayo mwanadamu au kiumbe kujipatia mahitaji yake. Kama vile kilimo, ufugaji, udereva, ualimu, udaktari, ufundi nguo, uchongaji, uongozi, uchungaji, usheikhe, uhakimu, uandishi wa habari miongoni mwa kazi zingine.

PESA/FEDHA
Ni zana au chombo cha ubadilishaji wa bidhaa au huduma kwa watu kwa kutumia sarafu(coin) au Noti(banknotes).
Historia ya pesa imeanza zamani kidogo zaidi ya miaka 5000 iliyopita, ambapo huko Mesopotamia(Iraq ya leo) ambapo walitumia shekel kama chombo cha kubadilishana bidhaa au huduma. Hisoria ya pesa ni ndefu, na sio langu kuieleza hivi leo.

Lengo kuu la Pesa ni kurahisisha mabadilishano ya bidhaa na huduma kwa watu.
Lengo kuu la kazi ni ibada.
Kwani Ibada ni nini?

IBADA
Ibada ni yale mambo yote afanyayo mwanadamu au kiumbe ili aweze kuishi. Mambo hayo sharti yawe hayakinzani na Nature bali yawe katika mfumo sahihi uliokuwepo tayari.
Ibada ni kufikiri, kusema, na kutenda kwa usahihi bila kuathiri viumbe wengine(Nature).

Kiimani, ibada huitwa amri na sheria za Mungu.

Kila kiumbe lazima kifanye kazi ili kiweze kuishi. Endapo kitashindwa kutekeleza ibada hii, basi ni wazi kitaathiri viumbe wengine.
Kutokana zama zimebadilika, kwa sasa watu hufanya kazi ili wapate Pesa waweze ishi vizuri.
Lakini kabla ya kufanya kazi lazima mtu awe na Afya njema kuanzia afya ya kimwili, kiakili, kihisia na kiroho.
Hivyo kama ni hesabu mlinganyo ungeweza kukaa hivi;
Afya(A)+ Kazi(K)= Pesa(P)
{A+K=P}
Afya= ni zawadi kutoka kwa Mungu tuliyopewa tuitunze kwa kufanya Ibada.
Kazi= ni moja ya ibada zinazotusaidia kupata mahitaji yetu ikiwemo pesa ili tutunze afya zetu.
Pesa= Ni zana/chombo kilichotengenezwa na binadamu kinachorahisisha bidhaa(zilizozalishwa au kutengenezwa kupitia kazi) na huduma(zinazotolewa au kupokelewa na watu)huduma ndio kazi zenyewe.

Hivyo katika mambo hayo tunaona kuwa Afya/uhai unatoka kwa Mungu, Ibada(kazi) kile alichotuamrisha Mungu tukifuate, alafu mwisho pesa, ni utashi na ubunifu wa mwanadamu kurahisisha maisha yake.
Anhaa! Kumaanisha mwanadamu anapaswa atumie kile alichopewa na Mungu (Afya ikiwemo) na kufuata yale asemayo Mungu ambayo huitwa ibada(kazi ikiwemo) na kuongezea utashi na ubunifu wake(pesa ikiwemo) ili kurahisisha maisha.

Pesa husemwa ni jawabu la moyo. Pesa ni sabuni ya roho.
Pesa kama ilivyo maana yake isemayo ni chombo cha kurahisishwa ubadilishanaji wa bidha na huduma baina ya watu na kuyafanya maisha kuwa mazuri.

Maisha mazuri ni yapi?
Maisha mazuri ni yale yaliyorahisishwa. Nafikiri jibu hili ni fupi linalojitosheleza. Na moja ya vitu vinavyorahisisha maisha ni pesa.
Pesa ni kama mashine ya maisha.
Tunajua kuwa Mashine ni chombo maalum kinachorahisisha kazi. Mashine kama vile mashine ya kusaga, kukoboa, magari, simu, trekta, meli, ndege, mashine ya kunyolea, kuchakata juisi miongoni mwa mashine zingine.

Halikadhalika na pesa, hurahisisha maisha na kuyafanya kuwa mazuri.
Pesa hununua machine zinazorahisisha kazi(ibada)
Kwa mfano, Mkulima hununua Trekta kulimia badala ya kutumia jembe la mkono.
Wachungaji na masheikhe hutumia vipaza sauti, vitabu vilivyoandikwa kwa mashine kuhubiri na kufundisha neno la Mungu.

Vijana wengi wa zama hizi hukosea na kujikuta katika vita kuu ambapo huishia kushindwa na kupata anguko kuu, kutokana vita walioiweka baina ya KAZI Vs PESA. Jambo ambalo wanajikuta wakichagua upande mmoja na kupuuza upande mwingine badala ya kutumia silaha zote tatu kuyafanya maisha yao kuwa mazuri.

