Parabolic
JF-Expert Member
- Dec 3, 2013
- 2,922
- 3,252
Kauli ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) anayeshughulikia Oganaizesheni, Paul Chacha, kwamba vyombo vya ulinzi na usalama ni “mali ya CCM”, imeibua mjadala mpana kuhusu uhusiano kati ya chama tawala, Serikali na vyombo vinavyotakiwa kulinda Jamhuri na wananchi wote.
Chacha alitoa kauli hiyo Septemba 26, 2026, mjini Iringa, katika mkutano wa chama.
"Hivi nani ambaye hajui vyombo vyote vya ulinzi na usalama ni mali ya Chama Cha Mapinduzi? Nani hajui Mawaziri wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mali ya Chama Cha Mapinduzi? Nani hajui Waziri wa Ulinzi ni mali ya Chama Cha Mapinduzi?’" alieleza Chacha
Soma: Chacha: Nani asiyejua kuwa Viongozi wote na Dola ni Mali ya CCM?
Kauli hiyo imekuja wakati CCM ikiwa imekuwa madarakani kwa miongo kadhaa, na inafufua maswali ya muda mrefu kuhusu maana ya “chama tawala”, matumizi ya dola katika siasa na mipaka kati ya chama na Serikali.
Lakini mjadala huo si mpya.
Kikwete: “Msitegemee polisi”
Mwaka 2012, wakati akiwa Mwenyekiti wa CCM, Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliwahi kuwaonya viongozi wa chama hicho dhidi ya kutegemea Jeshi la Polisi katika shughuli za kisiasa.
Kikwete alisema chama kilipaswa kujibu hoja za wapinzani kisiasa badala ya kutegemea polisi kukabiliana nao.
Soma: Kikwete: CCM tukiishi kwa kutegemea Polisi kufanikisha mambo yetu, tutakwisha na tutakwisha kweli
Alisisitiza kuwa CCM ikianza kutegemea polisi kufanikisha mambo yake ya kisiasa, chama hicho “kitakwisha”.
Kauli hii ni muhimu katika mjadala wa sasa kwa sababu ilitoka kwa mtu aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM na wakati huo akiwa pia Rais wa Jamhuri ya Muungano na Amiri Jeshi Mkuu.
Kwa mantiki ya kauli hiyo, kulikuwa na tofauti kati ya mamlaka ya Serikali ya kusimamia sheria na mahitaji ya chama ya kushindana kisiasa.
Bashiru Ally: Dola kama faida ya chama tawala
Mjadala huo ulipata sura nyingine mwaka 2020 kupitia kauli za aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally.
Soma: Dkt. Bashiru: Aliye na dola ndiye ananufaika nayo kubaki madarakani
Katika maelezo yaliyoripotiwa wakati huo, Bashiru alizungumzia faida ambayo chama kilichopo madarakani kinapata kutokana na kuwa na dola. Kauli hiyo ilielezwa kwa namna kwamba chama tawala kinaweza kutumia nafasi hiyo kujenga mazingira ya kuendelea kubaki madarakani.
Hapa ndipo neno “dola” linakuwa muhimu.
Dola si polisi pekee. Inahusisha taasisi na mamlaka za Serikali ambazo zina uwezo wa kutunga, kusimamia na kutekeleza sheria. Katika mjadala wa siasa za Tanzania, matumizi ya neno hilo yamehusishwa na taasisi kama polisi, vyombo vya usalama, mahakama na mamlaka nyingine za Serikali.
Hata hivyo, ni muhimu kutofautisha kati ya kauli ya kisiasa kuhusu faida ya incumbency na ushahidi wa tukio mahsusi ambapo chombo fulani cha usalama kimepewa amri ya kufanya kazi kwa maslahi ya CCM.
Katiba inasema nini?
Hapa ndipo kauli ya Chacha inapokutana na swali la kikatiba.
Ibara ya 147 ya Katiba inaweka majeshi chini ya Serikali na kueleza kuwa Serikali inaweza kuunda na kuweka majeshi kwa ajili ya ulinzi na usalama wa nchi na wananchi.
Muhimu zaidi, Ibara hiyo inataja Jeshi la Ulinzi, Polisi, Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa katika tafsiri ya “mwanajeshi”, huku ikikataza mwanachama wa vyombo hivyo kujiunga na chama cha siasa.
Hivyo, kikatiba kuna tofauti kubwa kati ya chama cha siasa na chombo cha Serikali.
Zaidi ya hapo, Sheria ya Vyama vya Siasa pia inakataza chama cha siasa kuunda, kuajiri au kuendesha wanamgambo, kikosi cha kijeshi au kundi la usalama linalolenga kuchukua majukumu ya Polisi au chombo kingine cha Serikali.
