Kampuni inayohusishwa na Mama Mkapa yabanwa
na Tamali Vullu, Dodoma
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
MBUNGE wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi, amezidi kuibana kampuni ya mikopo inayohusishwa na Mama Anna Mkapa, mke wa Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.
Katika hatua nyingine, mbunge huyo jana alionyesha vielelezo kuhusu kile anachokieleza kuwa ni utapeli unaodaiwa kufanywa kupitia kampuni ya Bayport Financial Services.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Zambi alisema alipoibua suala hilo bungeni, haikuwa nia yake kutuhumu tu, bali kueleza ukweli aliotumwa na watu wake.
Wabunge wanaposema mambo bungeni wanakuwa wametumwa na wananchi. Mimi haikuwa nia yangu kumshutumu mtu yeyote bungeni, bali kueleza ukweli kuhusu utapeli unaofanywa na kampuni hiyo, alisema.
Alisema katika kamati ya matumizi, mbunge anapewa muda mfupi, hivyo alishindwa kutoa vielelezo hivyo ingawa alikuwa navyo.
Zambi alisema baada ya kuibua suala hilo na kueleza kuwa riba hiyo ni asilimia 200, waathirika hao (walimu) walimpigia simu na kumweleza kuwa riba ya asilimia 200 aliyotaja ni ndogo.
Aidha, alisema kampuni hiyo ilipokwenda kwa walimu hao kujinadi, iliwadanganya kuwa itawalipia madeni mengine waliyo nayo, ili waweze kuchukua mikopo katika kampuni hiyo.
Hata hivyo, mbunge huyo aliilaumu Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushindwa kudhibiti viwango vya riba na kusababisha wananchi kuendelea kuumia.
Pia alisema Mama Mkapa anahusishwa na kampuni hiyo kupitia Taasisi ya Fursa Sawa kwa Wote (EOTF), ambayo ina hisa katika kampuni hiyo na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Ibrahim Kaduma, kupitia Kampuni ya Uwekezaji ya Taifa (NICOL). Kaduma ni mmoja wa wakurugenzi.
Mbunge huyo alionyesha vielelezo mbalimbali kuhusiana na suala hilo ikiwamo barua ya Shule ya Sekondari Mbeya kwenda kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ikitaka kusitisha makato ya mkopo wa fedha kutoka kampuni ya Bayport.
Katika barua hiyo ya Mei 8, mwaka huu, shule hiyo imeeleza kuwa hali hiyo inatokana na udanganyifu na utapeli uliofanywa na taasisi hiyo ya fedha.
Tunaomba kusitisha makato mpaka tutakapokubaliana na kampuni hiyo kwa sababu imebadili mkataba kutoka miezi 12 mpaka miezi 36.
Tulikopa fedha ya kulipa ndani ya miezi 12, lakini Bayport wameongeza miezi 24 ambayo ni mikopo hewa. Marejesho yalianza kukatwa kabla ya nakala ya mkataba kurejeshwa kwa waliokopa baada kupitishwa na mkuu wa kituo cha kazi pamoja mwajiri, alieleza sehemu ya barua hiyo.
Pamoja na barua hiyo, walimu hao waliambatanisha majina 16 ya walioathirika na suala hilo na viwango vya makato.
Walimu hao ni Idde Mwanjute aliyekopa sh 1,115,000. Alitakiwa kulipa sh 3,536,159; Mdewa Fungo alikopa sh 800,000 (kulipa sh 2,680,625); Yustus Mwalyambi alikopa sh 250,000 (kulipa sh 837,159); Eliza Mpesya alikopa 535,000 (kulipa 1,792,686); Nelusigwe Kajuni alikopa 600,000 (kulipa 2,010,489).
