Katika soko maarufu lililoko Changsha, mji mkuu wa mkoa wa Hunan katikati ya China, mwanamke mmoja aitwaye Li anachagua vitafunwa kwa ajili ya mtoto wake wa kike na wa kiume. Amechagua boksi mbili za dagaa wa maji chumvi waliokaushwa. Li anasema, anapenda watoto wake kula chakula bora, hivyo kila mara anapowanunulia chakula, anasoma orodha ya viungo vilivyopo na lishe kwa makini. Na katika dagaa hao wa maji chumvi waliokaushwa, kiwango cha protini ni kikubwa sana, na wana ladha nzuri.
Boksi moja la dagaa wa maji chumvi waliokaushwa lina pakiti 10 ndani, na linauzwa kwa yuan 25, sawa na dola za kimarekani 3.5, na Li anasema amekuwa akinunua bidhaa hiyo mara kwa mara. Dagaa waliokaushwa wa maji chumvi, wanaotokea kwenye pwani ya mashariki ya nchini Kenya, wanapatikana kwenye masoko mengi mjini Changsha.
Zhou Jinsong, mwenyekiti wa Kampuni ya Chakula ya Jinzai anasema, mauz ya dagaa hao yamevuka yuan bilioni moja kwa mwaka, na kwamba wanatakiwa kuagiza maelfu ya tani ya dagaa hao kwa mwaka. Mwaka 2018, kampuni hiyo ilijenga kiwanda nchini Kenya, ambako dagaa hao wanaonunuliwa wanatengenezwa kabla ya kuletwa nchini China.
Umaarufu wa dagaa za maji chumvi zilizokaushwa ni mfano wa mabadilishano yanayoshamiri ya uchumi na biashara kati ya China na Afrika. Bidhaa kama nanasi kutoka Benin, machungwa kutoka Afrika Kusini, pilipili iliyokaushwa kutoka Rwanda, kahawa kutoka Ethiopia, ufuta kutoka Tanzania na karanga kutoka Senegal vyote vimeonekana katika soko la China.
Kuwasili hivi karibuni kwa nyama ya kondoo kutoka Madagascar, mzigo ambao ulipitishwa na Forodha ya Changsha, uliashiria kuagizwa kwa mara ya kwanza kwa nyama ya kondoo kutoka Afrika, na pia ni alama muhimu katika biashara ya nyama kati ya China na Afrika. Kilogramu 900 za nyama ya kondoo zilisafirishwa kwa ndege, huku muda wa safari ukichukua karibu saa 36.
China imedumu kuwa mwenzi mkubwa wa biashara wa Afrika kwa miaka 15 mfululizo, na hii ni kwa mujibu wa takwimu za forodha. Biashara kati ya pande hizo mbili imefikia rekodi ya juu katika historia ya dola za kimarekani bilioni 281.1 mwaka jana, ikiwa ni ongezeko la asilimia 1.5 ikilinganishwa na mwaka 2022. Bidhaa zilizoagizwa na China kutoka Afrika mwaka jana ikiwemo karanga, mboga za majani, maua na matunda ziliongezeka kwa asilimia 130, asilimia 32, asilimia 14 na asilimia 7, ikilinganishwa na mwaka 2022.
Katika miezi 7 ya mwanzo ya mwaka huu wa 2024, mkoa wa Hunan umeagiza bidhaa za kilimo kutoka Afrika zenye thamani ya karibu yuan milioni 240, ikiwa ni ongezeko la asilimia 10.6 ikilinganishwa na mwaka jana kipindi kama hicho.
Mjini Kunshan, mkoani Jiangsu mashariki mwa China, migahawa kadhaa ya kahawa inauza mbegu za kahawa zilizoagizwa kutoka nchi za Afrika. Orodha ya vyakula katika migahawa hiyo inaeleza kwa ufasaha chanzo na ladha ya aina mbalimbali za kahawa kama vile Rirgacheffe, Geisha na Hambella, ambazo ni aina maarufu za kahawa zinazotoka nchini Ethiopia.
Kampuni ya Biashara ya Kimataifa ya Kunshan ni muagizaji wa kahawa kutoka Afrika. Mkurugenzi wa Maghala wa kampuni hiyo Zhang Lipeng anasema, buni kutoka Afrika zina ladha ya kipekee, ambayo inapendwa sana na Wachina wanaopenda kunywa kahawa. Anasema katika miaka mitatu iliyopita, kampuni hiyo imeagiza tani 800 za buni kutoka nchi za Afrika, ikiwemo Ethiopia na Uganda.