Vita vya Kagera: Historia yangu - Sehemu ya kwanza

Vita vya Kagera: Historia yangu - Sehemu ya kwanza

Inabidi sasa mumlipe afande japo kidogo!
Duhh wabongo kwa kupenda dezo!?!

We mtu kasota uganda kule! Sasa hivi kawaonjesha tu kidogo! Mnataka na part 2 bure! Lkn vitabu vya udaku mnanunua ma alfu!
Nimeona sapoti nyingi sana humu watu wanazompa afande! Lkn hakuna hata mbongo mmoja akatoa hata ushauri wa kumkatia chochote afande kama asante kwa kupigania nchi yenu!

Oovyoo!
Mtabaki tu!

Safi sana afande!
We ndio mwenyewe afande! Umenipa raha sana afande!
Lkn kitu kidogo!? Mnapeleka uwanja wa fisi!! Usiku!

Mhhhh! Acheni ubakhili nyie!

Heri yako uliyemchangia afande.
 
Toeni hela tumbembeleze afande!
Bure siku zote ni ghali!! Ubakhili waachieni wahindi!! Na waparokia!

Leo nilikuwa nimechefuliwa hapa home, lakini niliposoma post zako nimecheka mpaka moyo umelainika.
 
Huu ndio umuhimu wa JF,bila jukwaa hili vijana wa leo wangepataje taarifa kama hizi? Historia kama hizi ni muhimu mno na mbaya zaidi hata ukigoogle hupati habari za kutosha lakini sasa kupitia JF walau kutakuwa na source ya kuaminika yenye taarifa nyeti za historia ya Taifa hili.

Naunga mkono wazo la kuandika kitabu,kama kitabu cha mpango wa kumkamata Osama tayari kimetoka kwanini tunashindwa kuandika historia zetu hizi zinazotufanya tujisikie fahari kuitwa Watanzania?

CC Invisible
 
Last edited by a moderator:
Mkuu MTAZAMO

Ni kweli kabisa leo ukitafuta profile za mashujaa wetu huwezi kuzipata hata ukitumia google unaambulia zero lakini utashangaa ukitafuta profile za makamanda wa jeshi la Rwanda au Uganda zimejaa tele sasa sijui ni ugoigoi wa kitengo cha mawasiliano cha JWTZ wa kuzuia habari kama wanavyofanya katika operesheni ya DRC.
 
Last edited by a moderator:
Kama nilivyoelezea katika sehemu yangu ya kwanza nilifika kwenye uwanja wa vita tarehe 03-11-1978 hali ya mambo ilikuwa ngumu sana hasa kwangu binafsi pamoja na Wanajeshi wengine maana kipindi hicho mipango ya Vita ilikuwa haijapangwa na makamanda wetu,Na siku hiyo hiyo ya Tarehe 03-11-1978 ndipo lile Daraja la mto Kagera lililipuliwa na kukatika kabisa hivyo kulifanya Jeshi letu lisiweze kupitisha zana zile nzito kama vile Vifaru na mizinga mizito vilevile hata Magari hayangeweza kupita hapo, Kitu ambacho tulikuwa tunafanya ni kulinda himaya yetu kwa maana ya eneo lililopo mikononi mwetu na kukusanya habari za kijasusi na zaidi ya yote kujipanga vizuri kadri Wanajeshi wetu walivyokuwa wanaongezeka kwenye uwanja wa vita maana kila siku Wanajeshi wetu walikuwa wanakuja kujiunga nasi kwenye Uwanja wa Vita toka mikoa yote ya Tanzania.Kipindi hicho eneo lote la kaskazini mwa mto Kagera lilikuwa mikononi mwa majeshi ya Idd Amin.

Tarehe 04-11-1978 Maandalizi makubwa yalikuwa yanaendelea kwa kasi kubwa na kikosi cha vifaru kilikuwa tayari mstari wa Mbele kuhami maeneo yetu na tayari kuanza kuyakabili Majeshi ya Amin kama yangeamua kuendelea kushika maeneo mengine, juhudi kubwa ziliwekwa kwenye ulinzi wa maeneo tuliyokuwa tunayashikilia na wakati vifaa na wapiganaji wengine kutoka nyuma wanazidi kumiminika kwenye uwanja wa mapambano kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania wapiganaji waliokuwa wako Kyaka tayari walikuwa wanajishughulisha na matayalisho ya mapambano ilikuwa na pamoja na kufanya kazi ya Utafiti kuhusu ukubwa wa jeshi la adui,silaha alizonazo,sehemu aliyojichimbia na tabia zake za kila siku,Mimi pamoja na vikundi vingine vya doria vya jeshi la Tanzania,kwa siri na tahadhari kubwa tulijipenyenza na kuingia katika eneo la misenyi lililokuwa linakaliwa na wanajeshi wa Amin tulivuka mto kagera kwa mitumbwi iliyoachwa na wavuvi ambao wakati huo walikimbia vita.

