Hanan Ahmed, mmoja wa wajasiriamali 66 wa Ethiopia waliohudhuria warsha ya Programu ya Uwezeshaji wa Ujasiriamali wa Wanawake Duniani (GFEEP) inayofadhiliwa na China huko Addis Ababa, nchini Ethiopia, alikamilisha programu hiyo akiwa na moyo wa mafanikio na ujuzi mpya alioupata katika masuala ya usimamizi wa biashara, uvumbuzi, uongozi na mawazo ya kimfumo.
Warsha hiyo ya wiki mbili, ililenga mawazo ya kimkakati ya biashara, uelewa wa kidijitali, mifumo ya kisasa ya biashara, na ujuzi muhimu wa ujasiriamali. Pia ilitumika kama jukwaa la washiriki kuelelza maarifa na uzoefu na kujenga mitandao ya kitaalamu.
GFEEP ni mpango wa kujenga uwezo unaoongozwa na Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Beijing (BFSU) unaolenga wajasiriamali wanawake kutoka nchi zinazoendelea. Warsha hiyo nchini Ethiopia iliandaliwa na BFSU kwa ushirikiano na Kampuni ya Uhandisi ya Kiraia ya China (CCECC) nchini Ethiopia.
Ahmed, mwanzilishi na afisa mkuu mtendaji wa Han's With Care, kampuni ya ndani inayotengeneza taulo za wanawake nchini Ethiopia, alisema mafunzo hayo yalikuwa "ya kuelimisha na kuleta mabadiliko."
"Nimeshiriki katika programu nyingi za mafunzo, lakini hii ilikuwa tofauti. Ilinisaidia kuelewa ni kwa nini Wachina ni nambari moja duniani. Ni kwa sababu wana mfumo na mkakati wa kipekee wa kufanya biashara. Nilijifunza mbinu mpya, uvumbuzi mpya, na jinsi ninavyoweza kuunganisha uvumbuzi wa biashara na akili bandia (AI) katika biashara yangu," aliiambia Xinhua.
Kwa mujibu wa Ahmed, warsha hiyo ilisifiwa kwa umakini wake wa vitendo, ikiwa ni pamoja na mafunzo kuhusu matumizi bora ya AI, kutangaza bidhaa na huduma kwenye mitandao ya kijamii, na kujenga uhusiano wa kibiashara na kampuni zinazofanya kazi nchini China na sehemu nyingine za dunia.
Mulu Kemal, mjasiriamali mwanamke wa huko anayesafirisha nje injera, chakula kikuu nchini Ethiopia, alisema alipata faida kubwa kutokana na warsha hiyo, ambayo ilimsaidia kukuza mtazamo wa biashara ulio makini zaidi.
"Mafunzo hayo yalihusu ujuzi muhimu kama vile usimamizi wa biashara, uvumbuzi, uongozi na mengine mengi. Yalikuwa ni mafunzo jumuishi. Kabla ya kupata mafunzo, mbinu yangu ya biashara ilikuwa ya kizamani na ya kawaida tu," Kemal alisema.
Licha ya kuwa mama wa watoto wawili na kusimamia majukumu mengi ofisini, Kemal hakukosa kipindi hata kimoja cha mafunzo. Alisema programu hiyo ilimhamasisha kuanzisha mabadiliko ya kimuundo katika shughuli zake za biashara, ikiwa ni pamoja na kuongeza muda wa matumizi ya bidhaa zake kupitia vifungashio bunifu vilivyofungwa vizuri kwa vifaa vilivyoboreshwa, pamoja na kutangaza bidhaa kupitia majukwaa ya biashara ya mtandaoni na masimulizi kwenye mitandao ya kijamii.
Maheder Adimasu, meneja wa shughuli katika kampuni ya chakula ya ndani, alisema ushiriki katika warsha hiyo ulikuwa na manufaa makubwa katika kusaidia biashara kuzoea mazingira yanayobadilika.
"Mafunzo hayo yalikuwa ya kina na yalinisaidia kufikiria upya njia za kuboresha mikakati yetu ya uuzaji na kuimarisha minyororo yetu ya usambazaji," Adimasu aliambia Xinhua.
Akiwapongeza washiriki kwa kujitolea kwao na ushiriki wao katika warsha hiyo, Hu Ruomei, kiongozi wa kozi ya programu hiyo, alisema ni "ushuhuda mzuri" wa kile ushirikiano wa China na Afrika unaweza kufikia kupitia juhudi za pamoja.
"Hamkujiunga na warsha tu; bali mligeuza mafunzo haya kuwa kazi ya sanaa ya kipekee. Kujali kwenu kwa hali ya juu, ujuzi wenu mkubwa wa kupanga na azma endelevu ya kupata matokeo ndio chachu zinazowafanya wanawake kuwa wajasiriamali wa ajabu," Hu alisema.