Rasmi Karia mgombea pekee wa urais TFF, utata ukitawala uchaguzi
Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imewang'oa wagombea watano wa nafasi ya Urais, na kumuacha Wallace Karia pekee, anayetetea kiti hicho, akiwa mgombea asiyepingwa.
Uamuzi huu umekuja huku kukiwa na malalamiko mengi na maombi ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuingilia kati.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa TFF, Wakili Kiomoni Kibamba, alithibitisha kuwa Karia ndiye mgombea pekee aliyekidhi vigezo vyote vya kikanuni.
Kibamba alifafanua kuwa kati ya wagombea sita wa urais, mmoja hakutokea kwenye usaili huku wengine wanne wakishindwa kukidhi matakwa ya kanuni za uchaguzi.
"Kwenye nafasi ya urais kulikuwa na wagombea sita, mmoja hakutokea kwenye usaili na wengine wanne hawakukidhi matakwa ya kikanuni, mgombea mmoja amekidhi matakwa yote ya kikanuni na tumempitisha ambaye ni Wallace Karia," alisema Kibamba.
Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa Kanuni, bado kuna fursa kwa yeyote mwenye pingamizi kufanya hivyo.
Awali, wakati wa kurejesha fomu zao, baadhi ya wagombea wa urais, wakiwemo Ally Mayay, Shija Richard, Dk. Mshindo Msolla na Mustapha Himba, walilalamikia kukosa wadhamini. Walidai kuwa wajumbe wote wamemdhamini Rais wa sasa wa TFF, Wallace Karia.
Wakili Kibamba alisisitiza kuwa kamati yao inasimamia kanuni zilizotungwa na Mkutano Mkuu, na kwamba mgombea asiyekuwa na wadhamini wasiopungua watano hatapitishwa. Alifafanua kuwa kama kuna shida na udhamini, Kamati ya Uchaguzi si mahala pa kupeleka malalamiko, bali ni kwenye Mkutano Mkuu wa TFF.
Kuhusu pingamizi lililowekwa na Klabu ya Yanga dhidi ya Karia, Kibamba alifafanua kuwa limetupiliwa mbali. Alisema Mtendaji Mkuu wa Yanga, Andre Mtine, aliyewasilisha pingamizi hilo, hakutokea kwenye usikilizwaji, badala yake alimtuma wakili, jambo ambalo ni kinyume na kanuni ya 11, kanuni ndogo ya sita ya uchaguzi inayotaka mlalamikaji kuwepo mwenyewe.
Wakati huohuo, jopo la mawakili watano likiongozwa na Wakili Juma Nassoro, limepeleka maombi Baraza la Michezo la Taifa (BMT) likitaka liingilie kati Uchaguzi Mkuu wa TFF. Katika barua yao ya Julai 2, 2025, mawakili hao walitaka BMT kuhakikisha sheria na kanuni zinatekelezwa, wakidai kuwa kumeibuka malalamiko mengi, ikiwemo suala la mgombea mmoja (Karia) kujimilikisha wadhamini wote, jambo walilolieleza kuwa ni hila ya uchaguzi.
Wakili Nassoro alisisitiza kuwa wameingilia kati bila kutumwa na mgombea yeyote, na kwamba kama BMT haitachukua hatua, watalipeleka suala hilo mahakamani. Alibainisha kuwa Karia amechukua wadhamini 46 kati ya 47, isipokuwa mmoja tu aliyetoka Klabu ya Yanga.
Kuhusu nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji, Kibamba alieleza kuwa kati ya wagombea 19, 17 walihudhuria usaili. Saba wamekosa vigezo na kumi wamepitishwa kuendelea na mchakato wa uchaguzi katika hatua inayofuata.
Uchaguzi Mkuu wa TFF unatarajiwa kufanyika Tanga, Agosti 16.