Kazi iliyotupeleka huko ni kupeleleza ili kujua tabia za kila siku za jeshi tunalopambana nalo ni jambo la msingi maana linakuwezesha kuelewa ni muda na saa gani ulishambulie jeshi hilo yaani wakati unahisi halikujiandaa vyema kimapigano, Kazi ya vikundi vya Doria inakuwa ngumu na ya hatari zaidi kuliko hata ile ya kushiriki katika mapigano.hii ni kwa sababu pamoja na kumnyatia na kumjongelea adui kwa kawaida vikundi vyetu vilikuwa ni vidogo vyenye askari wasiozidi 30 na tulikuwa tumebeba silaha ndogo ndogo tu ukilinganisha na ukubwa wa jeshi lililoko kwenye ngome ambalo ndilo tulikuwa tunalinanyatia, na mara nyingi vikundi vyetu tulikuwa tufanya kazi ya Doria kuanzia saa za Magharibi mpaka usiku kabisa chini ya lindi la giza ili kupunguza uwezekano wa kuonwa na adui tunapomkaribia adui vikundi vyetu huhakikisha havitoi sauti na havisababishi mitikisiko mikubwa ambayo itamgutusha adui na kumfanya awe macho kuimaimarisha ulinzi, kwa hiyo hata wakati wa kutembea wakati wa kufanya kazi hiyo, inabidi ufanyike kwa makini na uangalifu mkubwa huku pia kukiwa na wasi-wasi wa kupambana na kikundi cha adui cha aina hiyo hiyo ambacho nacho kimetumwa upande unakotoka,pia vikundi hivyo vinakabiliwa na jukumu la kuwa macho sana hasa wanapoikaribia ngome ya adui la sivyo vinaweza kuingia katika Bustani iliyopandwa mabomu tayari kuangamiza adui yoyote anayekaribia ngome, tulimaliza kazi yetu na kuanza kurudi kambini kwetu na tulivuka tene mto kwenye mda wa saa nane usiku na ilikuwa bahati mbaya tulipoteza askari wetu wawili lakini kazi yetu ilifanikiwa vizuri sana maana wakati tulikuwa tunafanya Doria yetu saa sita usiku tulipambana na Doria nyingine toka Jeshi la Amin ambao walikuwa kwenye Jeep waliweza kutoroka na kuacha lile gari pamoja na Radio ya mawasiliano kwa ujumla kazi hiyo ya Doria iliyawezesha majeshi ya Tanzania kujua kwa uhakika yalipo majeshi ya Amin katika sehemu ya Misenyi kwa hiyo ikafanya iwe rahisi mizinga ya Majeshi yaTanzania kushambulia kwa uhakika ngome za majeshi ya Amin ng`ambo ya mto Kagera.

Tarehe 05-11-1978 Ndiyo siku majeshi ya Tanzania yalipoanza rasmi kazi ya kuyarudisha nyuma na kuyatoa majeshi ya Amin katika eneo la Misenyi.siku hiyo majeshi ya Amin yalinyeshewa mvua kali ya mabomu yaliyotoka katika majeshi ya Tanzania na baada ya majibizano makali majeshi ya Amin kwa kuzidiwa yalianza safari kurudi nyuma hadi Igayanza kilomita kama 20 hivi kutoka daraja la Kyaka Kitendo hicho cha majeshi ya Amin kurudi nyuma kuliyawezesha majeshi ya ya Tanzania kujenga daraja dogo la awali lililokuwa linaelea majini daraja lililoweza kuvusha magari ya uzito wa tani 12 kwa wakati mmoja.

Kujengwa kwa daraja hilo dogo na rahisi kwanza kulikuwa mhimu kwani madhumni yake ilikuwa kuziwezesha Brigedi za Tanzania kuvuka mto kagera na kuweka ulinzi ng`ambo ya pili yake ili ujenzi wa Daraja kuu la Kyaka liweze kufanyika, Brigedi zote tatu zilipovuka zilipewa kila moja uelekeo wake na ulinzi, ,Ikumbukwe hapa kuwa kazi ya kuyatoa Misenyi majeshi ya Amin ilifanyika kupitia njia zilezile ambazo majeshi ya amin yalitumia kulivamia eneo hilo wakati huo Meja Jenerali kiwelu na wataalamu wake wa mambo ya mbinu na upangaji wa vita yaani Kanali Mohamed kitete na luteni kanali Yusuph Abdalah walikuwa na makao yao Nyakimbimbiri lililoko kiasi cha kilomita 30 hivi toka Daraja la Kyaka.

Mnamo 15 -11-1978 huku vikundi vya doria vikiendelea na kazi ya kukusanya habari toka maeneo mbali-mbali Mizinga ya Tanzania iliyashambulia tena maeneo yaliyokuwa yanakaliwa na majeshi ya Amin mashambulizi ambayo yalifanikiwa sana kuyarudisha nyuma majeshi ya Amin kutoka Igayanza hadi Kabwoba matokea ya shambulio hilo la Mizinga yalikuwa kukombolewa nusu ya eneo la Misenyi katika eneo hilo lililokombolewa mauaji uporaji wa mali na uharibifu mali na mimea pamoja na ubakaji ndiyo picha ilikuwa imeachwa na majeshi ya Amin.

Siku hiyo hiyo ya 15-11-1978 hali katika uwanja wa Vita ilibadirika kabisa hasa baada ya Majeshi ya Amin kuzidiwa katika Nyanja zote majeshi yetu yaliendelea kuyashambulia majeshi ya Amin usiku na Mchana hatimaye Tarehe 25-11-1978 hadiTarehe 28-11-1978 Majeshi ya Amin yalikuwa yamefukuzwa kabisa toka ardhi ya Tanzania na majeshi hayo yalijikita katika maeneo ya mpakani ya Mtukula,Minziro na Kakunyu upande wa Uganda.
KRISMAS 1978.

Nilisherehekea Christmas nikiwa Minziro wakati huo Joto la kimapigano lilikuwa limepanda sana wengi wetu tulikuwa tunafurahia kuyafukuza majeshi ya Amin nchini mwetu na wengi wetu tuliamini tutarudi nyumbani na wachache watabaki kulinda mipaka yetu,kadri siku zilivyokuwa zinasonga mbele vivyo hivyo Joto la kuzuka vita lilikuwa linapanda sana kuashiria kuwa vita bado mbichi kabisa na mipango ya kuyafuatilia majeshi ya Amin huko huko yalikoilikuwa tayari imeshaanza kuandaliwa na Makamanda tayari kwa kutoa kipigo cha awamu ya pili maana awamu ya kwanza ilikuwa kuyatoa majeshi ya Amin nchini na awamu ya pili ilikuwa kuyapa adhabu kidogo.

Eneo la Uganda katika mpaka wake na Tanzania ni zuri zaidi Kijeshi (strategic) kuliko lile la Tanzania kwa sababu lile la Uganda liko katika miinuko mikali na kwa hiyo liko juu na lile la Tanzania liko Bondeni,kwa hiyo askari wa Amin ambao sasa walikuwa wamejichimbia katika miinuko((strategic) hiyo walikuwa wanamiliki Ki-Mapigano eneo karibu kilomita 10 mpaka 15 ndani ya Tanzania,Kutokana na hali hii mimi naamini ilisababisha mkondo wa Vita ubadirike badala ya kuishishia kuyatoa majeshi ya Amin kwenye ardhi yetu ikapelekea kuyafuata huko huko yaliko yaani Uganda,Eneo hilo la mpakani na Uganda Kijeshi liko((strategic) kimbinu yaani ina maana kuliachia eneo hilo ni sawa na kujitoa mhanga,Maana ingekuwa Majeshi ya Amin yakiwa kwenye vilima hivyo ndani ya Uganda yanaweza kupiga mizinga yao ndani ya Tanzania bila wasi-wasi wowote hivyo kuishia mpakani kwa majeshi ya Tanzania Kijeshi ingekuwa kama kujitoa mhanga.

