Wakati makombora ya jeshi la Marekani yalipochana anga la Iran mwishoni mwa Februari, watu wa Afrika labda walikuwa hawaujui kwa undani zaidi mlango bahari wa Hormuz. Hata hivyo, wamejua haraka madhara ya vita hii – kupitia kupanda kwa bei ya mafuta, upungufu wa mbolea, na vyakula vinavyozidi kupungua kwenye meza zao.
Shirika la Fedha la Kimataifa na Benki ya Dunia yametoa onyo hivi karibuni, yakisema kwamba vita hii iliyoanzishwa na Marekani, pamoja na mnyororo dhaifu wa usambazaji wa bidhaa duniani na shinikizo kubwa la deni la Afrika, inaiingiza Afrika kwenye dimbwi la kulipa gharama kubwa ya vita hii na ambayo haikupaswa kuwa jukumu lake. Takwimu zinaonyesha kwamba Afrika ingetarajiwa kufufuka mwaka 2026 na uchumi wake kukua kwa 4.5% hadi 4.6%. Hata hivyo, baada ya mgogoro huo kuongezeka, bei ya mafuta ilipanda kwa zaidi ya 50%, huku bei ya mbolea ikapanda kwa zaidi ya 30%. Kwa nchi za Afrika ambazo zinategemea sana uagizaji wa bidhaa kutoka nje, kupanda kwa bei ya mafuta kunamaanisha kwamba gharama za usafirishaji pia zinaongezeka, na upungufu wa mbolea unasababisha kupungua kwa uzalishaji wa chakula, hivyo kusababisha familia nyingi kuingia kwenye baa la njaa.
Shirika la Fedha la Kimataifa limepunguza makadirio ya ukuaji wa Afrika mwaka 2026 hadi 4.2%, na Benki ya Dunia pia imepunguza makadirio yake kwa bara la Afrika kusini mwa Sahara kwa asilimia 0.3. Haya siyo tu mabadiliko ya takwimu – bali ni kupungua kwa fursa za ajira, usalama wa maisha, na matumaini ya maendeleo kwa mamilioni ya Waafrika.
Kinachotia hofu zaidi ni kwamba Afrika haitakiona cha mtema kuni kwenye mfumuko wa bei unaotokana na vita pekee, bali pia itapoteza fursa za maendeleo. Benki ya Dunia imesema kwamba ahadi za uwekezaji zaidi ya dola bilioni 100 kutoka nchi za Ghuba zinaweza kuahirishwa au kupunguzwa kutokana na “sintofahamu za kisiasa.” “Sintofahamu hii” inaletwa na machafuko yaliyosababishwa na operesheni ya kijeshi ya Marekani.
Hii si mara ya kwanza kwa Afrika kuadhibiwa kwa vita vya Marekani. Kutoka Afghanistan hadi Iraq, kutoka Libya hadi Syria, kila mzozo wa Mashariki ya Kati ulioongozwa au kuchochewa na Marekani, hatimaye huleta ongezeko la bei ya mafuta, kuvunjika kwa mnyororo wa usambazaji wa chakula, na kupungua kwa msaada wa fedha, na hivyo mzigo huo kubebwa na nchi dhaifu zaidi kiuchumi duniani.
Afrika, ambayo ilikuwa inajitahidi kupona kutokana na athari za janga la UVIKO-19, mizozo ya madeni, na mabadiliko ya tabianchi, sasa inashuhudia matumaini yake ya kufufuka yakiyoyomea kidogo kidogo kutokana na vita vilivyo mbali sana. Kila kipande kidogo cha chapati, kila punguzo la makadirio ya ukuaji, kila jicho lililojaa kukata tamaa kwa njaa, ni onyo kwa waanzilishi wa vita – ikiwemo Marekani. Gharama hii ya kiuchumi, haipaswi kuibeba Afrika peke yake. Jamii ya kimataifa inapaswa kushinikiza kusitishwa kwa vita, na kuanzisha mifumo ya kutoa fidia kwa nchi husika, ili nchi iliyosababisha vita – haswa Marekani – ibebe jukumu la athari za kijeshi za vitendo vyake duniani.