Mkuu
baba anjela, naomba nichangie mada yako. Naweza kuwa si mbobezi wa sheria unayemtarajia lakini kwakuwa nami ni Mwanasheria na Wakili Msomi, nawiwa kuchangia jambo hili.
Mosi, kuna tofauti ya kuondoa/kufuta mashtaka na kusamehe mfungwa. Kuondoa/kufuta mashtaka hufanywa na Ofisi ya Mashtaka ya Taifa inayoongozwa na Mkurugenzi wa Mashtaka kupitia kwa Mawakili Wasomi wa Serikali wanaoendesha kesi husika. Hili hufanyika
kabla ya kesi husika kuhitimishwa kwa kutolewa hukumu. Mara zote, kifungu cha 91 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura nambari 20 ya sheria za Tanzania hutumika.
Msamaha hutolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wale ambao wameshapatikana na hatia na kuhukumiwa adhabu mbalimbali katika kufaidi mamlaka yake yaliyopo kwenye Ibara ya 145 (1) aya ya (a) hadi (d) ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Yaani, msamaha hutolewa kwa wafungwa. Hadi hapo, iko wazi kuwa Rais hana mamlaka ya kufuta/kuondoa mashtaka ya washtakiwa ila ni Mkurugenzi wa Mashtaka. Rais ana mamlaka ya kutoa msamaha kwa wafungwa.
Kimsingi, kwa ilivyo na ilipo kesi ya Mbowe na wenzake, Mkurugenzi wa Mashtaka aweza kuondoa/kufuta mashtaka dhidi yao. Hapo (kwakuwa hakuna hukumu bado) hakuna suala la kusamehewa kwa akina Mbowe.