Afya, kazi na pesa ni silaha zinazopaswa kutumiwa zote kwa pamoja vizuri ili kuyafanya maisha yawe mazuri.
Kupuuza kimojawapo ni kutengeneza anguko kuu ambalo lazima litaharibu maisha yetu.

Wapo vijana waliojikita katika kupenda kazi na kutukana pesa kuwa sio lazima. Watu hawa husema KAZI NI UTU, wanachoshindwa kuelewa ni kuwa Pesa ni chombo kinachorahisisha na kuufanya utu wa mwanadamu uwe bora zaidi.
Wafuasi wa KAZI wamejikuta wakifanya kazi na maisha yao yakiendelea kuwa mabaya sana, wakichoka na kunuka kama maiti wangali hai wanatembea.
Kundi hili lina mtazamo zaidi wa kizamani, ni wale wenye mtazamo wa kizamani kuwa maisha ni mazuri bila hata ya pesa.
Pia kundi hili linaathari kutoka katika imani za kidini, kwani wengi huamini kuwa kazi ni ibada(kweli kabisa) lakini shida ni kuiona pesa ni shetani, na kuona utajiri ni kosa.

Kundi la pili, ni WAFUASI WA PESA, hawa ni wanausasa.
Hili ni kundi linaloamini pesa pekee ndio inaweza kuyafanya maisha kuwa mazuri hata bila ya kufanya KAZI.
Kundi hili linashikiliwa zaidi na kizazi cha sasa watoto wa karne ya 21. Hawa huona pesa ndio kila kitu kwani ndio huleta maisha mazuri.
Kundi hili linachoshindwa kuelewa ni kuwa Pesa imetengenezwa na mwanadamu, pesa ni matokeo ya ubunifu wa mwanadamu.
Kuitegemea pesa pekee ni kutegemea akili, ubunifu wa binadamu pekee bila kutegemea Mungu.
Wakati KAZI ni ibada yaani amri ya mwenyezi Mungu, kutegemea kazi ni kumtegemea MUNGU kwani yeye ndiye aliyesema ufanye kazi.

Lakini wapo ambao hupenda kazi na kupenda pesa pia, na kuidharau Afya waliyopewa ambayo niyathamani kuliko pesa. Hujikuta wakibadili mitindo ya maisha yenye kuharibu afya zao, kama vile ulaji mbaya, unywaji wa vilevi vinavyoharibu afya ya mwili na akili, kufanya zinaa na kujikuta wakipata magonjwa ya zinaa n.k

Jambo moja la msingi ni kuacha kuingia katika vita vya maisha yako kwa kuchagua upande mmoja kati ya Afya, Ibada(Kazi ikiwemo) na pesa bali ili tuishi kwa amani basi hatuna budi kuchagua yote kwa pamoja.

Athari za kuchagua pesa pekee zipo nyingi sana na zinajulikana kwa wengi, mathalani
1. Kuongezeka kwa uhalifu kwani watu huweza kufanya kazi zinazodhuru binadamu wenzao na viumbe wengine. Kama vile biashara ya ukahaba, uuzaji wa madawa ya kulevya, uuzaji wa viungo vya binadamu, ujangili n.k

2. Vijana kuchelewa kuoa/na mabinti kuchelewa kuolewa
Moja ya athari za kuchagua pesa pekee ni pamoja na watu kuoa/kuolewa wakiwa na umri mkubwa, wakiwa wamezeeka. Kwa maana mtu mwenye miaka 30 tayari ni mzee kwa habari za mahusiano.
Vijana wanaogopa kuoa kwa sababu hawana pesa, na wanawake hawataki kuolewa na vijana wasio na pesa.
Vita hivi huleta athari katika taasisi ya ndoa.
Wakati kama kazi na pesa(bila kujali ni ndogo au nyingi) zingezinngatiwa basi watu wangeoa na kuolewa katika umri sahihi kabisa yaani 18 - 30

3. UKOSEFU WA AJIRA
Moja ya athari mbaya ambayo wafuasi wa pesa wanaipata ni ukosefu wa ajira. Ukishapenda pesa zaidi ya kazi utajikuta katika tatizo la kudharau kazi zisizo zalisha kipato kikubwa. Ukishadharau kazi hizo alafu muda huo huo kazi zenye vipato vikubwa ni chache utajikuta hauna ajira iwe ya kujiajiri au kuajiriwa. Kitakachotokea ni kuwa hauna ajira na wala hauna pesa. Hence huna UTU kwani kazi ndio inayokupa utu wako, na pesa ndio hurahisisha na kuufanya utu wako kuwa bora.

Kufikia hapa nadhani nimeeleweka kwa sehemu kubwa. Kwa wasionielewa basi tukutane wakati mwingine. Au waweze nicheki kwa mawasiliano hapo chini.

Ulikuwa nami;

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
0693322300
Kwa sasa Morogoro
 
Back
Top Bottom