BINTI 'ZUCHU' ADAIWA KUWA NA DR. ISACK SIKU NZIMA KABLA HAJAUAWA NYAMONGO!
Mpendwa,
Mimi ni mkazi wa Nyamongo katika Wilaya ya Tarime. Ninaomba kupitia kwako umma ujue mambo ya msingi kuhusu tukio la kutekwa na kuuawa kwa Dr. Isack Daniel Athumani.
Kwanza tunaomba ifahamike kuwa watu wa jamii ya Nyamongo tuliokuwa tunahudumiwa na Dr. Isack hatukuwa na tatizo naye. Ni kijana mmoja aliyekuwa na moyo wa kujituma kwenye kazi yake, alikuwa na moyo wa kujitoleo sana. Kama jamii hatukuwa na shida naye kwani ni mtu ambaye alikuwa social sana na wananchi. Kama jamii hatukuwahi kuona kitisho chochote kwa Dr. Isack alipokuwa miongoni mwetu, na tulishirikiana naye vyema hata kwenye matukio mengine ya kijamii hapa kijijini.
Marehemu Dr. Isack alikuwa anafanya kazi kama Mganga Mfawidhi katika Kituo cha Afya cha Nyamongo katika kijiji cha Kerende, Kata ya Kemambo, na alikuwa anaishi hapo hapo kituoni yeye na familia yake.
Siku ya tukio, Daktari alionekana akiwa kituoni hadi majira ya saa 3 usiku. Baada ya hapo, alielekea kwenye Bar moja iliyopo hapo Kijijini Kerende kwa jina la "Charles Bar and Guest House." Hiyo ni Bar ambayo ipo umbali chini ya kilomita 1 kutoka hapo Kituo cha Afya. Taarifa za watu waliokuwa naye pale Bar zinasema kuwa ilipofika majira ya saa 5 usiku, aliwaaga kwamba anaondoka kwenda kutafuta chakula Nyangoto (hii ni Senta kubwa iliyopo mbali kidogo na Kijiji cha Kerende).
Wakati anaondoka pale Bar aliondoka na binti mmoja maarufu kwa jina la "Zuchu" ambaye inasemekana kuwa ni Msukuma na alikuwa Mhudumu wa ile Bar. Pia taarifa zinasema kuwa marehemu alikuwa na mahusiono ya kimapenzi ya muda na huyo mhudumu wa Bar. Siku hiyo hiyo kabla daktari hajaondoka kituoni saa tatu usiku, huyu mhudumu alionekana pale hospitali kwenye Benchi akiwa anamsubiria daktari. Majirani wa eneo lile wanasema kuwa ilikuwa ni kawaida yake kwenda pale kumwona Dr. Isack. Wakati anaondoka pale Bar alitumia pikipiki yake ambayo ni mali ya serikali.
Wakati Dr. Isack anavamiwa, watu wa kwanza kufika eneo la tukio majira ya saa tano usiku, walimkuta huyo binti naye ametekwa pamoja na Dr. Isack. Kwa taarifa za awali ilionekana huyo binti alibakwa na wale watekaji na suruali yake ilichanwa na aidha kisu au panga. Japo kuna watu wanaojiuliza ni wabakaji wachane suruali ya binti yule bila hata kumchubua ngozi. Kama alibakwa au la hilo litabaki kuwa ni suala la kitabibu zaidi.
Usiku uleule Dr. Isack na yule binti walipelekwa Kituo cha afya Nyangoto kwa ajili ya kupatiwa msaada wa kuokoa maisha yao. Ilisemekana baada ya taratibu za kitabibu, binti alikabidhiwa mikononi mwa Jeshi la Polisi ambalo baadaye lilimwachia na kurudi kijijini. Wakati bado tupo msibani na taharuki, taarifa zinasema Polisi walimfuata yule binti, baada ya muda akarudi tena kwa boda boda. Lakini sisi hatukujua tena kilichokuwa kinaendelea.
Jambo la msingi tunalohitaji kutoka kwenye vyombo vya dola ni kuhakikisha kuwa wahalifu wanapatikana na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Kwa kuwa siku ya kuaga mwili hapa Kerende, OCD wa Wilaya ya Kipolisi Nyamwaga alitamka hadharani kwamba wameanza kupata muelekeo wa kuwapata washukiwa wa uhalifu huo, tunaomba hiyo aliyosema OCD yatimie ili tumalize vitendo vya uhalifu katika jamii yetu.
Mwananchi wa Nyamongo
Tarime, Mara; 7 Mei 2023