Kwa hiyo, kauli kwamba vyombo hivyo ni “mali ya CCM” haipaswi kuchukuliwa kama maelezo ya kisheria bila kuhojiwa. Inahitaji kutenganishwa na ukweli kwamba CCM ni chama kinachoongoza Serikali na kwamba Rais, kwa mujibu wa Katiba, ndiye Amiri Jeshi Mkuu.
Lubinga na matumizi ya jeshi kwa maslahi ya CCM
Katika historia ya CCM, kumekuwa pia na kauli kutoka ndani ya chama kuhusu namna ambavyo taasisi za dola zimehusishwa na utekelezaji wa maslahi ya chama.
Kauli zinazohusishwa na aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Kanali Ngemela Lubinga, zimekuwa zikitajwa katika mjadala huu kwa maelezo ya namna jeshi lilivyowahi kutumika katika mazingira yaliyokuwa na athari kwa CCM.
Kanali Lubinga aliteuliwa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Desemba 14, 2016 na akitokea kuwa msemaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), jambo lililozua mjadala.
Hata hivyo, akizungumza na gazeti la Mwananchi Desemba 15, 2026, Lubinga alisema alistaafu JWTZ Desemba 2, 2016 na kabla ya hapo alijiunga na CCM mwaka 1979, lakini ulipofika wakati wa mfumo wa vyama vingi kadi yake ilihifadhiwa kwenye faili lake.
Jambo linaloonyesha kuwa aliendelea kuwa mwanachama wa CCM kinyume cha ibara ya 147 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano kinachokataza watumishi wa majeshi kujihusisha na siasa.
Samia na JWTZ: “Jipangeni kwa chaguzi”
Mjadala kuhusu nafasi ya vyombo vya ulinzi na usalama katika siasa hauwezi kukamilika bila kuangalia kauli za Rais Samia Suluhu Hassan mwenyewe, hasa kwa nafasi yake mbili Rais wa Jamhuri ya Muungano na Amiri Jeshi Mkuu.
Januari 22, 2024, wakati akifungua Mkutano wa Saba wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF) na Makamanda wa mwaka 2023, katika kambi ya 302 Lugalo, Dar es Salaam, Rais Samia alilitaka JWTZ kujiandaa kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka huo na Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Katika hotuba hiyo, Rais alisema:
“Ombi langu kwenu ni kwamba mwaka huu (2024) na mwakani (2025) tunaelekea kwenye chaguzi wa nchi yetu na hapa ndipo usalama mkubwa ndani ya nchi unapotakiwa kuangaliwa kwa ukaribu zaidi... niwaombe sana Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwenye Kamandi zenu tofauti kujipanga kwa ajili hii.”
Akaendelea kueleza kuwa uchaguzi ungehusisha vyama vingi vyenye nia tofauti na kwamba jeshi lilipaswa kuwa tayari kwa hali ambayo huenda isingeenda kama ilivyopangwa.
Kauli hii ina umuhimu katika mjadala wa sasa kwa sababu haikuhusu ulinzi wa mipaka au tishio kutoka taifa jingine, bali ilitaja moja kwa moja uchaguzi wa vyama vingi kama mazingira ambayo JWTZ lilipaswa kujipanga kuyakabili.
Hata hivyo, muktadha wa kauli hiyo unakuwa muhimu zaidi inapowekwa pamoja na kauli nyingine zilizotolewa na viongozi wa CCM kabla na baada ya uchaguzi.
“Hatutakuwa na nywinywi”
Mwaka uliofuata, wakati kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2025 zilipokuwa zikielekea ukingoni, Rais Samia alirejea tena katika nafasi yake kama Amiri Jeshi Mkuu.
Katika hotuba yake ya kampeni, alisema Tanzania ilikuwa imejipanga kuhakikisha usalama na akatumia kauli maarufu:
“Hakutakuwa na nywinywi wala nywinywinywi.”
Katika kauli nyingine wakati wa kampeni, alisisitiza:
“Mimi ndiye Amiri Jeshi Mkuu.”
Soma zaidi: Rais Samia: Hakutakuwa na Nywinywinywi
Kauli hizo zilipata uzito kutokana na kutolewa katika mazingira ya kampeni za uchaguzi, ambako chama chake, CCM, kilikuwa kinawania kuendelea kuongoza Serikali.
Alipokuwa akizungumza kama Rais na Amiri Jeshi Mkuu, alikuwa akizungumza kwa niaba ya mamlaka ya Serikali na taasisi za dola. Lakini wakati huo huo alikuwa mgombea wa urais kupitia CCM.
Mchanganyiko huo wa nafasi mbili ndio unaofanya matumizi ya lugha inayohusisha Amiri Jeshi Mkuu na uchaguzi kuwa suala linaloweza kuchunguzwa kisiasa.