Hali kama hii tunaweza kuiona hata nchi nyingine zimeweza kushikilia eneo la Kimbinu (strategic) mfano tunaweza kuona Israel toka ilipoliteka eneo la milima ya Golan toka Syria mpaka sasa hivi hawajaliachia ni kwa sababu liko kwenye Mwinuko wao wanaamini kama wakiwakabidhi Syria eneo hilo basi watakuwa wamepoteza eneo mhimu la Kimbinu la kilomita 20 na zaidi ndani ya Israel litakuwa linamilikiwa kijeshi na Syria, Kwetu sisi hali hii binafsi niliamini pamoja na mambo mengine ilibadirisha Mwelekeo wa vita badala ya kukomea mpakani ikawa kusonga mbele kukabiliana na Adui.

Majeshi ya Tanzania baada ya kuyatoa Majeshi ya Amin ndani ya nchi yetu Majeshi yetu yalijijenga katika maeneo ya Kabwoba,Minziro na Kakunyu kiasi cha kilomita kumi toka mpakani yalipo majeshi ya Amin katika sehemu hizo Majeshi yetu yalikaa mpaka 22-01-1979 ambapo uamuzi ulitolewa wa kusonga mbele ili kuyaadhibu Majeshi ya Amin kama nilivyoeleza katika sehemu ya kwanza Makamanda walikuwa tayari wamekabidhiwa majukumu ya kufanya yaani nani aelekee huku na nani aende huko Makamanda wetu walikuwa wamejipanga kama Ifuatavyo;

Luteni kanali R.R.Rajab alipewa jukumu la kusimamia ujenzi wa Daraja la mto KAGERA maana yeye alikuwa kamanda wa Uhandisi.Kitu cha kwanza ilikuwa kujenga Daraja la mda ambalo lilijengwa usiku na mchana na lilipokamilika lilianza kutumika mara moja lilikuwa na uwezo wa kupitisha magari ya kijeshi na zana zingine za kivita.

Meja Jenerali T.N.Kiwelu kamanda wa kwanza aliyepewa jukumu la kuyaongoza mapambano ya kuyasukuma nyuma Majeshi ya Amin toka Kagera Kiwelu ndiye aliyekusanya nguvu kubwa za awali ambazo ndizo zilizomng`oa Idd Amin katika eneo aliloliteka kazi hii ilikuwa ngumu sana lakini aliifanya kwa utulivu hatimaye akapanga mipango madhubuti iliyowezesha Majeshi ya Amini kuondolewa kabisa katika ardhi ya TANZANIA.

Meja Jenerali Mwita Marwa(Jenerali Kambale) alikuwa mkuu wa Brigedi iliyopewa jukumu la kuelekea uelekeo wa Mtukula na kuelekea Igayanza.Marwa alikuwa Mkuu wa brigedi ya 208,alishirikiana na Brigedi za 201 na 207 katika kuuteka mji wa Kampala Jinja Mbale na Moroto.

Meja Jenerali Silas Mayunga(Mti Mkavu)Ndiye aliyeyaongoza Majeshi ya TASK-FORCE yaliyokuwa uelekeo wa Kakunyu,Kasumba,Gayanza,Mbarara Bshenyi,Kasese,Fort-portal,Hoima,Masindi,Pakwachi,Arua,Koboko alikozaliwa Idd Amin mpaka Oraba mpakani na Sudan.

Brigedia Walden(Black Mamba)Ndiye aliyeongoza Brigadi ya 207 yeye alichukua uelekeo wa Minziro mpaka Katera baada ya kuweza kumshinda adui maeneo hayo alijiunga tena na uelekeo wa Mtukula kuanza safari ndefu ya kuyachapa majeshi ya Amin hadi kukamata Kampala baadaye alipewa jukumu la kulinda mji mkuu Kampala na vitongoji vyake.

Brigedia Helman Lupogo alikuwa anaongoza na kuamrisha Brigedi ya 205 kutoka mpaka wa Tanzania na Uganda hadi eneo la Sembabule baadaye alipewa kazi nyingine maalum na badala yake alipewa Brigedia Kimario.

Brigadia Muhidini Kimario(Kamanda Mbogo)yeye alichukua uongozi wa Brigedi ya 205 katika eneo la Sembabule kutoka kwa Brigedia Lupogo ambaye alipewa shughuli nyingine mhimu,Brigedia Kimario aliongoza Brigedi hii kuanzia Sembabule hadi Masindi na kuelekea Guru,alipambana vikali sana na Adui katika eneo la Sembabule,Hoima na Masindi.

Brigedia Imran Kombe(Brigedia Ngono) yeye alikuwa kamanda wa Brigedi ya 201 ambaye alishirikiana na Brigedi ya 207 na 208 waliweza kuuteka mji mkuu wa Uganda ikumbukwe kuwa Brigedi ya 201 ndiyo iliyopambana vikali sana na majeshi ya Amin katika mji wa Lira na kuua askari wa Amin zaidi ya 200 na kuteka silaha nyingi sana za Adui,Baada ya hapo Brigedi hiyo ya 201 ilijikusanya katika mto Ngono na kusonga mbele mpaka Adjumani kama maili hamsini kutoka mpaka na Sudan.

Brigedia Yusuph Himid naye alikuwa wa kwanza kwanza kupambana na majeshi ya Amin mwezi October 1978.

Brigedia Haji aliongoza Brigedi ya Kagera katika mapambano jukumu lake kubwa lilikuwa kulinda maeneo yote ya nyuma yaliyotekwa na majeshi yetu,pia Brigedi yake ilipewa jukumu la kuyafundisha majeshi ya Uganda Huru.

