Hayati mmoja mwanasiasa akiwa waziri wa fedha aliongea kwa jeuri sana kauli iliyomfuata hata baada ya kifo chake, pale aliposema ndege ya Rais ni lazima itanunuliwa ikibidi hata wote tule majani!. Kauli ile ilileta mijadala mingi miongoni mwa wafuatiliaji wa siasa za nchi hii.
Ilikuwa ni jeuri ya hali ya juu sana, kwamba walio katika tabaka la siasa hawawajali wavuja jasho wala hisia zao kwamba watayapokea maneno yao. Ndege ya Rais ikaja na kutumika na ndipo tukagundua kuwa tumepigwa tena pesa ndefu.
Kauli kama ile ya RIP waziri wa fedha wa awamu ya tatu ni kama ilijirudia mwaka huu kutoka kwa waziri mwingine mwenye cheo hicho hicho. Aliposema kuwa tozo zitalipwa tu kama mtu hapendi basi na aende Burundi. Alikutana na kauli nyingi za wanaharakati na ikambidi ajirudi aongee kwa adabu siku alipotangaza kuwa tozo zimefutwa.
Hiki kiburi ni tofauti kabisa na ile hulka ya Bilionea mmoja mwenye asili ya visiwani, ambaye tangu miaka ile ya 1980 mwanzoni akiishi kariakoo amekuwa ni binadamu mwenye kujishusha sana. Miaka ile kila siku ya Ijumaa na siku zile za sherehe za kiislam Mzee Bakhresa anagawa pesa kwa wazee maskini na watu wasiojiweza.
Mpaka miaka ya sasa anabeba jukumu la mazishi ya wapemba wengi wanaofia huku bara, kubeba mwili kuupeleka visiwani na gharama nyingine anazichukua yeye. Utu wake ni baraka kubwa kwa biashara zake.
Watu wanapomuona Bakhresa akitanua biashara zake katika mataifa yanayotuzunguka watambue kuwa hiyo ni faida ya kujishusha na wema ndani yake. Kujinyenyekeza kwamba mzee kuna watu wanakuita hapo nje na yeye akaenda kuwasikiliza shida zao, sio kila mtu mwenye uwezo huo.
Wanasiasa vijana msilewe sana vyeo, magari mazuri ya bei mbaya, walinzi na wasaidizi. Hivyo ni vitu vya kupita tu. Chungeni kauli zenu muda wote, msitegemee ulinzi wa kibinadamu huo hutoweka kama upepo wa baharini.
Ni fahari ya muda mfupi tu. Malkia Elizabeth aliishi ndani ya kasri yenye thamani ya dola bilioni tano lakini siku ya kufa ilipofika walimtoa kutoka alipokuwa analala na kuandaa mipango ya mazishi yake.
Ile kofia ya Malkia ni mabilioni ya fedha thamani yake, siku moyo wake uliposimama na uhai kumtoka kila alichokuwa anavaa kikawekwa pembeni.
Wanasiasa vijana jishusheni siku zote, vyeo na madaraka ni mtego wa muda mfupi.