Wakili Mpoki: Katiba mpya ni msingi wa kulinda haki za binadamu

Wakili Mpoki: Katiba mpya ni msingi wa kulinda haki za binadamu

Parabolic

JF-Expert Member
Joined
Dec 3, 2013
Posts
2,922
Reaction score
3,252

Mpale Mpoki.png

Wakili Mpale Mpoki, ambaye amekuwa katika taaluma ya sheria kwa zaidi ya miongo mitatu, amesema mabadiliko ya Katiba ni muhimu katika kujenga mfumo imara wa kulinda haki za binadamu nchini Tanzania.​


Mpoki, ambaye ameshiriki katika kesi mbalimbali zilizogusa haki za binadamu, uhuru wa kujumuika, uwakilishi wa kisheria na mfumo wa uchaguzi, amesema Katiba ya sasa ina mapungufu yanayohitaji kushughulikiwa ili kuweka misingi imara ya utawala wa sheria na mgawanyo wa madaraka.

Kwa mujibu wa Mpoki, uzoefu wake katika kesi mbalimbali umemwezesha kushuhudia namna tafsiri za sheria zilivyoweza kubadilika kupitia hatua za kisheria na maamuzi ya mahakama.

Miongoni mwa kesi anazozitaja ni ile ya Mchungaji Christopher Mtikila iliyohusu haki ya kufanya maandamano. Mpoki anasema alihusika katika kesi hiyo baada ya Mtikila kukamatwa na polisi na kushtakiwa kwa kufanya mkutano usio halali na kutukana viongozi.

Katika mahakama ya chini, Mtikila alipatikana na hatia na kufungwa, lakini Mpoki alikata rufaa katika Mahakama Kuu ambako aliachiwa.

Anasema kesi hiyo ilikuwa na mchango katika kubadilisha namna sheria ilivyotafsiriwa kuhusu maandamano, ikiwamo suala la polisi kutoa kibali.

“Zamani sheria ilikuwa inataka polisi atoe kibali. Lakini baada ya kesi hiyo, ikawekwa kwamba polisi haruhusiwi kutoa kibali cha maandamano. Kinachotakiwa ni polisi kupewa taarifa na yeye anatakiwa kutoa ulinzi kwa watu wanaoandamana,” amesema.

Mpoki anasema licha ya mabadiliko hayo, bado kumekuwa na changamoto katika utekelezaji wa haki hiyo, akisema tatizo liko katika utekelezaji wa sheria na siyo kukosekana kwa haki yenyewe.

Amesema mtu anayefahamu haki zake anaweza kwenda mahakamani kupinga hatua zinazokiuka haki hizo.

Haki ya uwakilishi​

Mbali na kesi ya Mtikila, Mpoki anasema aliwahi kushughulikia kesi iliyohusu haki ya mtu kupata uwakilishi wa kisheria.

Anasema kesi hiyo ilihusu mtu aliyeshtakiwa kwa kosa ambalo adhabu yake ilikuwa ndogo, ambaye Serikali ilimuwekea wakili, huku mtu aliyekuwa akikabiliwa na adhabu kubwa zaidi kutokuwa na uwakilishi wa kisheria.

Kwa mujibu wake, hoja iliyowasilishwa ilikuwa kwamba mtu anayekabiliwa na adhabu kubwa anastahili kupata uwakilishi wa kisheria kwa kuwa haki hiyo ni sehemu ya haki ya kusikilizwa kwa haki chini ya Ibara ya 13 ya Katiba.

Mpoki pia anataja kesi ya mgombea binafsi iliyohusisha Mtikila, ambayo ilianza mwaka 2000 na kupita katika ngazi mbalimbali za mahakama.

Anasema Mahakama Kuu ilikubali hoja hiyo katika kile kinachojulikana kama Mtikila 1, lakini Mahakama ya Rufaa ilitengua uamuzi huo katika Mtikila 2. Baadaye suala hilo lilifika African Court katika kesi iliyojulikana kama Mtikila 3, ambayo yeye hakushiriki.

Kesi za usawa na dhamana​

Mpoki pia anataja kesi ya Rebecca Gyumi iliyohusu tofauti za kisheria kati ya wasichana na wavulana kuhusu umri wa ndoa.

Anasema kesi hiyo ilipinga sheria iliyomruhusu mtoto wa kike mwenye miaka 14 kuolewa wakati masharti hayo hayakutumika kwa mtoto wa kiume.

