Changamoto ya ubovu wa miundombinu ya barabara katika eneo la Kiruweni, Kata ya Mwika Kusini, Wilaya ya Moshi, imewalazimu wananchi wa eneo hilo waishio maeneo mbalimbali nchini kuchangishana fedha na kuanza ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 72 kwa kiwango cha changarawe.
Eneo hilo ambalo wananchi wake wanajishughulisha na uzalishaji wa ndizi na kilimo cha mazao mbalimbali, limekuwa na changamoto kubwa ya miundombinu ya barabara.
Hali hii imewalazimisha kusafirisha mizigo kwa kichwa hadi sokoni, hivyo kushindwa kufikia ndoto zao za kujikwamua kiuchumi.
Chimbuko la wazo la ujenzi wa barabara lilianzia katika Usharika wa Kiruweni wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), baada ya mvua kubwa zilizonyesha mwishoni mwa Machi na Aprili, 2024.
Mvua hizo zimesababisha barabara hizo zishindwe kupitika kwa vyombo vya usafiri, zikiwamo pikipiki.
Akizungumza kuhusu ujenzi huo, Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Kiruweni, Joram Mamuya amesema barabara hizo zimefikia hatua mbaya na kufanya wananchi kushindwa kutumia vyombo vya usafiri na hivyo kulazimika kubeba mazao yao kichwani kuyapeleka sokoni, huku wakitembea umbali mrefu.