Kanali Kitete(Supersonic) yeye alikuwa Mkuu wa shughuli za Utendaji Kivita yaani Mkuu wa mipango Uamrishaji Kivita katika Division ya 20 baadaye aliteuliwa kuwa Brigedia wa muda na aliongoza Brigedi ya minziro iliyomchakaza nduli sehemu za Bushenyi,Kasese,Fort-portal,Hoima,Masindi,Karuma Falls,Pakwachi,Bondo,Arua,Yumbe hadi Moyo mpakani na Sudan.

Kanali Tumbi(Kamanda Radi) yeye alikuwa Mkuu wa kikosi cha Mizinga ya masafa marefu BM.

Brigedia Makunda(Kamanda Torpedo)alichukua uongozi wa Brigedi ya 206 na kuiongoza kuanzia miji ya Mbarara,Fort-portal,Hoima,Masindi,Karuma Falls,Pakwachi Bondo,Arua,Koboko,Oraba mpakani na Sudan.

Brigedia Mboma-Kamanda mkuu wa ndege za kivita-Tanzania uongozi wake mzuri na kazi yake kubwa aliyoifanya katika Vita haina budi kupongezwa daima.
Kanali Bayeke alikuwa anaongoza na kuamrisha kikosi cha askari wa miguu Mstari wa mbele eneo la Minziro.

Meja Jenerali David Msuguri (Jenerali Mtukula)Kamanda aliyeamrisha Mapambano ndani ya Uganda alikabiliwa na kazi nzito ya kuyaongoza na kuyaamrisha Majeshi ya Tanzania na yale ya Umoja wa kuikomboa Uganda yapatayo zaidi ya wapiganaji 40,000 pamoja na zana za kivita
Brigedia M.N.Mwakalindile wakati wote wa vita alikuwa Kamanda mkuu wa mafunzo ya vita COT katika Jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania alifanya kazi kubwa mno ya kuyahusisha majeshi ya nyuma nay ale yaliyoko mstari wa mbele pia ndiye mwenye kuweza kuyaendeleza mafunzo yote ya mbele na nyuma katka vita.bidii yake katika kuipenda kazi ilianza tangu zamani akingali katika uongozi wa kati aliweza kukutana na makamanda wa vikosi imara na kuwapa mawazo na mbinu kamambe kuhusu matumizi ya silaha kubwa.



Luten kanali D.N.Nsimanyi aliyekuwa kamanda wa kikosi cha 20 cha askari wa miguu Infrantry alionyesha uongozi wa kishujaa ulioweza kukiongoza kikosi chake kujikwamua katika mtego Ambush ambayo ingewamaliza yeye na askari wake wote lakini aliweza kupambana kiume hatimaye majeshi ya Task force kufika kuwaokoa yeye na kikosi chake katika mapambano ua Umrwekubo kadri vita vilivyokuwa vinasonga mbele vilevile vita ndiyo ilikuwa kali kabisa hasa kabla ya kuuteka mji mkuu wa Uganda Kampala.

Tarehe 20-01-1979 Brigedi ya Mayunga ambayo ilikuwa katika milima ya Kakunyu,magharibi kabisa ya Tanzania iliingia Uganda na kukalia vijiji vya kasasa,Mrema na Kikagati vilivyoko mpakani,Brigedi hiyo iliyaburuza majeshi ya Amin na kuyasukuma nyuma na kwa hiyo kuwa Brigedi ya kwanza ya Tanzania kuingia Uganda na kukalia ardhi ya nchi hiyo.huo ulikuwa ni mwanzo tu wa uwanja wa vita kubadirika toka Tanzania hadi Uganda.

Tarehe 21-01-1979 baada ya mapigano makali na majeshi ya Amin Majeshi yetu yaliweza kuzikamata ngome zilizokuwa zinashikiliwa na Adui za Minziro na Mtukula na hivyo kuhakikisha kuwa sehemu zote zilizokuwa zimekaliwa na zimekombolewa kazi iliyokuwa mbele yetu ilikuwa kutoa adhabu kwa Mvamizi ndani ya Uganda kupitia Kakunyu,Mtukula na Minziro.

Tarehe 22-01-1979 ilikuwa siku mhimu sana katika vita hii wapiganaji waliandaliwa vizuri kihamasa ili kuweza kushinda katika vita ambayo ingekuwa ni kipimo cha sisi kusonga mbele au kurudishwa nyuma kwetu sisi kuichukua Kakunyu,Mtukula na Minziro lilikuwa jambo la Mhimu Kivita maana kushindwa kuichukua miji hiyo kungemaanisha udhaifu katika mipango yetu ya Ki-vita hivyo mikakati kamambe ilipangwa ili kuweza kuichukua miji hiyo toka majeshi ya Amin.

Asubuhi yake saa kumi usiku vikosi vya Mizinga vikiongozwa na Kanali Tumbi vilianza kurusha makombora kuelekea ngome za Adui za Mtukula na Minziro wakati huohuo askari wa miguu walikuwa wakisonga mbele pamoja na vifaru pamoja na Wahandisi wa Medani chini ya msaada wa mapigo ya mizinga,Kufikia asubuhi saa kumi na mbili Mizinga ilisimamisha kipigo na kuwaachia askari wetu wa Miguu pamoja na vifaru kuingia katika ngome hizo, Mapambano yalikuwa makali sana na yalikuwa magumu kwa sababu Amin aliweka askari wake kipindi kirefu hivyo walikuwa wamejijenga sana na kurundika silaha nyingi pamoja na hayo yote askari wetu waliweza kuwashinda na kuteka silaha zao nyingi sana baada ya masaa mawili ngome za Adui zote zilikuwa zimetekwa na Amin alipoteza askari wake wengi pamoja na ndege ya Kijeshi Mig 21 iliyokuwa inarushwa na Kapten Atiku kuangushwa na yeye Rubani kufa baada ya kuwasumbua kwa kipindi kirefu Kapten Atiku alikuwa Rubani alikuwa anaujuzi wa hali ya juu sana alijua namna ya kuirusha ndege yake aliweza kufanya Acrobatics za ajabu sana lakini siku hiyo alifikia mwisho wake.Kuanzia siku hiyo Mtukula na Minziro ilikuwa mikononi mwetu.

