Mtikisiko wa uchumi duniani waiathiri Tanzania
Imeandikwa na Faraja Mgwabati; Tarehe: 28th March 2009 @ 20:03 Imesomwa na watu: 760; Jumla ya maoni: 1
Athari za mtikisiko wa uchumi duniani zinaendelea kugusa sekta mbalimbali nchini na kusababisha hofu miongoni mwa wananchi na wadau mbalimbali kama hali hiyo itaendelea kwa muda mrefu. Kwa mujibu wa taarifa zilizosomwa na wizara mbalimbali jana katika mkutano wa kujadili athari hizo, kila sekta ya uchumi imeathirika, huku sekta za madini na nishati ambazo ndizo zinachangia kwa kiasi kikubwa uchumi na pato la taifa (GDP), ikiwa hatarini zaidi. Mkutano huo ambao unafanyika Dar es Salaam, ukiwa umeandaliwa na Wizara ya Fedha na Uchumi, ukishirikisha wataalamu na wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi uliambiwa na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, kuwa athari hizo tayari zinaonekana nchini.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Nishati na Madini, ilionyesha kuwa baadhi ya migodi ya madini kama vile North Mara ambao unamilikiwa na Barrick Tanzania, unatarajia kupunguza wafanyakazi 200. Pia miradi mingi ya madini na nishati imekwama ukitolewa mfano wa miradi ya umeme wa gesi ambayo ilikuwa itekelezwe na kampuni ya Artumas Mtwara kwa thamani ya dola milioni 153 za Marekani ambao sasa umesimama. Aidha, mradi wa makaa ya mawe wa Kiwira ambao ulikuwa uzalishe megawati 200 nao umekwama.
Mingine iliyokwama ni wa Kabanga Nickel ambao kutokana na kushindwa kuanza, utaikosesha serikali mapato ya dola bilioni 1.9 (Sh trilioni 2) kwa mwaka, huku mradi wa umeme ambao ulikuwa uzalishwe na kampuni ya Sekab ya Sweden nao umechelewa. Hali kadhalika mtikisiko wa uchumi umeshusha bei ya tanzanite kutoka dola 500 kwa kipimo cha carat hadi dola 200 na almasi imeshuka kwa asilimia 60 na imeelezwa kuwa hali huenda ikazidi kuwa mbaya. Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Miundombinu inaonyesha kuwa ndege za kimataifa zinazotua nchini kuanzia mwaka jana zilipungua kutoka asilimia 16.1 mwaka juzi hadi asilimia 6.4.
Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko ilionyesha miradi minane muhimu ambayo ilikuwa itekelezwe kushindikana au kuchelewa kuanza na haifahamiki lini itaanza. Miradi hiyo ni pamoja na wa magadi Ziwa Natron ambapo mwekezaji, TATA Chemicals Limited amejitoa, mradi wa kufufua kiwanda cha Kilimanjaro Machine Tools, Mchuchuma na Liganga, Bandari Kavu Dar es Salaam, mbao Mtwara, umeme Mnazi Bay na saruji Nangote Mtwara nayo imesimama.
Naye Waziri Mkulo alisema kilimo kinatarajia kushuka kutoka asilimia 3.6 mwaka jana hadi 3.1 mwaka huu, sekta ya hoteli na migahawa itashuka kutoka asilimia 4.1 mwaka jana hadi asilimia 1.4 mwaka huu na ajira zinatarajia kupungua kwa nchi masikini. Baadhi ya maoni ya wizara hizo kuhusu nini kifanyike ni pamoja na kupunguza utegemezi kwenye misaada kutoka kwa wahisani wa nje, kupunguza utegemezi kwenye masoko ya Ulaya na Marekani na kuimarisha masoko ya ndani na kutazamwa upya kwa mfumo wa fedha wa Dunia ili uweze kukidhi mahitaji ya nchi zote.
HabariLeo | Mtikisiko wa uchumi duniani waiathiri Tanzania