Wakazi wa maji chumvi walia na uchimbaji haramu wa mchanga unaotishia kuangusha nyumba zao

Wakazi wa maji chumvi walia na uchimbaji haramu wa mchanga unaotishia kuangusha nyumba zao

Ambakucha

JF-Expert Member
Joined
Aug 16, 2019
Posts
435
Reaction score
733
Wakazi wa Majichumvi Mtaa wa Tembomgwaza-Kimanga, wilayani Ilala jijini Dar wamefunua vinywa vyao kulalamikia uchimbaji haramu wa mchanga pembeni ya Mto Luhanga unaofanywa na vijana, hivyo kusababisha mmomonyoko unaohatarisha kuanguka kwa nyumba zao.

Kwa mujibu wa baadhi ya wakazi wa eneo hilo, eneo hilo ambalo linapita mto huo unaokwenda kumwaga maji Mto Msimbazi, halijahalalishwa na mamlaka yoyote husika kuchimba mchanga, hivyo wanachofanya vijana hao ni uharibifu wa mazingira unaohatarisha makazi zikiwemo nyumba.

Mkazi mmoja wa eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina la Jemima Kato, alisema uchimbaji huo haramu wa mchanga unafanywa na vijana kwa lengo la kujipatia pesa za kujikimu baada ya kuuza, lakini unaleta madhara kwa nyumba zilizoko maeneo hayo.

"Ni kweli vijana wanataka pesa kwa sababu kuna watu wanakuja kununua kwenda kujengea. Lakini wanapochimba mchanga wanasababisha mto kutanuka kwa sababu maji yanasambaa na kutengeneza mto mpana kuelekea kwenye makazi yetu," alisema Jemima ambaye ni mjasiriamali.

Kwa upande wake, Dauli Sulemani yeye alisema miaka sita nyuma, mto huo ulikuwa wa kawaida ukipitisha maji toka Mbezi kwenda Msimbazi, lakini kwa sasa baada ya uchimbaji wa mchanga, mto umetanuka hadi kufikia makazi ya watu na baadhi ya nyumba misingi yake imeanza kuning'inia kwa sababu ya kufikiwa na maji.

Dauli alisema walishapeleka malalamiko yao Serikali ya Mtaa wa Tembomgwaza ambao nao walifika kuangalia madhara hayo lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kuwadhibiti wachimbaji hao.
Baadhi ya taarifa kutoka kwa watu waliotaka kutotaja kwa majina yao walisema, uchimbaji huo haramu unapewa nguvu na baadhi ya wasimamizi wa sheria ambao hupata fungu kutoka kwa vijana hao hivyo 'kuwalinda'.

"Tatizo lipo kwa baadhi ya wasimamizi wa sheria ambao wanafika kuchukua 'chochote' kwa wachimbaji. Wakati mwingine wanapelekewa walipo. Kwa hiyo vijana wanaochukia wanajiona wako salama," alisema mkazi mmoja wa eneo hilo ambaye hakupenda jina lake liandikwe.

Mkazi mwingine alikwenda mbele zaidi kwa kusema kuwa, maeneo yanayochimbwa mchanga tayari yanaitwa Machimbo jambo ambalo siyo sawa.

"Kutokana na shughuli za uchimbaji mchanga hapa, sasa eneo hili watu wameanza kuliita Machimbo. Hapa siyo Machimbo. Hapa ni Majichumvi," alisema mkazi huyo aitwaye Salum maarufu kwa jina la Simbaka.
Mwisho kabisa wakazi hao wameiomba serikali kupitia kwa mamlaka husika za usimamizi wa mazingira kufika eneo hilo na kuweka TANGAZO linalopiga marufuku kwa mtu ywyote atakayekutwa akichimba mchanga achukuliwe hatua kali za kisheria ili kuleta utulivu wa kimazingira kwa eneo hilo.

** PICHA INAONESHA MATUNDU MAWILI KWENYE DARAJA MOJA DOGO YAKIWA YAPO KWA JUU BAADA YA UDONGO WA CHINI KUONDOKA KWA UCHIMBAJI HARAMU WA MCHANGA.
 
Huko kuchimba mchanga kawaida tangu kitambo ila sasa hivi watu wamekua wengi sana
 
Back
Top Bottom