Siku hiyo hiyo ya 22-01-1979 yaani kama siku mbili tu baada ya Brigedi ya Mayunga kuingia Uganda,Brigedi mbili zaidi ziliingia nazo ndani ya Uganda Brigedi zilizoingia ni ya Marwa na Walden katika pambano ambalo liliwadhihirishia wa-Tanzania kuwa Uwezo wa kumpiga Amin wanao,pambano hilo wachunguzi wa mambo wanasema lilikuwa kipimo cha nguvu kati ya majeshi hayo mawili yaliyokuwa yanapambana Brigedi ya Tanzania ilikuwa inakabiliana na Adui iliyeko Mtukula ilikuwa ile iliyoongozwa na Mwita Marwa na ile iliyomkabili adui kwa upande wa Minziro iliongozwa na John Walden,Baada ya askari wa miguu wa brigedi hizo kufika katika maeneo yao ya kuanzia mapigano huku mapigano makali ya mizinga na vifaru yakiwa yanaendelea,askari hao walianza mashambulizi ya kuzivamia ngome za Amin katika miinuko ya Mtukula na Minziro ndani ya Uganda,mapigano ya ana kwa ana kati ya wapiganaji wa majeshi ya Tanzania na yale ya Amin yalizuka kila upande ukusaidiwa na mizinga na vifaru.

Ilipofika saa 12 asubuhi majeshi ya Amin yalikuwa yamezidiwakwa mapigo na kurudi nyuma kwa kukimbia bila mpango huku yakiwa yameacha nyuma vifaa tele vya kijeshi na kupoteza askari wasiopungua 50 kwenye maeneo ya Mtukula na Minziro peke yake navifaa vya kijeshi vilivyotekwa ni pamoja na vifaru viwili aina ya T-54 na magari ya Deraya tisa maroli manne Landrover tatu na jeep tatu zikiwa zimefungwa mizinga ya mm 106 na 160 na vifaa vilivyoteketezwa ni pamoja na vifaru viwili magari manne ya Deraya na lori moja.

Ikumbukwe kuwa kabla ya kufanyika kwa shambulio hilo la mpakani lililoyawezesha majeshi ya Tanzania kuingia Uganda kulitokea mabadiliko ya viongozi wawili wa vyeo vya juu katika Jeshi la Tanzania kwenye uwanja wa mapambano.

Meja jenerali kiwelu alirudi kuendelea na kazi yake ya mkuu wa utawala jeshini na nafasi yake ikachukuliwa na Brigedia na Brigedia David Msuguri ambaye wiki moja tu baada ya kuchukua madaraka ya mkuu wa uwanja wa Mapambano hapo tarehe 05-01-1979 alipandishwa cheo kuwa Meja Jenerali.

Baada ya kuziangamiza ngome za Mtukula na Minziro mapambano yaliendelea ndani ya Uganda,Mapigano yalikuwa makali sana katika baadhi ya miji na vijiji katika eneo la Uganda magharibi Adui alijenga vituo vikubwa katika ziwa Nakivali ambako hasara kubwa ilitokea kwa pande zote mbili tuliweza kupoteza askari pamoja na vifaa lakini hili halikutuvunja moyo,Vifaru vyetu viliweza kuingia katika ngome ya Adui katika ziwa Nakivali na kumng`oa lakini kabla ya kumng`oa ilihitajika msaada maana kabla ya msaada vikosi vyetu vya miguu vilikuwa vimezuiwa visisonge mbele.

Kikosi cha Luten kanali Nshimanyi kilikuwa mbele katika mapambano ya kuelekea ziwa Nakivali,kazi ilikuwa ngumu lakini chini ya uongozi wake shupavu aliweza kuwakwamua wapiganaji wake katika mtego hatari wa adui,Majeshi ya Amin yaliweka Ambush katika kijiji cha Umurwekubo karibu sana na ziwa Nakivali eneo hilo ki jiografia lilikuwa zuri sana kwa adui kwa sababu ya miinuko na mabonde yaliyokuwa mikondo pekee ambayo tungelipitia,Kikosi cha 20 kikiongozwa na Luten kanali Nshimanyi kilisonga mbele toka saa 12 asubuhi kwa madhumni ya kupambana na maadui,Mnamo saa tatu asubuhi tulikutana na maadui wakaanza kutupiga kwa mabomu na mizinga ya 106mm na vifaru toka masafa marefu,nia yao ilikuwa ni kutuchelewesha kuwakaribia, Kikosi kiliendelea kusonga mbele na kumsukuma nyuma adui toka katika eneo lake la ulinzi wa mbele(screen)Kikosi cha Makao makuu ilibidi kiingilie kwa madhumni ya kusaidia uongozi wa kombania za mbele na kuwahamasisha wapiganaji,Luten kanali Nshimanyi mkuu wa kikosi mwenyewe alikuwa katika kombania zinazoongoza,komania hizo zilikuwa zimefika katika eneo lisilikuwa na maficho,kutoka umbali kama mita 100 hivi kwa ghafla na ukali adui aliamru mapigo yaanze,kombania zilianguka chini kujibu mapigo kwa mfulilizo na huku adui aliendelea kutoa kipigo kikali sana toka mbele na mbavuni.

Kwa mda wa saa moja mapigo yaliendelea toka pande zote mbili,Mizinga yetu ilishindwa kutoa mapigo ya msaada kwa sababu maadui na sisi tulikuwa tumekaribiana sana,ilitulazimu kujitegemea kwa silaha zetu za binafsi,baada ya mapigano ya saa moja askari wangu wa mstari wa mbele waliishiwa risasi kwani sikusikia milio ya risasi kutoka upande wetu.

Huku nikiwa katika nafasi ya kubabaisha,nilitazama kushoto na kulia kwangu nikaona maiti za askari wenzangu,punde si punde,kama mita 75 hivi mimi na kijana wangu wa radio tuliona maadui wakisonga mbele kuja kufyeka masalia yetu niliweza kusikia maadui wakijigamba na na kusema-Ninyi ndiyo mnatusumbua sisi,sasa tumeshaua ninyi.

