Amani iwe nanyi.
Hivi karibuni Mkuu wa wilaya ya Kisarawe ameonekana akizua taharuki na sintofahamu kwa waislam wa wilaya ya kisarawe na Tanzania kwa ujumla baada ya kuvamia msikiti huko Kiluvya na kufungia kituo cha kuhifadhisha Quran. Huku akiamuru kuwa wanafunzi warudi makwao na kuita kitendo cha wanafunzi wa kiislam kukusanyika na kuisoma dini yao ni udhalilishaji.
Hii tunaita ni chokochoko dhidi ya Uislam na waislam .Jamii ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikijenga amani na maadili mema katika nchi hii. Masuala ya Imani sio masuala ya kuyafanyia mzaha kwa kuwa yanagusa mioyo ya watu wengi na ni rahisi sana kuivuruga amani endapo atatokea mtu akaichezea ama kuidhihaki dini ya watu fulani.
Watanzania tumelelewa katika misingi ya amani,upendo,umoja na mshikamano. Ndio mizizi iliyoasisiwa na wapigania uhuru wa nchi hii na tumeweza kudumu katika misingi hiyo kwa miongo kadhaa sasa.
Anapotokea mtu awe kiongozi ama yoyote yule akafanya dhihaka ,kukashifu ,kubeza na kuingilia imani za dini fulani basi bila ya shaka anapaswa kukemewa kwa nguvu zote.
Serikali ya Rais Mama Samia ni serikali sikivu na weledi inayosimamia misingi iliyowekwa na waasisi wa Taifa hili. Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe hakupaswa kuzua taharuki kwenye vyombo vya habari kwa kufanya ziara ya kushtukiza Usiku wa manane msikitini ,ambayo waislam wameitafsiri kama uvamizi dhidi ya msikiti huko kisarawe na kuamuru kituo cha kuhifadhisha Quran kifungiwe huku akiita kuwa ni udhalilishaji.
Na pia akidai kuwa misikiti ni sehemu ya watu kuswali na kuondoka tu huku akitumia kauli za kebehi na dharau kuwa watoto wanalala kama nyanya ,wamepangwa kama tofali za block, hata nguruwe hawezi kulala katika mazingira hayo.Mara aseme watoto hao walipaswa wachapwe viboko wote na wazazi wao wawekwe gerezani kwa kuwa wameshindwa kuwalea! Hizi ni dharau kwa wazazi wa kiislam! Mzazi anayempeleka mwanae kuisoma dini yake ili awe na maadili mema katika jamii yake aonekane ameshindwa kumlea mwanae!
Leo hii mkuu mpya wa Wilaya ya kisarawe aje kuwafundisha waislam tafsiri na kazi ya msikiti.Ni jambo la ajabu na aibu sana.
Waislam nchini Tanzania wana taasisi yao ya BAKWATA, ambayo inashirikiana na taasisi nyingine ndogondogo kusimamia masuala ya waislam kwa ujumla. Petro Magoti alishindwa nini kuongea na uongozi wa BAKWATA unaoongozwa na Mufti Abubakar bin Zuber kuwa waboreshe kituo hicho cha msikiti wa kiluvya ili kuweka mazingira rafiki ya vijana wa kiislam kuisoma dini yao na jambo hilo lisifike kwenye mitandao na kuzua sintofahamu kama alivyofanya yeye?
Msimamizi wa kituo cha msikiti wa Kiluvya alionekana akimueleza Mkuu huyo wa wilaya kuwa wanafunzi wanaishi katika hali hiyo kwa dharura tu huku jitihada mbalimbali za kuanzisha ujenzi wa mabweni zikiendelea.Nondo,mchanga,cement na matofali tayari vimeshakusanywa na jitihada za kuomba vibali vya ujenzi zikiendelea kufanyika ili kuhakikisha wanafunzi wanaishi katika mazingira rafiki
Wito wangu kwa Rais ni kuhakikisha kuwa wateule wake kama Petro Magoti hawaingilii masuala ya kidini moja kwa moja kwasababu ni eneo nyeti linaloweza kuvunja amani ya hii nchi kwa haraka sana. Awashauri wateule wake wawe na busara katika masuala ya utawala.
Alilofanya Petro Magoti ni kutafuta "kiki" tu, na kuleta kebehi na kudhalilisha waislam na uislam kwa ujumla. Jambo la hatari sana.
Video ya sheikh akitoa mapendekezo kwa serikali nini kilipaswa kufanyika.
Pia soma:
Kisarawe: DC Petro Magoti ameutaka Msikiti unaotoa elimu ya dini kwa watoto 96, kuwarudisha walipowatoa sababu ya Mazingira Mabovu ya malazi