Return Of Undertaker
JF-Expert Member
- Jun 12, 2012
- 4,572
- 26,885
Jaji mstaafu na Mwenyekiti wa Tume ya Katiba Mpya amewajia juu wanasiasa hasa wanaowaambia wafuasi wao waseme nini na mawazo mengine yanatolewa majukwaani kwa utashi wa kisiasa kwamba hawatayajumuisha na wasahau kama watayafanyia kazi.
Kadai kuna vyama vya siasa vinatoa mawazo kimaslahi ya kichama nao wasahau kwani Katiba ni ya Watanzania na si ya kichama!
===============================
Habari kwa kirefu
===============================
Kadai kuna vyama vya siasa vinatoa mawazo kimaslahi ya kichama nao wasahau kwani Katiba ni ya Watanzania na si ya kichama!
===============================
Habari kwa kirefu
===============================
MWENYEKITI wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba, amekemea vyama vya siasa, kupenyeza maoni yao katika mabaraza ya Katiba huku vikikejeli wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Alisema hayo jana wakati akifunga mjadala wa siku mbili wa Rasimu ya Katiba, uliofanywa na Baraza la Katiba la Wabunge Wanawake mjini hapa.
"Nazungumza wazi hapa leo, vyama vya siasa ni taasisi, vifuate utaratibu vijadili kama Baraza la katiba la Taasisi na kutuwasilishia maoni yao, sisi Tume hatutachukua maoni ya jukwaani wala ya kwenye helikopta.
"Ukiangalia kwenye Katiba hii, utaona kuwa wananchi wanataka dira ya Taifa, dira ya uchumi, kisiasa na kijamii, lakini cha kushangaza mambo yanayozungumzwa ni machache tu ya madaraka, sasa haya mengine yataboreshwaje?,''alihoji.
Alitaka wanasiasa wasitafute mchawi katika mvutano na mjadala unaoendelea wa kipengele cha Rasimu ya Katiba kinachopendekeza serikali tatu, kwa kuwa kimetokana na maoni ya wananchi na si ya Tume.
"Hili jambo tujue Watanzania wote wamechangia, sisi Tume tumekusanya maoni, wapo waliotaka serikali moja, mbili, tatu na wengine hadi nne, tulichofanya ni kuchanganua maoni na kuyaweka kwenye Rasimu, naomba katika hili asitafutwe mchawi.
"Nasisitiza, hakuna mchawi, mimi nimepokea maoni kutoka kwa Watanzania na naamini walikuwa na akili timamu walipokuwa wakizungumzia suala hili, lakini pia suala la serikali tatu halikuzungumzwa na wananchi pekee, wapo pia viongozi walipendekeza, chonde tusitafute mchawi jamani," alisisitiza.
Alionya vyama vya siasa vinavyofanya kampeni na kuingilia majadiliano ya mabaraza ya Katiba ya wananchi, kupenyeza maoni yao huko, kuwa Tume itayabaini kwa kuwa kwa sasa ina uzoefu wa kutosha.
Kukejeli wajumbe Warioba alisema amepokea pia malalamiko kutoka kwa wajumbe wake ambao walidai kuwa tangu kutoka kwa Rasimu hiyo, wamekuwa wakikejeliwa na kuhusishwa moja kwa moja na yaliyomo.
Alisema wajumbe walionesha kufedheheshwa na kejeli hizo kwa kuwa kazi waliyofanya ni kukusanya maoni ya wananchi, kuyachanganua na kutengeneza Rasimu inayoonesha dira ya nini Watanzania wanataka.
"Nimewaambia wasiwe na wasiwasi, wafanye kazi kwa moyo mmoja, ukifanya kazi ya Taifa lazima ubezwe na hii si mara ya kwanza, hata tulipoanza tulikejeliwa na kubezwa, jambo la msingi ni kuhakikisha wanafanya kazi yao kwa juhudi na weledi," alisema.
Mambo yaliyoachwa Wakati Tume ikikusanya maoni, Warioba alisema katika eneo la elimu wananchi walitaka shule za kimataifa zifutwe, kwa kuwa zinasababisha matabaka ya elimu kwa watoto wa walionacho, viongozi na watoto wa wananchi wa kawaida, jambo ambalo halileti usawa.
Alisema katika afya, pia wananchi walipendekeza safari za viongozi na wagonjwa wengine nje ya nchi kwa matibabu zifutwe, kwa kuwa wananchi wengi wasio na uwezo hupoteza maisha katika hospitali za nchini, jambo ambalo pia linasababisha matabaka.
"Sasa haya na mengine mengi kama vile kwenye kilimo, wakulima kudai kuwa wanatengwa na wafanyakazi, kwamba wafanyakazi wanapewa kipaumbele sana, ndio yanayotakiwa kujadiliwa na kuboreshwa, ili kupatikana Katiba itakayohakikishia Watanzania wote usawa na haki," alisema.
Alisema hatua iliyobaki katika kujadili Rasimu ni ndogo na kushauri Watanzania kuwa huu si muda wa kulumbana, kusemezana na kutafuta uchawi, bali kuheshimiana na kupeana fursa ya kutoa maoni yatakayotengeneza Katiba yenye manufaa kwa wote.
Awali akimkaribisha Jaji Warioba kufunga mjadala huo, Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge Wanawake, Anna Abdallah, alisema Baraza lao lilijadili masuala ya jinsia na yanayosababisha ukatili dhidi ya mwanamke ili yapigwe marufuku na kuingizwa kwenye Katiba hiyo ili yatambulike kisheria.
Pamoja na hayo, kiongozi huyo alizitaka taasisi zote zinazotambulika na kukubalika kisheria, vikiwamo vyama vya siasa, kufuata utaratibu wa kujadili Rasimu na kuwasilisha maoni yao kwa Tume, kwa kuwa tume haitachukua wala kuzingatia maoni ya majukwaani.
Kwa hisani ya Habarileo.