Wengine walisema kamata kubwa yao iko pale,ili kuepukana na kutekwa ilibidi tutumie mbinu za hali ya juu sana,risasi nyingi sana zilitumiminikia mimi na operator wangu bila mafanikio na tuliweza kujikwamua na hatimaye tukajiunga na kombania zilikuwa nyuma.kupona kwetu,mbali ya matumizi bora ya silaha zetu na mbinu za Medani huenda pia ilikuwa pia ni Bahati yetu maana kuuwawa na kutekwa ndiyo ilikuwa hakika lakini kwa Msaada wa Mungu tulipona Luten kanali Nshimanyi alisema.

Siku hiyo tulipatwa na madhara makubwa tulipoteza askari wetu 24 katika mapigano hayo,askari waliojikwamua katika Ambush hiyo pamoja na kombania zingine mbili zilikuwa nyuma,kwa pamoja tuliendelea kukamata eneo tulilokuwa tumelishika na kiongozi wa Task-force,Brigedia Silas Mayunga aliendelea kurekebisha hali kwa kuleta misaada ya vikosi vya 29kj na 14kj.kulingana na hali ya ardhi ilivyokuwa na wingi wa maadui,ni ushujaa na ujeuri mwingi wa 20kj wa kutokukimbia uliokuwa msingi wa ushindi uliopatikana kesho yake kwa majeshi ya Task-force.

Mji wa masaka ulitekwa tarehe 01-03-1979 siku mbili baada ya Mbarara kutekwa,Awali miji hii ilikuwa imepangwa itekwe kwa siku moja ndiyo maana ilizingirwa kuanzia 28-02-1979 na ilikuwa ikipigwa mabomu usiku na mchana hivyo kupelekea kutekwa bila upinzani kutoka majeshi ya Amin baada ya miji hiyo kutekwa askari wa Tanzania walijitanua katika vitongoji vya mji wa Masaka na wanainchi ambao hawakukimbia vita waliwakaribisha wanajeshi wa Tanzania kwa vigeregere na hoihoi nyingi huku wengine wakivamia maduka na ofisi za serikari na kupora vitu walivyoweza,kwa ujumla miji yote ya Mbarara na Masaka ilivamiwa na vurumai za waporaji wa Magari na bidhaa mbali-mbali na waliokuwa wanywaji walizivamia Bar na Mahoteli na kunywa pombe ovyo ovyo wengine walikuwa wanaendesha magari ovyo ovyo hivyo kusababisha vifo vingi,Kuna watu nilioshuhudia walikuwa na furaha kupita wote watu hawa wanaitwa Wafungwa baada ya majeshi ya Tanzania kuteka miji ya Masaka na Mbarara Wafungwa wote waliachwa huru kabisa.

Baada ya kuuteka mji wa Mbarara Brigedia Silas Mayunga(Mti Mkavu) alihamishia makao makuu ya Brigedi yake katika jumba la Gavana wa Mbarara,siku hiyo hiyo ya 01-03-1979 Majeshi ya amin yakiwa na silaha nzito sana yaliamua kurudi kujaribu kuuteka tena mji wa Mbarara ndipo yalipozuka mapigano ya zaidi ya saa 7 Majeshi ya Tanzania yakiutetea mji Mapigano haya yalianza saa 10 alfajiri mpaka saa 5 usiku mji wa Mbarara ulikuwa katika wasiwasi mkubwa kutokana na majeshi ya Amin kuchachamaa kutaka kuuteka tena mji wa Mbarara.

Mkuu wa vikosi vya mbele vilivyokuwa vinapigana Luten kanali mtuma alituma taarifa kwa njia ya Redio kuwa hali ni mbaya majeshi ya Amin yanazidi kusonga mbele,Mwishowe Brigedia Mayunga alivitaka vikosi vya vifaru na vingine kusonga mbele ili kuvisaidia vikosi vya mbele baadaye ilipofika saa 5 usiku Luten kanali Mtuma alituma taarifa akisema baada ya kupata msaada wa vikosi vingine na vifaru adui aliweza kushindwa kusonga mbele na sasa anarudi nyuma.

08-03-1979 Brigedi ya Kombe ikiwa inasonga mbele katika barabara kuu iendayo Kampala huku ikiwa inafuatana na Brigedi ya Walden zilikuwa zinajiandaa kuingia Lukaya mji ambao ulitekwa kwa taabu sana kuliko miji yote katika vita vya Kagera,Brigedi ya Kombe ilikuwa inasonga mbele kwenye barabara kuu iendayo Kampala kutoka Masaka,Brigedi hii ilifuatana na ya Walden na Brigedi ya Marwa ilikuwa inasonga mbele kuelekea Mityana wakati Brigedi ya Lupogo ilikuwa inasonga mbele kuelekea Mubende kutoka Masaka vilevile Brigedi ya Silas Mayunga ilikuwa inasonga mbele kupitia magharibi ambayo kwa kweli ilisitahili kuitwa Division kutokana na ukubwa wake.

Ilikuwa sasa inasonga mbele kuelekea Kasese shabaha ya kuwa na mikondo ya aina hiyo ilikuwa kuhakikisha hakuna majeshi ya adui yanayobakizwa nyuma kwa maana halisi ya fyeka-fyeka.katikakati ya Mpungwe na Lukaya majeshi ya pande zote mbili yalikutana mapigano yalikuwa ya ana kwa ana,majeshi ya Amin yalikuwa kama Brigedi moja hivi,Upande wa majeshi ya Tanzania yalikuwa yakiongozwa na Brigedia Kombe hii ilikuwa Tarehe 08-03-1979 kila upande ulikuwa unashambulia kwa Mizinga vifaru na Askari wa miguu, vita hivyo viliendelea hadi usiku wa Tarehe 09-03-1979 hadi asubuhi hiyo kila upande ulikuwa umeelewa nguvu za mwezake huku Brigedi ya kombe ikipambana ana kwa ana na askari wa Amin Brigedi ya ya Walden ilizunguka kushoto kupitia msitu mdogo wa Karungu katikati ya Barabara kuu iendayo Kampala toka Masaka na barabara ndogo itokayo Masaka hadi Kabulasoke,hadi Mityana(iko Magharibi mwa Kampala)Maksudi ya kwenda huko ilikuwa kujaribu kuziba na kukata Supply-Route kutoka Kampala na kuyazuia yasitoke.

