Maandamano ya kupinga nyongeza ya mishahara kwa wabunge wa Kenya yanatarajiwa kuanza leo.Maandamano hayo yataanza katika mji wa Mombasa,pwani ya Kenya.Lakini pia yamepangwa kufanyika katika maeneo mengine nchini.
Ni maandamano yaliyopangwa kufanyika wiki nzima kuteta kuhusu kuongezewa posho kwa wabunge. Chama kikuu cha wafanyakazi nchini Kenya COTU kinaongoza maandamano hayo kikishirikiana na chama cha waalimu pamoja na mashirika mengine.
Wajumbe wa Kenya ni miongoni mwa wajumbe wanaolipwa mishahara ya juu duniani. Wabunge hao wamekataa kwenda mapumzikoni wakitaka suala la mishahara lijadiliwe kwanza. Wanaoandama wanasema wanafanya hivyo kutokana na kuwa wabunge wameonyesha kutojali maslahi ya raia kwa kupitisha ripoti iliyopendekeza kuongezwa kwa mishahara yao.
Tangu wakati huo kumekuwa na hisia mbali mbali huku wabunge wengine wakipinga nyongeza hiyo na wengine kusema wanastahili kupata nyongeza kwa kuwa sasa mishahara yao itakuwa inatozwa kodi.
Source:BBC