“Nguvu iliyotumika ilistahili”
Mjadala kuhusu matumizi ya vyombo vya ulinzi na usalama wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2025 haukuishia kwa viongozi wa CCM kupongeza Polisi. Rais Samia Suluhu Hassan mwenyewe alitetea matumizi ya nguvu yaliyofanywa na vyombo hivyo wakati wa vurugu za Oktoba 29.
Akizungumza na wazee wa Dar es Salaam Desemba 2, 2025, zaidi ya mwezi mmoja baada ya uchaguzi, Rais Samia alisema nguvu iliyotumika na vyombo vya dola dhidi ya waandamanaji “ilistahili”, akieleza kuwa hatua hizo zililenga kuzuia kile alichokitaja kuwa jaribio la kuvuruga nchi na kufanya mapinduzi.
“Nguvu inayotumika inaendana na tukio lililopo… tunapoambiwa kwamba tumetumia nguvu kubwa sana kwenye tukio lile, nguvu ndogo ilikuwa ipi?”
Rais alihoji iwapo Serikali ilipaswa kuwaangalia waandamanaji waliojiandaa kufanya kile alichokiita mapinduzi hadi wafanikiwe, akisisitiza kuwa dola haiwezi kufanya hivyo. Pia alisema Serikali ilikuwa imejipanga kukabiliana na maandamano au vurugu nyingine.
CCM yawatetea polisi
Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk Asha-Rose Migiro, alipoulizwa katika mahojiano na Crown TV kuhusu kazi ya vyombo vya ulinzi na usalama katika matukio ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, alieleza kwamba polisi walikuwa na jukumu la kulinda vituo vya kupigia kura na kukabiliana na vurugu zilizotokea katika maeneo mbalimbali.
Soma: Asha-Rose Migiro: Vyombo vya Ulinzi vilifanya kazi ya kutukuka Oktoba 29 kwa Taifa letu
Alisema vyombo hivyo vilifanya kazi kubwa kuhakikisha uchaguzi unaendelea na kwamba, kwa mtazamo wake, kutokuchukua hatua kungeweza kusababisha madhara makubwa zaidi.
Wakati huohuo, alikiri kuwa kulikuwa na dosari na akasema vifo vilivyotokea vilihitaji kuchunguzwa.
Kauli hiyo iliongeza maswali kwamba: kitendo cha CCM kuvipongeza vyombo vya usalama kwa namna vilivyoshughulikia machafuko ya uchaguzi kinamaanisha chama kinaviona vyombo hivyo kama vyombo vyake, au ni chama kinachotambua utendaji wa taasisi za Serikali?
Kutoka “chama tawala” hadi “chama na dola”
Historia ya Tanzania inaonyesha kwamba uhusiano kati ya CCM na Serikali haukuanza jana.
Tanzania ilitoka katika mfumo wa chama kimoja hadi mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. Tangu wakati huo, CCM imeendelea kushinda chaguzi za kitaifa na kubaki chama kinachoongoza Serikali.
Hali hiyo imeipa CCM kile kinachojulikana katika siasa kama incumbency advantage—faida inayotokana na kuwa chama kilichopo madarakani.
Faida hiyo inaweza kuwa na vipengele vya kawaida vya kisiasa: kuwa na uzoefu wa Serikali, mtandao mpana wa chama, viongozi waliopo kwenye Serikali na uwezo mkubwa wa kufikia wananchi.
Lakini mjadala unakuwa mzito zaidi pale ambapo rasilimali na mamlaka ya Serikali vinadaiwa kutumika katika ushindani wa vyama.
Hapo ndipo kauli ya Bashiru ya kuhusu “dola”, onyo la Kikwete dhidi ya kuitegemea Polisi, na kauli ya sasa ya Chacha zinapokutana.
Kauli ya Chacha imefanya mjadala kuwa wazi zaidi
Tofauti kubwa ya kauli ya Chacha na kauli nyingi zilizotangulia ni lugha aliyotumia.
Badala ya kusema CCM ina faida kwa sababu iko madarakani, alisema vyombo vya ulinzi na usalama ni “mali ya CCM”.
Hii inaibua maswali matatu: Kwanza, je, alikuwa akimaanisha taasisi hizo ni mali ya CCM kikatiba na kisheria, jambo ambalo haliendani na muundo wa Katiba?
Pili, je, alikuwa akimaanisha kuwa kwa sababu CCM ndiyo chama kinachoongoza Serikali, ina ushawishi wa kisiasa juu ya uteuzi na uongozi wa taasisi hizo?
Tatu, au alikuwa akielezea mtazamo wa ndani wa CCM kwamba vyombo vya dola ni sehemu ya mfumo unaolinda utawala wa chama?