Mapigano makali yalizuka na kuendelea kuendelea usiku mzima wakati huo Brigedi ya Walden ilikuwa imezunguka kushoto ili kutokea mji wa Lukaya kwa nyuma,kila upande ukishambulia kwa mizinga na vifaru mapigano makali yaliendelea ilipofika saa 7 usiku majeshi ya Amin yalikuwa yamechachamaa mno na baadhi ya vikosi vilivyokuwa vinayakabili majeshi ya Amin ana kwa ana vilizidiwa wakatawanyika na kusambaratika huku vikirudi nyuma kila mtu kwa wakati wake na bila mpango na wapinganaji wake wakiwa wamechanganyikiwa kutokana na ukali wa mapigano yaliyowakabili baadhi ya askari hao walikimbia na kurudi nyuma hadi Masaka na wengine walirudi nyuma hadi Kyaka,na wengine waliweza kwenda mpaka Bukoba mjini kurudi nyuma huko kwa badhi ya askari hao wa Tanzania kuliwafanya hadi majeshi ya Amin kushikwa na mshangao na kushindwa kuyafuatilia majeshi hayo ya Tanzania kwa kuzani kuwa yanatumia mbinu ya kurudi nyuma ili kuyavuta Majeshi ya Amin yaingie kwenye mtego wa kuzungukwa.

Brigedi Kombe na makamanda wake wengine walijaribu kuwakusanya askari hao waliokuwa wanasambaa ili wajijenge upya na kuendelea na Mapigano lakini hawakufanikiwa kwani askari hao walikuwa wameingiwa na woga na wasiwasi mkubwa ambao uliwafanya wachanganyikiwe kiasi fulani 10-03-1979 Baada ya jitihada zake za kuwashawishi askari hao wajijenge upya ili kumkabiri adui kushindwa Brigedia Kombe ambaye makao yake makuu yalikuwa Mpugwe kama kilomita 15 mbele ya Masakaaliamua kurudisha nyuma Brigedi yake ili kuweka ulinzi katika mji wa Masaka na makao yake makuu yakawa Kabowoko kilomita 7 kutoka masaka mjini,pamoja na kusambaa kwa wapiganaji wake Brigedia Kombe na makamanda wake walikuwa bado Imara sana na waliojawa na Imani adui aliyewasambaza askari wake bado atashindwa,Imani yao hiyo ilitokana na kujua kuwa ile Brigedi ya Walden iliyopita upande wa kushoto ilikuwa imemtokea adui kwa nyuma na hiyo alikuwa hana mawasiliano ya kupata msaada kutoka nyuma,Brigedia Kombe alijua kuwa adui atakapobaini kuwa amezungukwa ataingiwa na wasiwasi na kusambaa na hivyo ndivyo ilitokea baada ya kutambua kuwa amezungukwa na majeshi ya Tanzania.

Majeshi ya Amin ya yaliyokuwa Lukaya yalitawanika na kurudi nyuma huku yakiacha nyuma silaha na maiti.

13-03-1979 waziri mdogo wa ulinzi wa Tanzania Baba Nape akifatana na mkuu wa mbinu za kivita katika uwanja wa mapambano Kanali Kitete walifika Kabowoko kuzungumza na askari na kujua hali ya mambo ilivyokuwa katika mapigano ya Lukaya,katika mkutano huo kati ya wanajeshi wa Tanzania na Baba Nape wapiganaji hao walidhihisha jinsi gani walikuwa wamechanganyikiwa,siku hiyo walipoambiwa watoe mawazo yao kuhusu pambano la Lukaya wapiganaji hao walieleza hofu iliyokuwa imewaingia na kukiri kuwa kwa kweli walikuwa wamechanganyikiwa kiasi kikubwa wengine walidai wapewe likizo wengine walidai warudishwe nyuma kiasi cha mwezi mmoja ndipo warudi kwenye uwanja wa Mapigano wapiganaji hao walimwambia Baba Nape(Moses Nnauye) naye hapo hapo alitumia kipaji chake cha Propaganda aliweza kuwahamasisha wapiganaji hao na wakakubali kurudi katika uwanja wa Mapigano na kuendelea na Mapambano tena kwa juhudi kubwa sana.

Baba nape((Moses Nnauye) aliwaeleza mafanikio ambayo yamekwisha patikana na jinsi mafanikio hayo yalivyopatikana kwa taabu pia aliwaelewesha kazi ambayo walikwisha kuifanya ilikuwa ni kubwa mna kulinganisha na ile iliyobakia na kwa hiyo wakawafanya wajue na kuona hasara itakayopatikana Kijeshi,Kiuchumi na Kisiasa endapo kama operation hiyo haitakamilika,vilevile aliwafahamisha kuwa adui aliyewafanya wakimbie amezungukwa,na silaha nyingi alizokuwa anatumia zimetekwa,Maelezo fasaha na yanayoingia akilini yalitolewa na Baba Nape((Moses Nnauye) akisaidiwa na Kanali Kitete na Kombe yalifanikisha kuwabadirisha mawazo wapiganaji hao na kuwapa moyo mpya wa Mapigano.

Baba Nape(Kamanda wa Hamasa) ni Kamanda aliyeshikilia nafasi mhimu katika vita dhidi ya Amin pamoja na kwamba yeye ni Waziri mdogo wa ulinzi Baba nape pia ni mkuu wa siasa katika Jeshi la wananchi wa Tanzania na ni kazi ya siasa katika mapambano ambayo ilifanya umhimu wake uonekane kwa kila mtu,Baba Nape(Kamanda wa Hamasa) aliwasiri kwenye uwanja wa vita january 1979 siku chache tu kabla ya majeshi ya Tanzania kuvuka mpaka na kuingia Uganda.

Kabla ya Mapigano ya kuvuka mpaka Baba Nape((Moses Nnauye) alizungukia brigedia zote kuwatia Hamasa na kuwaandaa wapiganaji kwa kazi ngumu iliyokuwa mbele yao.

