Walimu na ualimu: Jamii ina mchango mkubwa katika malezi na makuzi ya vijana wetu

Walimu na ualimu: Jamii ina mchango mkubwa katika malezi na makuzi ya vijana wetu

Hermenegild sulle

New Member
Joined
Mar 8, 2016
Posts
1
Reaction score
0
Elimu bora ni hazina ambayo wazazi wenye uelewa hujivunia wanaposhuhudia imewakomboa kupitia kwa watoto wao. Wazazi wa namna hii hutambua ili kufanikisha utume huu, wanajukumu la kuwa walimu wakwanza kwa kuonyesha mfano bora kupitia imani na maisha yao. Katika hali hii watoto wanakuwa ni kioo kwa wazazi wao hivyo huwasaidia wazazi kutambua jukumu la kuwarithisha mambo msingi yatakayowasaidia katika hatua za maisha. Katika kila hatua ya ukuwaji, mtoto huendelea kutambua kuwa yeye ni kiumbe huru na anapaswa ajitegemee katika nyanja zote za kimwili, kiakili na kiroho. Wakati huu wazazi wanajukumu kubwa la kuhakikisha wanawapa elimu bora watoto wao ili wanapokuwa watu wazima na kujiona wapo huru waweze kukabiliana na changamoto za kimaisha.

Katika nchi yetu ya Tanzania mtoto anapofikisha umri wa miaka minne huanza kwenda shule ambazo zina mifumo inayomuwezesha kujipatia malezi, maarifa na ujuzi unaoaminika na kuhitajika ili aweze kuwa msaada katika kulijenga taifa. Mtoto anapoingia katika mifumo hii anakutana na wakufunzi ambao ni “walimu” wanaomsaidia kuelewa mambo ambayo anapaswa kuyaelewa. Na kama ulivyo uhalisia, ili mwanafunzi amuelewe mwalimu, jambo la msingi ni kumwamini mwalimu wake na wanafunzi wenye nidhamu, bidii na imani kwa walimu wao hujichotea maarifa na kuwa hodari wawapo mashuleni. Kwa maono haya tunatambua kwamba walimu ni watu muhimu wanaobeba imani na mitazamo ya watoto wetu. Mambo haya kwa ujumla yanaweza kuwa na athari chanya au hasi kwa mwanafunzi.

Mwalimu pia ni mzazi wa pili wa mtoto kwa maana ya kwamba hufurahia na kujivunia kuona mwanafunzi wake anafanikiwa pindi awapo shuleni na nje ya shule. Jambo hili linamfanya mwalimu kuwa wa pekee katika jamii zetu. Mwalimu makini pia hutambua analakujifunza kutoka kwa wanafunzi wake. Walimu wa namna hii huzidi kukomaa na kujikuta ni wapya kila wakati kwa kujifunza mambo tofauti kutoka kwa vizazi vilivyo tofauti. Walimu hawa huwa na uelewa mpana kuhusu maisha na kupelekea kuwa watu wa kutegemewa katika jamii zetu pale wanapoonekana na kupatiwa jukumu la uongozi.

Kijana anapotoka katika mifumo rasmi ya elimu anategemewa na jamii kwamba amekomaa katika kuendeleza na kuleta mabadiliko chanya katika jamii na taifa lake. Katika kipindi hiki kijana makini huendelea kujifunza kama ilivyo kwa walimu wanavyojifunza kwa wanafunzi wake. Jamii ndio inakuwa mwalimu wake na mitazamo ya kijana huyu inaendelea kuathiriwa na jamii yake. Kwa kunukuu maneno aliyoyasema Raisi Samia Hassani alipokuwa akihutubia bunge jijini Dodoma tarehe 22.04.2021, “makuzi ma umakini wa akili hutegemea jamii inayokuzunguka na shughuli zinazokuzunguka katika makuzi yako”, jamii zetu zinamchango mkubwa katika malezi na makuzi ya vijana wetu.

IMG_0330.jpg

(Picha mtandaoni)

Katika uhalisia wa kwamba kila mmoja wetu ananafasi katika jamii zetu, tunashiriki katika malezi kwa kujua au kutokujua. Kwa mtazamo huu sisi sote ni “walimu” na walezi hivyo katika kutenda na kutimiza wajibu wetu tukawe walimu bora ili tujenge vizazi imara vitakavyoweza kupeleka mbele taifa na dunia kwa ujumla.

Nawasilisha!
 
Back
Top Bottom