Lugha ya Kichina imeendelea kupata umaarufu katika nchi mbalimbali duniani, na imekuwa ni chaguo kwa vijana wengi ambao wanaona faida yake katika soko la ajira. Shule nyingi duniani hasa za barani Afrika zimejumuisha lugha hii kwenye mitaala yao ya masomo, ikionyesha jinsi ambavyo lugha hii inapewa umuhimu mkubwa katika masomo na nchi husika.
Mara nyongi tumesikia mashindao ya lugha ya Kichina yanayofanyika katika nchi mbalimbali, na washindi kupata fursa ya kutembelea nchini China ambako wanapata uelewa zaidi wa mila na desturi za Kichina. Wanafgunzi wengi waliosomea lugha ya Kichina wameeleza mafanikio makubwa waliyopata katika maisha yao, ikiwemo ajira, na kuwawezesha kubadili maisha yao na jamii zao.
Muthoni Kimani, mwenye umri wa miaka 20, ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Nairobi, alipata umaarufu kutokana na uwezo wake wa kutamka kwa ufanisi maneno ya Kichina. Akiwa ni mwanafunzi anayesome lugha ya Kichina, Muthoni alialikwa kutoa hotuba kwa niaba ya wanafunzi wenzake ambao watajiunga na Chuo Kikuu cha Ualimu cha Tianjin mwezi Septemba mwaka huu kwa kozi ya miaka miwili kuboresha ujuzi wao wa lugha ya Kichina. Muthoni anasema alifurahi sana kupata ufadhili huo wa kusomea lugha ya Kichina nchini China na kuahidi kurejea Kenya kuboresha ufundishaji wa lugha ya Kichina mashuleni.
Muthoni ni miongoni mwa wanafunzi 20 kutoka Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Nairobi ambao wameondoka Kenya hivi karibuni kuja nchini China kwa ajili ya kuendelea na masomo yao yanayohusiana na lugha ya Kichina. Wanafunzi hao ni wafaidika wa makubaliano ya pande tatu yaliyosainiwa Desemba, 2023 kati ya Chuo Kikuu cha Nairobi, Kituo cha Elimu na Ushirikiano kilicho chini ya Wizara ya Elimu ya China, na Chuo Kikuu cha Ualimu cha Tianjin, yanayolenga kuboresha ufahamu wa lugha ya Kichina kupitia mradi wa “Ufadhili wa Shahada mbili ‘2+2’.”
Mradi huo unajikita katika mafunzo ya pamoja katika elimu ya kimataifa ya lugha ya Kichina na kuunga mkono lengo pana la kujumuisha lugha hiyo katika mtaala wa masomo wa Kenya. Wahitimu wa mradi huo wanatarajiwa kukidhi vigezo chini ya Tume ya Walimu ya Kenya na wataajiriwa kufundisha lugha ya Kichina katika shule za sekondari, na hivyo kutoa mchango katika ukuaji wa elimu ya lugha ya Kichina nchini humo.
Akiwa tayari amesoma kwa miaka miwili lugha ya Kichina mjini Nairobi, Muthoni anasema ana matarajio makubwa ya kuendeleza ujuzi wake na kuanzisha urafiki wa kudumu wakati akiwa mafunzoni nchini China.
Hafla ya kuwaaga wanafunzi hao ilihudhuriwa na maofisa wa ngazi ya juu wa serikali ya Kenya, wafanyakazi wa kitivo hicho pamoja na familia za wanafunzi waliopata ufadhili wa masomo nchini China.
Katibu wa Idara ya Elimu ya Juu na Utafiti iliyo chini ya Wizara ya Elimu ya Kenya, Carol Hunja, amewataka wanafunzi hao kujifunza kwa kina utamaduni wa China watakapokuwa nchini China, na kuwataka kuwa mabalozi wa kubadilishana tamaduni, huku wakijifunza tamaduni mbalimbali za China, ikiwemo chakula.
Mwalimu wa lugha ya Kichina katika Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Nairobi, Song Chunzhi, amewasifu wanafunzi hao kwa nia yao thabiti, na kusema wanafurahia sana fursa hiyo adimu ya kuendelea na masomo yao nchini China.