Wengine ni Thabita Mhagama aliyekopa sh 1,780,000 (kulipa sh 5,964,451); Antonia Kileo aliyekopa sh 405,000 (kulipa sh 1,357,080); Hastings Alamu aliyekopa sh 1,085,000 (kulipa 3,635,634); Sicknesye Sanga aliyekopa 310,000 (kulipa sh 1,038,752); na Reuben Kaminyoge sh 690,000 (kulipa sh 2,312,062).
Wako wengi. Elisala Mina alikopa sh 525,00 (kulipa sh 1,759,178); Lucy Liwungo alikopa sh 1,000,000 (kulipa sh 3,350,815); Redempta Mlingi alikopa sh 710,00 (kulipa sh 2,379,078); Elizabeth Mhilwa alikopa sh 1,000,000 (kulipa sh3,350,815); Benedicta Kagoro alikopa sh 1,000,000 (kulipa sh 3,350,815).
Vielelezo vingine ni barua kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kwenda kwa wakurugenzi watendaji wa Halmashauri na Mkurugenzi wa Jiji wa Mkoa wa Mbeya, kuonyesha kukubali kuanzishwa kwa kampuni ya Bayport Finacial Services na Platinum Credit Limited.
Katika barua hiyo ya Januari 16, mwaka huu, iliyosainiwa kwa niaba yake na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Ndewa, J.L, imewaomba viongozi hao kuzikubalia kampuni hizo kufanya huduma hiyo katika ofisi zao.
Pia mbunge huyo alionyesha barua kutoka Ofisi ya Rais (Ikulu) ya Julai 11, 2006, iliyoeleza kuikubalia kampuni kutoa huduma hiyo kwa wafanyakazi wake, lakini ilikataa kuidhamini kampuni hiyo.
Kielelezo kingine ni muhtasari wa kikao cha walimu waathirika wa Bayport na mwakilishi wa kampuni hiyo aliyetajwa kwa jina moja la Gama, kilichofanyika Aprili 3, mwaka huu.
Katika kikao hicho, Gama alikiri kupata malalamiko ya walimu hao na kueleza kwamba mawakala waliotumwa walikuwa wamewapotosha wateja.
Pia Gama alikaririwa akisema kuwa kampuni hipo ipo tayari kumsikiliza mteja atakayeamua kurejesha mkopo na kuongeza kwamba kampuni hiyi ipo tayari kumuongezea mteja fedha kwa mkataba wa awali au kupunguza makato.
Katika kikao hicho, walimu hao na mwakilishi huyo wa Bayport walikubaliana kampuni hiyo itapokea na kusikiliza malalamiko ya kila muathirika (mwalimu), ili kufikia ufumbuzi.
Pia walikubaliana kufikia Aprili 12, mwaka huu, nakala za fomu za mikataba ziwe zimewasilishwa Ofisi ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Wilaya ya Mbozi, na kwamba walimu waliotaka kurudisha fedha, ili kufuta mkataba wakubaliwe bila kikwazo.
Kampuni hiyo juzi ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari na kueleza kuwa Anna Mkapa hana hisa binafsi anazomiliki kwenye kampuni hiyo.
Kampuni hiyo ilieleza Anna Mkapa na Kaduma wameteuliwa na taasisi hizo kuziwakilisha kwenye Bodi ya Wakurugenzi ya Bayport.
Bayport iliwataja wanahisa wengine kuwa ni Afrika Yetu na Bayport Management Ltd.
Kuhusu riba, kampuni hiyo imeeleza kuwa inatoza riba inayotokana na gharama halisi za mkopo na kuongeza kuwa riba hiyo ni ya ushindani katika sekta ya masoko, lakini haikutaja kiasi cha riba.
Jumanne wiki hii, Zambi aliibua tuhuma hizo bungeni na kusema watu hao wanamiliki kampuni hiyo ambayo imekuwa ikiwatapeli walimu na watumishi wengine wa halmashauri za wilaya, kwa kuwakopesha kwa riba kubwa.
Akijibu hilo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe, aliahidi kulifuatilia suala hilo.