Mahakama ya chini ilikubaliana na hoja hiyo na baada ya Serikali kukata rufaa, Mahakama ya Rufaa iliunga mkono uamuzi wa mahakama ya chini.

Anataja pia kesi ya Mtobesi kuhusu Ibara ya 148 ya sheria iliyohusu dhamana. Kwa mujibu wake, hatua za kisheria zilisababisha mahakama kutangaza kwamba kifungu hicho kilikuwa kinakinzana na Katiba na kuamuru kifanyiwe marekebisho.

Pia anasema aliwahi kushiriki kesi iliyopinga mfumo wa mtu kupita bila kupingwa katika uchaguzi, akieleza kuwa hoja yao ilikuwa kwamba hata kama mgombea hana mpinzani, wananchi wanapaswa kupewa nafasi ya kumpigia kura.

Anasema Mahakama Kuu ilikubali hoja hiyo, ingawa Serikali ilikata rufaa, na baadaye sheria ilibadilishwa na kuzuia utaratibu wa mtu kupita bila kupingwa.

Akosoa CHRAGG​

Akizungumzia hali ya haki za binadamu nchini, hasa baada ya matukio ya Oktoba 29, 2025, Mpoki ameelekeza lawama kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG), akisema taasisi hiyo haijatumia ipasavyo mamlaka iliyopewa.

Amesema matukio hayo yaliibua masuala mbalimbali ya haki za binadamu, yakiwamo haki ya kufanya kazi, kutembea na kupata taarifa kupitia vyombo vya habari, lakini anaona CHRAGG haikutoa majibu ya kutosha.

Mpoki amependekeza CHRAGG ibadilishwe na kuwa taasisi huru zaidi isiyokuwa na utegemezi kwa Serikali.

“CHRAGG is very weak. Mimi ninapendekeza ivunjwe na iwe taasisi huru ambayo haitaegemea upande wa Serikali kama ambavyo sasa hivi inafanya,” amesema.

Mahakama nazo zakosolewa​

Mpoki pia amekosoa kasi ya mahakama katika kushughulikia masuala ya haki za binadamu, akisema taasisi hiyo ina nafasi muhimu ya kuziba mapengo pale sheria inapokuwa haijaweka mambo wazi.

Akizungumzia tume zilizoundwa kuchunguza matukio ya Oktoba 29, 2025, amesema kuundwa kwa tume hizo kunaonyesha udhaifu wa taasisi ambazo kwa kawaida zinapaswa kushughulikia masuala hayo.

Kwa mtazamo wake, tume huja pale ambapo vyombo vingine havijatekeleza majukumu yao ipasavyo.

“Polisi hawajafanya kazi, CHRAGG hawajafanya kazi, mahakama hawajafanya kazi, kwa hiyo unaenda kuunda tume kufanya kazi ambazo ni za kawaida watu walitakiwa kufanya,” amesema.

Mpoki pia ameitaja sheria ya tume za uchunguzi inayotumika nchini kuwa ya zamani, akisema haiwezi kutumika ipasavyo kushughulikia changamoto za sasa.

Apendekeza mabadiliko ya Katiba​

Kwa Mpoki, suluhisho la msingi la changamoto hizo ni kufanya mabadiliko makubwa ya Katiba.

Amesema Katiba ya mwaka 1977 haikuwa na vifungu vya haki za binadamu, ambavyo viliongezwa mwaka 1984, lakini anaona viliongezwa bila kuwekwa misingi imara ya utekelezaji.

Anataka Katiba ijengwe katika misingi ya utawala wa sheria, mgawanyo wa madaraka, Parliamentary Supremacy na Constitutional Supremacy, akisema misingi hiyo inaweza kusaidia kujenga taasisi zenye uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi katika kulinda haki za wananchi.

Kwa mujibu wa Mpoki, mahakama haipaswi kuwa na jukumu la kutoa haki pekee, bali pia inapaswa kusimamia uwiano wa mihimili ya dola kupitia mfumo wa checks and balances, ili kuzuia mhimili mmoja kuvuka mipaka yake ya kisheria na kikatiba.

Amesema hali ya sasa inaonyesha kuwa mhimili wa Serikali una nguvu zaidi kuliko mihimili mingine, jambo analoona linahitaji kushughulikiwa kupitia mabadiliko ya mfumo wa kikatiba.
 
Back
Top Bottom