- Source #1
- View Source #1
Wakuu nimekutana na hili jambo huko mtandaoni, na mimi pia nimekuwa nikijiuliza swali hili kwa muda mrefu naomba mtusaidie. "Naomba kuuliza wadau,,wachezaji na wanamitindo kukaa katika maji ya barafu husaidia nini?"
- Tunachokijua
Tovuti ya National Library of Medicine ya nchini Marekani inaeleza kuwa mazoezi na mashindano huuweka mwili kwenye msongo unaosababisha uchovu, lakini pia husaidia kuboresha uwezo wa mwili baadaye. Ili kuongeza ufanisi na kuharakisha kupona kwa misuli, wanamichezo wanashauriwa:- Kupumzika vya kutosha.
- Kufanya mazoezi mepesi ya kushusha mwili na kunyoosha misuli.
- Kula lishe bora na kunywa maji ya kutosha.
- Kupata masaji inapohitajika.
Aidha inaongeza kuwa matumizi ya maji ya moto na baridi kwa kubadilishana yanaweza kusaidia baadhi ya wanariadha, lakini bado hakuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha ufanisi wake kikamilifu. Kwa ujumla, mchanganyiko wa mbinu mbalimbali za kurejesha mwili hutoa matokeo bora kuliko kutegemea njia moja pekee.
Dkt. A. Brion Gardner, daktari bingwa wa upasuaji wa mifupa kutoka The Centers for Advanced Orthopaedics kupitia tovuti ya Healthline anaeleza kuwa kuoga maji ya barafu kunaweza kuwa na faida hasa kwa watu wanaofanya mazoezi makali au wanariadha wa mashindano. Baadhi ya faida hizo ni pampoja na:
Kupunguza maumivu na uchovu wa misuli: Baridi inaweza kusaidia kupunguza hisia za maumivu na kuwaka kwa misuli baada ya mazoezi makali.
Kusaidia mfumo wa fahamu: Inaweza kusaidia kuboresha usingizi, kupunguza uchovu na kuongeza uwezo wa mwili kuitikia haraka katika mazoezi yanayofuata.
Kupunguza mwitikio wa uvimbe mwilini: Kushusha joto la mwili baada ya mazoezi kunaweza kusaidia kupunguza uvimbe na kuharakisha mchakato wa kupona.
Kupunguza athari za joto na unyevunyevu: Kuoga maji ya barafu kabla ya mashindano katika mazingira yenye joto kali kunaweza kushusha joto la ndani la mwili na kusaidia kuboresha utendaji.
Kufundisha mfumo wa neva kukabiliana na msongo: Maji ya barafu yanaweza kusaidia kuimarisha utendaji wa mfumo wa neva unaohusika na utulivu wa mwili wakati wa hali zenye msongo.
Aidha hospitali ya Bugando kupitia Bugando Magazine inaeleza kuwa Kujinywesha katika maji baridi kwa sekunde 30 kunasaidia mwili kupunguza uvimbe na kuamsha mfumo wa kinga. Wana soka hutumia hii kupona haraka baada ya mazoezi.
Je, kuna tahadhari yoyote inapaswa kuzingatiwa?
Dkt. A. Brion Gardner, daktari bingwa wa upasuaji wa mifupa kutoka The Centers for Advanced Orthopaedics kupitia tovuti ya Healthline anaonya kuwa ingawa kuoga maji ya barafu kunaweza kusaidia baadhi ya wanamichezo, lakini kuna hatari kwa baadhi ya watu.
Hatari kuu ni kwa wenye magonjwa ya moyo, shinikizo la damu, au matatizo ya mzunguko wa damu, kwani baridi kali inaweza kubana mishipa ya damu na kuongeza hatari ya matatizo kama mshtuko wa moyo au kiharusi. Pia, kukaa kwenye maji ya barafu kwa muda mrefu kunaweza kusababisha joto la chini mwilini (hypothermia). Watu wenye kisukari aina ya 1 na 2 wanapaswa kuwa waangalifu kutokana na changamoto ya kudhibiti joto la mwili.
Kupitia tovuti ya Cleveland Clinic, Daktari bingwa wa tiba ya michezo, Dkt. Dominic King, DO, anaongeza kuwa hatari hizi ni kubwa zaidi kwa watu wenye magonjwa ya moyo, shinikizo la damu au walio katika hatari ya kiharusi. Aidha, kutumia maji ya barafu mara tu baada ya mazoezi ya kujenga misuli kunaweza kupunguza uwezo wa mwili kujenga misuli kwa kupunguza mwitikio wa asili wa uchochezi unaohitajika katika ukuaji wa misuli.
Dkt. King, anashauri kufuata tahadhari hizi ili kuepuka madhara,
Kwanza, hakikisha joto la maji ni salama: Maji yanapaswa kuwa baridi, lakini si chini ya 4°C. Kwa wanaoanza, kiwango salama ni kati ya 10°C hadi 15°C.
Pili usikae muda mrefu, dakika 5 ndiyo kiwango cha juu kinachopendekezwa, huku wanaoanza wakishauriwa kuanza kwa dakika 1–2.
Vilevile sikiliza mwili wako, ukihisi kizunguzungu, maumivu makali au hali isiyo ya kawaida, toka majini mara moja.
Jipatie joto baada ya kutoka, jikaushe haraka, vaa nguo za joto na uurejeshe mwili kwenye joto la kawaida.