Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
Sahihisho picha ya akina mama walimsindikiza Mwalimu.
Kulia ni Bi. Tatu bint Mzee na kushoto ni Bi. Chiku bint Said Kisusa
Hapo chini anaeleza jinsi alivyoshuhudia nyumbani kwao jinsi baba yake alivyowaingiza akina mama katika harakati za TANU:
''Ilikuwa katika kipindi hiki cha mimi kuanza kupata akili katika kukua kwangu ndipo nilipokutana na wanawake wazalendo waliokuwa wanaochipukia katika uongozi wa Tanganyika, wanawake kama Bi. Lucy Lameck kutoka Moshi, Mary Ibrahim na akina mama wa Kiislam kama Bi. Titi Mohamed, Bi. Tatu bint Mzee, Bi. Hawa bint Maftah, hawa kutoka Dar es Salaam, wote hawa kwangu mimi walikuwa bibi zangu.
Kitu cha kufurahisha ni kuwa hawa akina mama wote walivutwa katika siasa na Bibi Chiku bint Said Kisusa, maarufu akijulikana kama Mama Sakina.
Soma pia: Bi. Chiku Kisusa (Mama Sakina)
Alikuwa Mama Sakina ndiye aliyewapa hawa wanawake niliowataja hapo juu utambulisho na wakaja kuwa watu maarufu.
Baba yeye ndiye alikuwa kiongozi wa mikakati hii yote kwa sababu bila yeye kuwatia hima kwa kutumia ushawishi wake ingekuwa vigumu kuweza kuwatia hawa wanawake katika kuwahamasisha wanawake wenzao wa Kiislam na wao watoke majumbani kuja mstari wa mbele katika mikutano wakiimba na kutoa vibwagizo vya kuunga mkono TANU na kudai uhuru.
Hili jambo lilikuwa jipya, jambo ambalo katika utamaduni wetu kwa wakati ule halikutarajiwa na ni kinyume katika utamaduni wetu kwa wanawake wa Kiislam kulifanya katika siku zile.
Nimesikia mazungumzo mengi wakati baba na wenzake walipokuwa wakijadili majina na shughuli ambazo hawa akina mama walikuwa wahusishwe ili kuleta mvuto wa kisiasa katika mikutano yao ya TANU.
Nakumbuka vizuri sana jinsi baba alivyokuwa karibu sana na Mwalimu Sakina na ndugu yake Mwalimu Fatna (wote hawa watoto wa Mama Sakina), na jinsi alivyowaleta ndugu hawa karibu na Mama Maria na hawa wakamjulisha Mama Maria Nyerere kwa mama yao na mashoga zake Bi Hawa Maftaha, Bibi Titi Mohamed na Bi Tatu binti Mzee.
Hawa wanawake ndiyo waliomsaidia Mama Maria kufungua duka lake dogo pale Mtaa wa Livingstone kona na Mchikichi, mahali ambako Mama Maria alishinda kutwa nzima akiuuza duka lake.
Nikiwa mtoto nakumbuka kwenda kwenye duka lile kila siku mchana kupeleka chakula kwa Mama Maria, ambako hapakuwa mbali kutoka nyumbani kwetu.
Kwa kuwa baba alikuwa anataka ratiba hii yake ya chakula ifuatwe sawasawa kwa wakati wake, wakati mwingine hii ilikuwa changamoto kubwa sana.''