Vunja Imani Hizi Potofu Sita (6) Kama Unataka Kujenga Utajiri Mkubwa Kwenye Maisha Yako.

Vunja Imani Hizi Potofu Sita (6) Kama Unataka Kujenga Utajiri Mkubwa Kwenye Maisha Yako.

Makirita Amani

JF-Expert Member
Joined
Jun 6, 2012
Posts
1,915
Reaction score
3,422
Rafiki yangu mpendwa,

Kila mtu aliye hai, ambaye ana shughuli yoyote ya kumwingizia kipato, anao uwezo wa kujenga utajiri kwenye maisha yake.

Ndiyo, nimesema kila mtu, hata wewe unayesoma hapa, bila ya kujali unaanzia wapi, uwezo wa kujenga utajiri tayari unao.

Kama unashangaa huo uwezo uko wapi, wakati umefanya kazi au biashara kwa miaka mingi na kitu pekee ulichoweza kujenga ni madeni, leo ninayo dawa yako. Kwa dawa unayokwenda kupata hapa, ukifanyia kazi utabadili kabisa maisha yako.

Tukirudi kwenye huo uwezo ambao kila mtu anao lakini wengi hawautumii, kinachokwamisha ni mitazamo potofu ambayo wengi wanayo. Hakuna kitu ambacho kina nguvu kwa mtu kama mtazamo anaokuwa nao.



Mwandishi Chris Hogan kwenye kitabu chake kinachoitwa EVERYDAY MILLIONAIRES ameonyesha jinsi watu wa kawaida kabisa walivyoweza kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yao na jinsi hata wewe unaweza kufanya hivyo.

Kitabu hicho ni matokeo ya utafiti uliofanywa kwa mamilionea zaidi ya elfu 10 na kuweza kupata taarifa nyingi sana kuwahusu. Utafiti huo uligusa kila eneo la matajiri, kuanzia mitazamo, fikra, shughuli wanazofanya, mahusiano, familia n.k.

Kupitia matokeo ya utafiti huo, Hogan aliweza kuona kwamba ndoto ya utajiri inawezekana kwa kila mtu ambaye anaweza kuifanyia kazi. Lakini kabla ya kufanyia kazi ndoto hiyo, Hogan anatutaka tuvunje kwanza imani potofu ambazo tumejengewa. Kwenye sura 4 za kwanza za kitabu amezungumzia imani 6 potofu zinazowakwamisha wengi.

Karibu ujifunze imani hizo potofu na jinsi ya kuvivunja ili kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yako.

SURA YA KWANZA; UMEDANGANYWA.

Kama umezaliwa na kukulia familia masikini, mambo karibu yote unayojua kuhusu utajiri na matajiri umedanganywa. Jamii inapenda kuonyesha kwamba utajiri ni kitu kibaya na matajiri ni watu wabaya.

Huo siyo ukweli, utajiri ni kitu kizuri na matajiri ni watu wazuri. Utajiri unakuwezesha kuishi maisha ya uhuru kwako. Na kuwa tajiri kunakufanya uweze kuwa na mchango mzuri kwa wengine.

Hivyo kama una mtazamo wowote mbaya kuhusu utajiri, kubali kwamba umedanganywa na chukua hatua sasa ya kuupenda utajiri na kuwapenda matajiri.

Unapaswa kuamini kwamba unaweza kuwa tajiri, kuikataa sauti zote zinazokukatisha tamaa na kuweka kazi inayohitajika ili kupata huo utajiri.

SURA YA PILI; POTOFU; MATAJIRI HAWASTAHILI UTAJIRI WAO, HAWAJAUFANYIA KAZI.

Watu ambao hawajaweza kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yao, huwa hawaelewi wengine wamewezaje kujenga utajiri huo. Badala ya kujifunza kwao ili nao waweze kujenga utajiri, wanaishia kujifurahisha na imani potofu kwamba matajiri hawastahili utajiri mkubwa walionao kwa sababu hawajaufanyia kazi. Hapa kuna imani potofu mbili ambazo ni lazima uzivunje kama unataka kujenga utajiri;

Imani potofu ya kwanza; matajiri wamerithi utajiri wao.

Hii siyo kweli, sehemu kubwa ya matajiri hawajarithi utajiri wao, badala yake wameanzia chini kabisa na wakapambana kujenga utajiri.

Na kwa wachache ambao wamerithi utajiri, pia wameweka kazi kubwa kuendeleza utajiri huo ndiyo wakaweza kubaki kwenye utajiri.

Kuna wengi sana ambao walirithi utajiri, lakini wameishia kuupoteza wote.

Hivyo unapowaona matajiri na kuanza kujifariji kwamba wamerithi utajiri, fikiria mara mbili, siyo rahisi kihivyo.

Kama unaona huna nafasi yoyote ya kurithi utajiri usione huwezi kujenga utajiri, jua kwa juhudi zako unaweza kuanzia chini kabisa na ukajenga utajiri mkubwa.

Imani potofu ya pili; matajiri wamekutana na bahati ndiyo ikawapa utajiri.

