Nelson...
Nelson...
BAADA YA KIFO CHA BILAL WAIKELA WANACHAMA WA TANU ILE YA 1954 WAMEBAKIA WANGAPI?
Mimi nina hesabu yangu ya wanachama wa TANU ile ya New Street mwaka wa 1954.
Hadi leo sasa ni miaka 68 imetimia toka kuundwa kwa TANU.
Fikra hii ya kutaka kuwajua wanachama wa TANU wa 1954 imenijia baada ya kila mtafiti anaekuja kunihoji na wakati wengine watu wa vyombo vya habari huwa wananipa maswali ambayo huwaambia kuwa watapata historia ya uhakika sana endapo watapata kuzungumza na Mama Maria Nyerere.
Huwaeleza hawa hivyo kwa sababu wao wanavutiwa sana na zile ziku za mwanzo a kuunda TANU wakati Julius Nyerere kafika Dar es Salaam na kakutana na Abdul Sykes.
Mama Maria na mumewe wote walikuwa karibu mno na Abdul Sykes mkewe Bi. Mwamvua Mrisho kwa hiyo wana mengi katika siku zile za mwanzo za kuunda TANU.
Historia hii ya Nyerere na Abdul Sykes imewavutia watu wengi sana.
Bahati mbaya mwaka wa 1952 ndiyo mwaka niliozaliwa mimi na huwaeleza wanaonihoji ukweli huu na huwaambia mwaka huo ndiyo mwaka baba yangu anamtia Nyerere machoni kamkuta nyumbani kwa Abdul Sykes Mtaa wa Stanley na Sikukuu.
Huwaambia ikiwa nyie mnataka historia hii kwa ukamilifu kabisa kwa nini hamuombi kuonana na Mama Maria?
Siku hizi Abbas Sykes alikuwa hai lakini mengi aliyoona Abbas Sykes nilikuwa nayajua kwa yeye na nimeyaeleza yanafahamika.
Ndipo siku moja nikajiuliza kwani hawa wanachama wa TANU ya 1954 wamebakia wangapi?
Nikawa najisemeza mwenyewe na kuanza kuwahesabu wale ambao mimi nawajua.
Mwalimu Nyerere alikuwa keshafariki mwaka wa 1999 na hapa ikanijia siku nilipokwenda kumpa pole Balozi Abbas Sykes nyumbani kwale alipotoka London kuchukua mwili wa Mwalimu Nyerere baada ya kifo chake.
Abbas Sykes alimjua Nyerere toka siku ya kwanza alipofika nyumbani kwao na wamekuwa pamoja uhai wao wote.
Katika ndege ile ATC iliyobeba mwili wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere walikuwa wanachama watatu wa TANU ile ya 1954; Julius Nyerere ambae alikuwa keshaaga dunia, Mama Maria na Abbas Sykes.
Abbas Sykes ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa ATC.
Nikawa naendelea kujisemeza lazima watakuwapo wana TANU wa 1954 walio hai ambao mimi siwajui wako Dar es Salaam na kwengineko mikoani.
Lakini hawa unawapataje?
Historia a TANU yote haipo na CCM warithi wa TANU haielekei kama wanaithamini sana historia ya TANU na waasisi wake.
Kingunge Ngombale Mwiru alikuwa hai na kwa kauli yake mwenyewe anasema yeye aliingizwa TANU na Ally Sykes miaka hiyo ya mwanzo.
Akili inagota simpati mwana TANU mwingine katika wale niliopata kuwajua.
Anakuja Bilal Rehani Waikela kichwani mwangu kutoka Tabora.
Najiambia na kujiuliza kuwa hawa wanachama wa TANU 1954 sasa wanahesabika kiganjani?
Ina maana wote wameshakufa?
Wamebakia Mama Maria Nyerere, Abbas Sykes na Rehani Bilal Waikela?
Usilojua usiku wa kiza.
Kumbe hapa jirani ya nyumbani kwangu Magomeni Mapipa kuna mwana TANU 1954 jina lake Athmani Matenga.
Nilipokwenda kumuona akaniambia kuwa yeye kadi yake ya TANU kauziwa na Ali Msham kwenye tawi alilofungua nyumbani kwake Mtaa wa Jaribu.
Na haya ndiyo katika maajabu ya Allah si tu kuwa Othman Matenga yu hai hadi leo hii bali yupo pia kwenye picha ya tawi la TANU la Ali Msham ya mwaka wa 1955.
Mzee Athmani Matenga akanieleza kuwa alikwenda kumpokea Nyerere alipotoka UNO safari ya kwanza 1955 na kushiriki katika yale maandamano makubwa akiwa anaendesha pikipiki yake.
Nikawa sasa nina wanachama wa TANU 1954 wanne walio hai - Mama Maria Nyerere, Abbas Sykes, Bilal Rehani Waikela na Athmani Matenga.
Kisha siku moja ghafla nikatembelewa na Rajabu Matimbwa muasisi wa kwaya ya kwanza ya TANU New Street mwaka wa 1954.
Leo hivi ninavyoandika wana TANU 1954 baada ya kifo cha Bilal Rehani Waikela wamebakia watatu - Mama Maria Nyerere, Athmani Matenga na Rajabu Matimbwa.
Allah katuwekea wazalendo hawa ili waje kuwa mashahidi wa historia ya kweli ya chama cha TANU na harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika.
Picha ya kwanza ni Abbas Sykes, Bilal Rehani Waikela, kulia Bi. Titi Mohamed, Maria Nyerere, Julius Nyerere, Rashid Kawawa na nyuma ya Nyerere ni Tewa Said Tewa, Othman Matenga kama alivyo hivi sasa na picha ya mwisho wa pili kushoto aiyevaa tarbush ni Othman Matenga katika ujana wake yuko katika sherehe ya TANU Tawi la Ali Msham, Magomeni Mapipa.