Wadau: Tutasubiri upatikanaji wa sheria mpya za Habari Zanzibar mpaka lini?

G-Mdadisi

Senior Member
Joined
Feb 15, 2018
Posts
165
Reaction score
100


ZANZIBAR.
WADAU wa vyombo vya habari wameiomba serikali ya Mapinduzi Zanzibar kukamilisha mchakato wa marekebisho ya sheria za habari zilizotolewa maoni na wadau ili kutoa mazingira rafiki kwa waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao bila vikwazo.

Imeelezwa kwa muda mrefu licha ya wadau mbalimbali kutoa na kuwasilisha mapendekezo yao kuhusu mapungufu yaliyopo kwenye baadhi ya sheria hizo, lakini utekelezaji wake bado umekuwa wa kusuasua jambo linalopelekea mazingira magumu ya utendaji kazi wa vyombo vya habari nchini.

Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), Dkt. Mzuri Issa alieleza mchakato wa mabadiliko ya sheria za habari umekuwepo kwa miaka mingi lakini bado sheria hizo ambazo nyingi ni za muda mrefu zimekwama kurekebishwa.


Aliongeza wadau wa habari wamefanya mapitio ya sheria nane za habari ikiwemo Sheria ya usajili wa wakala wa habari, magazeti na vitabu namba 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na sheria no.8 ya 1997, Sheria ya Tume ya Utangazaji Zanzibar namba 7 ya mwaka 1997 iliyorekebishwa na sheria namba 1 ya mwaka 2010 na kuwasilisha ripoti ya mapendekezo yao kwa mamlaka husika ikiwemo kukutana na Rais na waziri.


Akigusia kuhusu uhuru wa vyombo vya habari na mabadiliko ya tabianchi, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura, alieleza vyombo vya habari vitatekeleza kwa ufanisi wajibu wao katika kulinda mazingira iwapo waandishi watakuwa huru kupata na kutoa taarifa bila hofu kisheria.


Katika hatua nyingine alivitaka vyombo vya habari kubuni mbinu mpya za kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kufikiria namna ya kuendana na kasi ya mageuzi ya masuala ya kiteknolojia ili kulinda uhuru wao.


Akifafanua kuhusu maendeleo ya mchakato wa mabadiliko ya sheria za habari Zanzibar, Katibu Mtendaji Tume ya Utangazaji, Suleiman Salim alieleza tayari mapendekezo ya sheria hizo yapo ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali kwaajili ya hatua zaidi.


Aidha Suleiman alisema tayari serikali imekamilisha mchakato wa kuandaa Sera mpya ya habari Zanzibar na kuwatoa hofu wadau wa habari juu ya uwepo wa sera hiyo kuwa itazinduliwa muda sio mrefu.

Akichangia mdahalo kwenye maadhimisho hayo, Salim Said ambaye ni mwandishi wa habari mkongwe alieleza uwepo wa sheria bora ni muhimu katika kuwezesha mazingira bora ya waandishi wa habari kuwajibika.

"Vyombo vya habari ni washirika wa maendeleo, hivyo kuwa na sera na sheria bora itawawezesha waandishi wa habari kuwa na mazingira rafiki katika kutekeleza majukumu yao," alifahamisha, mwandishi wa habari huyo mkongwe Zanzibar.

Maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari 2024 yameandaliwa Baraza la habari Tanzania Ofisi ya Zanzibar (MCT ZNZ), Chama cha Waandshi wa Habari Tanzania Zanzibar (TAMWA,ZNZ) Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo (WAHAMAZA), Klabu ya Waandishi wa Wabari Zanzibar (ZPC) na Shirika la Commonwealth Foundation yakiambatana na kaulimbiu ya “UHURU WA VYOMBO VYA HABARI NA MAGEUZI YA SERA NA SHERIA ZA HABARI ZANZIBAR.”
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…