Hii siyo kweli, matajiri wameweka juhudi kubwa sana kuweza kujenga utajiri ambao wanao. Wanafanya kazi kwa juhudi kubwa na wana nidhamu kali kwenye mambo yao yote. Matajiri wana malengo makubwa na muda wote wanafanyia kazi malengo hayo.

Katika kuweka kwao juhudi, matajiri huwa wanakutana na fursa nzuri ambazo zinawapa matokeo mazuri. Kwa nje fursa hizo huonekana kama ni bahati. Lakini hazikuwafanya kitandani, bali walikutana nazo wakiwa wanaweka juhudi.

Kama na wewe unataka ukutane na bahati itakayokupa utajiri, kuwa na malengo makubwa na weka juhudi kubwa ya kazi kwenye malengo hayo. Peleka umakini wako wote kwenye juhudi zako za kujenga utajiri. Hapo unakuwa umejiweka kwenye nafasi ya kukutana na fursa nzuri na kuonekana una bahati.

Bahati ni pale maandalizi yanapokutana na fursa. Kama unataka kuwa mwenye bahati, weka juhudi kubwa mara zote na changamkia fursa sahihi zinazokuja kwako. Utaweza kujenga utajiri mkubwa kwa uhakika.

SOMA; Mjadala Wa Njia Kumi Za Kujenga Utajiri Kutoka Kitabu The Ten Roads To Riches.

SURA YA TATU; POTOFU; MATAJIRI WANACHUKUA HATUA ZA HATARI NA FEDHA ZAO.

Masikini huwa wanatafsiri vibaya sana kauli ya hakuna hatari, hakuna faida (no risk, no reward). Hiyo ni kauli ambayo imewazamisha wengi kwa kuchukua hatari za kijinga ambazo zinafanya wapoteze kila kitu. Imani hii potofu imekuwepo kwa wengi na kuwasababishia majanga makubwa. Kwenye eneo hili la hatari kuna imani potofu mbili za kuvunja ili uweze kujenga utajiri.

Imani potofu ya tatu; matajiri wanafanya uwekezaji hatari.

Kwa kuwa matajiri wanafanikiwa kujenga utajiri mkubwa, ambao masikini wanashindwa kuuelewa, huwa wanaamini kwamba wanafanya uwekezaji unalipa faida kubwa sana. Kwenye uwekezaji, pale faida inapokuwa kubwa, hatari pia inakuwa kubwa.

Wote walioweza kujenga utajiri na wakadumu nao, huwa wanakwepa sana uwekezaji wowote wenye hatari kubwa. Badala yake wanachagua uwekezaji wenye faida ya wastani na ambao hatari yake ni ndogo, kisha wanawekeza kwa muda mrefu.

Kinachowapa matajiri faida kubwa kwenye uwekezaji siyo marejesho makubwa, bali muda mrefu wanaowekeza bila ya kuvuruga uwekezaji wao.

Kama unataka kujenga utajiri mkubwa na unaodumu, achana na uwekezaji wowote wenye hatari kubwa. Chagua aina za uwekezaji ambazo hatari yake ni himilivu kisha wekeza kwa muda mrefu.

Kwa mfano uwekezaji kwenye masoko ya mitaji, kuwekeza kwenye hisa moja moja kunakuwa na faida kubwa, lakini hatari yake ni kubwa pia. Kukabiliana na hilo, mtu unachagua kuwekeza kwenye mifuko ya pamoja ya uwekezaji, ambayo hiyo inapunguza hatari kwa kutawanya uwekezaji kwenye hisa nyingi. Japo utapata faida ndogo, lakini unakuwa huna hatari kubwa.

Imani potofu ya nne; matajiri huchukua hatari za kijinga kujenga utajiri haraka.

Inapokuja kwenye kujenga utajiri, masikini ndiyo huwa wanakimbizana sana na njia za kujenga utajiri wa haraka. Kila mara huwa wanatafuta njia za mkato za kujenga utajiri ambazo hazihusishi kazi. Wanachoambulia ni kupoteza hata fedha kidogo wanazokuwa nazo.

Masikini ndiyo huwa rahisi zaidi kutapeliwa kwenye ahadi za kupata utajiri wa haraka. Masikini ndiyo wanacheza zaidi michezo ya kubahatisha kwa matumaini ya kushinda na kupata utajiri wa haraka.

Hata kwa wale ambao wanabahatika kupata utajiri wa haraka, labda kwa kushinda bahati nasibu, kupata mafao, urithi au fidia, huwa hawadumu na utajiri huo. Kwa sababu hawajaujenga kwenye misingi sahihi, huwa wanaishia kuupoteza haraka.

Kama unataka kujenga utajiri unaodumu, achana kabisa na njia za mkato za kujenga utajiri. Kila unapoitwa kwenye fursa ya kujenga utajiri wa haraka bila kufanya kazi, jua wewe ndiyo fursa yenyewe. Utaenda kuwanufaisha watu na kupoteza hata fedha kidogo ulizonazo.

Jenga utajiri wako kwa njia sahihi, inayohusisha kuweka juhudi ya kazi na kwa muda mrefu. Utaweza kudumu zaidi kwenye utajiri huo.

