Pili Mwinyi
Katika kipindi cha kuanzia mwezi Juni wanafunzi wengi wanaojiandaa kuingia chuo kikuu wanakuwa wameshafanya mitihani yao ya kumaliza, na wengi wao wanakuwa wamepata matokeo ya mtihani. Kadiri miaka inavyosonga mbele ndivyo inaonekana kwamba maendeleo ya elimu kwa wanawake yanazidi kuwa makubwa na kuleta fahari isiyo na kifani kwa wanawake wengi ambao huko nyuma walikuwa wakisahauliwa sana kielimu na kuonekana kana kwamba wao hatima yao ni kuhudumia mume, watoto na nyumba tu.
Kitu chochote kile ukikifanya kwa bidii na maarifa, matunda yake huonekana bila kificho, na juhudi za wasichana hawa kuondoa dhana hii ambayo tunaweza kusema kuwa ni potofu kabisa zimezaa matunda, kwani mwaka huu wasichana wameonesha maajabu makubwa katika matokeo yao ya kuingia chuo kikuu.
Katika miaka ya hivi karibuni, wanafunzi hodari wengi wa kike wa China wamekuwa wakijitokeza sana na kufanya vizuri kwenye masomo yao. Mwongozo wa Maendeleo ya Wanawake wa China (2011-2020) umeonesha kuwa, pengo la kijinsia katika ngazi ya elimu ya lazima nchini China kimsingi limeondolewa, na idadi ya wasichana inazidi ile ya wavulana katika ngazi zote za elimu ya juu.
Tangu mwongozo huo uanze kutekelezwa, elimu ya juu imepata maendeleo ya kasi nchini China, huku fursa za wasichana kupata elimu ya juu zikizidi kuongezeka na njia nyingi zimetolewa kwa wanafunzi wa kike wenye matatizo ya kiuchumi na ulemavu, ili kuhakikisha wanapewa elimu ya juu kwa usawa.
Mwaka 2017, idadi ya wasichana ilichukua asilimia 52.5 ya idadi ya jumla ya wanafunzi wa vyuo vikuu, na kuchukua asilimia 48.4 ya idadi ya jumla ya wanafunzi waliosoma shahada zaidi ya uzamili. Takwimu hizo zimeonesha kuwa, katika miongo saba iliyopita tangu Jamhuri ya Watu wa China ianzishwe, wasichana wamepata haki sawa na wavulana katika kupata elimu, ambayo ni maendeleo makubwa na ya kihistoria.
Karl Marx aliwahi kusema kuwa, “Katika jamii yoyote ile, kiwango cha ukombozi wa wanawake ndio kipimo cha asili cha kiwango cha jumla cha ukombozi.” Maneno haya yanadhihirika baada ya hivi karibuni Tanzania kutangaza matokeo ya kidato cha sita, na kuwaacha wengi mdomo wazi kwani hawakuamini kabisa pale waliposikia kwamba kati ya wanafunzi 10 bora katika masomo ya sayansi basi saba ni wasichana na nafasi tatu tu ndio zimechukuliwa na wavulana.
Haya ni mafanikio makubwa sana kwa upande wa wasichana na ni motisha kubwa kwa wale ambao wanaendelea kujiandaa kufanya mtihani ujao wa kumaliza kidato cha sita na cha nne, kwasababu tayari wasichana hawa wamewawekea wenzao kiwango cha juu zaidi cha kujitahidi na kufaulu. Ikimaanisha kwamba wasichana sasa wanatakiwa kuendeleza moto huohuo ulioonesha na wenzao wa mwaka huu, kuhakikisha katika kumi bora kwenye masomo ya sayansi na mengineyo wasichana wanazidi kuwa wengi.
Catherine Alphonse Mwakasige ni msichana aliyesoma tahasusi ya PCB na kumaliza kidato cha sita katika shule ya St. Mary's Mazinde juu iliyopo mkoani Tanga, Tanzania. Huyu ni msichana aliyepata nafasi ya kwanza kwenye matokeo ya mtihani yaliyotangazwa Julai 7 mwaka 2022, na kung’ara zaidi kwenye matokeo hayo ya kidato cha sita katika masomo ya sayansi huku akiwaburuza wavulana wengi sana nyuma yake. Msichana huyu amefaulu vizuri sana na ndoto yake kubwa anasema ni kuwa daktari wa magonjwa ya moyo hapo baadaye.
“Napenda kuwa daktari wa moyo, kwasababu magonjwa ya moyo ni magonjwa yanayotesa watu kwa muda mrefu, ambapo inabidi wapate matibabu nje ya nchi, wakati tupo watu ambao nchi ikitupigania, ikatusomesha tuna uwezo wa kusaidia watu wasio na uwezo wakatibiwa hapahapa nchini” alisema Catherine
Kwa upande wa Tanzania Zanzibar, pia cherekochereko zimetawala katika kipindi hiki baada ya wanafunzi wengi kufanya vizuri ikilinganisha na miaka ya nyuma. Mwanamvua Mfamau Bwanga ambaye ni mwalimu wa shule ya sekondari Zanzibar, lakini kwa sasa ni mwanafunzi katika chuo kikuu cha taifa cha Zanzibar (SUZA) anayesomea ngazi ya uzamivu, anasema kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), kiwango cha ufaulu kimeongezeka hadi asilimia 99.87, huku ufaulu wa wasichana ukiwa juu kwa asilimia 0.08 ukilinganishwa na wa wavulana.
“Kama ilivyo kwa Tanzania Bara, matokeo kwa wasichana ni mazuri sana hapa Zanzibar. Mimi kama mwalimu lakini wakati huohuo kama mzazi ambaye mwanangu pia amefanya mtihani wa kidato cha sita, nathubutu kusema kwamba matokeo yalikuwa mazuri kuliko miaka ya nyuma”. alieleza Mwanamvua
Mwamko wa watoto wa kike kusoma unaonekana kujijenga taratibu kwa muda mrefu sasa. Kwani watoto wa kike wanahamasika baada ya kuona katika jamii inayowazunguka, wanawake wengi wanafanya vizuri na kufika mbali zaidi. Hivi sasa tunashuhudia mambo mengi yakibadilika ulimwenguni, ambapo mwanamke anashika wadhifa katika ngazi mbalimbali kitaifa na kimataifa. Hivyo kwa upande wao watoto wa kike wanaona thamani ya elimu, na kujua namna wanawake wanavyopambana katika ngazi mbalimbali za kimaendeleo na uongozi. Hivyo sasa wameamka na kuona njia pekee ya kufikia walipofika wanawake walio juu ni elimu tu.
“Katika vyuo vikuu bado wanawake tuko wengi. Nikitolea mfano wa chuo kikuu cha SUZA ambako mimi nipo nasoma, katika ngazi zote iwe stashahada, shahada, uzamili au hata uzamivu, bado ukiangalia utakuta wanawake wako wengi.” aliongeza Mwanamvua.