Katika mapigano ya Lukaya Majeshi ya Amin yalifanikiwa kuvisambaratisha baadhi ya vikosi vya Majeshi ya Tanzaniza kutokana na sababu kadhaa zilizokuwepo wakati wa mapambano,Majeshi ya Amin yaliwasiri katika Mstari wa mbele wa kuanzia mapigano jioni ya siku hiyo hiyo mapigano yalipozuka kwa hiyo haikuwa rahisi kwa vikundi vyetu vya Doria kukungundua yalipo majeshi ya ya Amin kwa sababu hiyo mizinga ya Tanzania ilipiga usiku kucha bila mafanikio kwa sababu ilikuwa haipigi kwa uhakika kutokana na kutokujulikana mahali yalipokuwa majeshi ya Amin.

Siku hiyo majeshi ya Amin yaliyanjongelea kimya kimya majeshi ya Tanzania na kuanza kufanya mashambulizi ya karibu kabisa yakitumia mizinga ya Masafa mafupi aina ya Katyusha 160mm na mizinga ya 106mm sababu ya pili ilikuwa woga uliowaingia baadhi ya askari wa Tanzani hasa baada ya kupata habari kuwa Libya ilikuwa imemtumia Amin askari wapatao 2000 na mizinga ya masafa marefu aina BM-21 na ile ya 122mm pamoja na madege mawili ya aina ya Tupolev-22 mizinga hiyo ya masafa marefu hasa BM-21 ambayo Majeshi ya Tanzania yalikuwa nayo toka mwanzo wa vita ilikuwa inawatia moyo na matumaini makubwa ya kushinda vita Wapiganaji Wa Tanzania. Kwa hiyo habari kuwa adui aliyekuwa wanapambana naye alikuwa amepata mizinga hiyo, Habari hizo ziliwavunja sana moyo na kuamini kuwa sasa vita itakuwa ngumu sana wapiganaji hao walisahau kuwa kitu mhimu katika vita siyo silaha kali pekee yake bali ni pamoja na mbinu na ustadi wakuzitumia silaha hizo.

Tarehe 16-03-1979 Ndege tatu za Amin zilijaribu kushambulia sehemu za maeneo ya Kyaka karibu na mto kagera,Jeshi la wananchi wa Tanzania liliziangusha ndege zote tatu,katika mapambano makali ambayo mpaka wakati huo yalikuwa hayajatokea,Brigedi nzima ya majeshi ya Amin ilizungukwa na kuangamizwa kabisa na Brigedi ya Majeshi ya Tanzania iliyozungukia upande wa Magharibi mwa Lukaya na kutokea nyuma ya mji huo hivyo iliweka Mtego kwenye kona kali na ilifanikiwa kuuwa askari wengi sana wa Amin na askari zaidi ya 165 wa Libya walipoteza maisha yao pale pale na majeruhi wengi sana waliokuwa wakipiga kelele za kuomba msaada kwa lugha yao ya Kiarabu baada ya majeshi ya Tanzania kutoa kipigo hicho ilituchukua zaidi ya masaa 4 kukusanya maiti na waliojeruhiwa na Mateka wote walichukuliwa na kuwekwa sehemu salama na zana zilizotekwa zilichukuliwa na kupelekwa kunakohusika.

Baada ya majeshi ya Tanzania kufanikiwa kuuchukua mji wa Lukaya Brigedi ya Kombe ambayo tangu Mtukula ilikuwa inaongoza katika barabara iendaye Masaka na Kampala ilibadirishwa uelekeo hasa baada ya askari wake ambao wengi walikuwa ni WANAMGAMBO wasiokuwa na uzoefu mkubwa wa mambo ya kijeshi kupata kipigo katika mapambano ya Lukaya Brigedi yake hiyo ilipewa uelekeo wa Mityana na ile ya Marwa ambayo ndiyo ilikuwa inashughulikia uelekeo huo ikaja katika Barabara kuu ya kuelekea Kampala Brigedi ya Marwa ilikuwa miongon mwa Brigedi chache zilizokuwa na askari wengi wa Jeshi la wananchi wa Tanzania wenye uzoefu wa siku nyingi katika mambo ya kijeshi, wakati huu upande wa magharibi nako Brigedi iliyokuwa inaongozwa na Mayunga ilikuwa inasonga mbele kuelekea Kasese na Fort-portal wakati zile Brigedi za mashariki zinazosonga mbele kwenda kampala katika eneo la Kashaka lililoko katikati ya Mbarara na Kasese Brigedi ya Mayunga ilipata upinzani mkali Kwa saa moja hivi kutoka kwa majeshi ya Amin upinzani ambao baada ya kushindwa Brigedi hiyo iliweza kusonga mbele hadi Fort-portal bila upinzani mwingine.

Wakati huo huo Brigedi ya Marwa na ile ya Walden zilikuwa zinasonga mbele kwenda Mpigi kutoka Lukaya na ile ya kombe ikawa inakwenda Kabolasoke kutoka Kanone barabara ya Mityana 21-03-1979 siku hiyo Brigedi ya Mayunga ambaye alikuwa amekaribia mji wa kasese alipandishwa cheo na kuwa Meja jenerali na akawa anaongoza Brigedi mbili ambazo zilikuwa zinaunda Task-force Brigedi hizo zilikuwa zinaongozwa na Makunda na Kitete ambao wote walikuwa wamepandishwa vyeo na kuwa Mabrigadia kabla ya uteuzi huo Brigedia Makunda alikuwa kiongozi wa wanamaji katika ziwa Victoria na kitete alikuwa mkuu wa mbinu katika uwanja wa mapambano nafasi ambazo sasa zilichukuliwa na kanali Lupembe 21,22-03-1979 zilishambulia kwa mizinga mji wa Mityana na kijiji cha Kamengo kabla ya kuuteka 23-03-1979 bila upinzani mkali.
 
A terrible story,mlifanya kazi kubwa, mnatakiwa kupongezwa na kutambuliwa maisha yenu yote, sio kwa staili ya kumbukumbu zetu za ajab wakati mnakufa njaa na serikali haiwaoni kama mlilikomboa taifa, naona umekatisha story...ni historia kali sana japo inatisha...i feel it in my heart
 
Back
Top Bottom