SURA YA NNE; POTOFU; MATAJIRI WANA ELIMU BORA NA KAZI NZURI.

Masikini huwa hawakosi sababu za kwa nini wanazidiwa utajiri na wengine. Na viti vingi wanavyojifariji navyo, huwa havina mchango wa kuwapa wengine utajiri au kuwazuia wao wasipate.

Eneo la elimu na kazi nalo limekuwa na imani potofu ambazo zimewakwamisha wengi. Kuna imani potofu mbili ambazo unapaswa kuvivunja kwenye hili eneo ili uweze kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yako;

Imani potofu ya tano; matajiri walipata elimu bora zaidi.

Imani potofu kwa wasio na utajiri ni kuona kwamba matajiri walipata elimu ambao ni bora kuliko waliyopata wao. Hilo siyo kweli, matajiri wengi hawana elimu kubwa na hata wenye elimu kubwa hawakuwa na ufaulu mkubwa darasani.

Ni kweli elimu ina mchango kwa mtu kuweza kuingiza kipato kizuri kuliko ambao hawana elimu kubwa. Lakini inapokuja kwenye kujenga utajiri, elimu kubwa inaweza kuwa hata kikwazo kwa baadhi.

Utajiri unataka mtu kubana sana matumizi na kuweka akiba na kuwekeza kwa muda mrefu. Wenye elimu kubwa huwa wanaonekana kuwa na hadhi fulani inayowataka waishi maisha ya gharama za juu na hilo kupelekea safari ya kujenga utajiri kwao kuwa ngumu.

Kwa mfano, ni rahisi kwa mwalimu kujenga utajiri mkubwa kuliko daktari, kwa sababu daktari licha ya kuwa na kipato kikubwa, gharama zake za maisha zinakuwa kubwa hivyo kushindwa kujenga utajiri.

Kama huna elimu kubwa au bora usione hicho ni kikwazo kwako kujenga utajiri. Badala yake ona ni fursa nzuri kwa sababu huna cha kukuzuia. Weka malengo yako ya kujenga utajiri na fanya kazi kwa juhudi kubwa, utaweza kuujenga utajiri kwa uhakika.

Imani potofu ya sita; matajiri wana kazi zinazowalipa vizuri.

Watu wengi huwa wanachanganya kipato kikubwa (rich) na utajiri (wealth). Huwa wanadhani mtu kuingiza kipato kikubwa ndiyo utajiri. Wakati utajiri ni mtu kuwa na thamani ya mali kubwa.

Kujenga utajiri hakutegemei sana kipato unachoingiza, bali jinsi unavyokitumia. Watu wengi wenye vipato vikubwa, kama wasanii, wachezaji, wafanyabiashara na hata viongozi wakubwa, huwa wanakuwa na matumizi makubwa pia. Matokeo yake ni wanashindwa kujenga utajiri na pale kipato hicho kinapoondoka wanarudi kwenye umasikini.

Wewe usihangaike sana na kuangalia kipato, bali angalia nini unafanya na kipato hicho. Kwa kila kipato unachoingiza, bila kujali ni kikubwa au kidogo kiasi gani, hakikisha unatenga sehemu kwa ajili ya kujenga utajiri.

Ni kwa njia hiyo ndiyo unaweza kujenga utajiri mkubwa, hata kama una kipato cha chini kabisa. Na kama tulivyoona kwenye utangulizi hapo juu, mtu yeyote mwenye kipato, hata kama ni cha kima cha chini, akiwekeza sehemu ya kipato hicho kwa muda mrefu, yaani miaka zaidi ya 30, lazima atajenga utajiri.

Rafiki, hizo ndizo imani sita potofu ambazo zimekuwa kikwazo kwa wengi kujenga umasikini. Jikague kwenye hizo imani na uone uko upande gani. Kama umekuwa na hizo imani, zivunje mara moja ili uweze kukaa sawa sawa kwenye safari yako ya kujenga utajiri.

Karibu upate UCHAMBUZI KAMILI wa kitabu hiki cha EVERYDAY MILLIONAIRES kwa kubonyeza MAANDISHI HAYA.

Tumekuwa na mjadala mzuri wa uchambuzi wa kitabu hiki cha EVERYDAY MILLIONAIRE ambapo watu wameshirikisha yale waliyojifunza na hatua wanazochukua. Fungua hapo chini kujifunza zaidi kutoka kwenye kitabu na michango ya wengine.


View: https://youtu.be/70lRAv9uKYk

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.
 
Eti naye huyu ni mwandishi wa vitabu. Nani anasoma huo upuuzi? Mbona mimi sina hizo imani na ni maskini? Umefeli sana ndugu mwandishi wa kitabu.
 
Utajiri ni codes zisizo wahi kuandikwa na hazitokuja kuandikwa..
Hebu fata hicho ulichoandika au kinachoandikwa halafu uwe tajiri..
Utajiri ni process iliyopo gizani na kamwe haitakuja wekwa hadharani.
Nilifikiri atatwambia nini tufanye kuingiza kipato na tusave vipi ili tutajirike.
 
Back
Top Bottom