Ukitaka kutawala milele jenga jamii ya watu wajinga na masikini
Kupiga vita umasikini ni kuongeza Wigo wa ajira..
Katika vitu vinavyonihuzunisha sana ni kuona jinsi nchi inavyoporomoka toka kwenye uchumi rasmi wa wastani uliotawaliwa na viwanda na makampuni makubwa ya biashara ambayo ndiyo yalikuwa yanaajiri sehemu kubwa ya wakazi wa Dar hadi kuelekea uchumi usio rasmi wa machinga, mama lishe, bodaboda, gereji bubu, magenge, n.k.
Eti tunaita “kujiajiri; ujasiriamali”. Tunasifu vijana wenye digrii kuendesha bajaji na kuuza genge. Najiuliza, haya mamilioni ya machinga ambao ni vijana chini ya miaka 35 watakuwaje na watakuwa wapi wakigonga 45 na kuendelea? Bado watakuwa barabarani wakining’iniza bidhaa wanazouza kwa wateja kwenye magari? Na watoto wao watakuwa wapi?
Ushauri kwa wakulu wa chama tawala: punguzeni “mdadi” kwenye ma-flyover na madege ya cash; wekeni uzito mkubwa sana kwenye sera ya TANZANIA YA VIWANDA ili kuokoa vizazi vijavyo na dhiki ya kutisha. Ni sera yenu ingawa siku hizi imebakia blabla zaidi. Achaneni na hii porojo ya wasomi kujiajiri kwenye sekta isiyo rasmi.
Mshirika wenu mkuu, CHINA, juzi alitangaza rasmi nchi yao kufanikiwa kutokomeza umasikini - 100%. China sasa haiko tena kwenye kundi la nchi zinazoendelea. Kilichowainua fasta ni kujijengea uwezo mkubwa wa viwanda kiasi cha kuvutia uwekezaji mkubwa toka nchi za Magharibi. Vijana wa kiChina wengi waliandaliwa kitaaluma na wameajiriwa huko; hakuna hizi porojo za kujiajiri kwenye umachinga. Wanajua huwezi kuendeleza nchi kwa shughuli zinazoangamiza taaluma muhimu katika fani za sayansi, teknolojia, ufundi na mikakati ya uchumi kwa ujumla.
Kwa Afrika, Ethiopia, Rwanda na Ghana wameshaanza kufuatilia mkakati wa China.