Summarization
Hoja ni tatu
1. Ngamia mnyama kupita kwenye tundu la sindano(sindano hapa inamaanisha kifaa). Hii ni hoja kongwe na iliyozoeleka mno. Kifupi hapa tunaona haiwezekan kabisa ngamia kupita kwenye hilo tundu.
2. Ngamia kama kamba kupita kwenye tundu la sindano kifaa. Hii ni tafsiri ambayo siyo maarufu sana. Hapa ngamia inamaanisha kamba ambayo ni nene na hutumika kuvitia meli iliyozama au kutia nanga. Pia hapa kimantiki ni ngumu kamba hiyo kupita kwenye matundu ya sindano nyingi tunazozifahamu.
3. Ngamia kama mnyama kupita kwenye mlango wa kuingia mji Jerusalem ambao kwao ulijulikana kama tundu la sindano. Kihistoria inaonyesha ni lango ambalo lilikuwa ni dogo kwa umbile lake hivyo ili kupitisha ngamia ilibidi alazimishwe sana kwa kuwa alikuwa hapiti amesimama na watu ndiyo walitumia nguvu kubwa zaidi kumpitisha. Hapa huenda yesu alitaka kututizamisha kuwa ni kwa unyekekevu wa hali ya juu kwa Mungu ndiyo kitu pekee kinachoweza kumuingiza tajiri mbinguni.
Majumuisho:
Hoja ya tatu hapo inaonyesha kuwa kuna uwezekano wa tajiri kuingia mbinguni tofauti na hoja mbili za awali.
Maoni yangu ya awali kabla sijatafuta maandiko zaidi kuhusu hili yananiaminisha hoja ya tatu ni sahihi kwa sababu
kwanza inaonesha kuna uwezekano wa tajiri kuingia mbinguni tofauti na mbili za awali.
Pili, pamoja na kuwa hoja kuwa ngamia kama kamba inajishikiza kwenye ukweli wenye nguvu kwamba alikuwa anaongea na wavuvi ambao bila shaka walielewa vema maudhui ya kamba hiyo. Ikumbukwe ni kanuni ya mawasiliano kuwa mada lazima izingatie muktadha husika lakini ni hakika bila shaka kama alikuwa anaongea na wakazi wa mji wa yerusalemu basi walijua uwepo wa mlango ulioitwa tundu la sindano. Hivyo Yesu alijua fika wataelewa kwa kuwa wanaujua mji wao.
Kosa lenyewe la tafsiri. Kama ulishawahi kufanya kazi au kusomea maarifa kuhusu taaluma ya tafsiri basi pasi na shaka unaweza kuona kuwa huenda mfasiri alitumia tafsiri sisisi zaidi kulifasiri neno ambalo linaibua kiini cha mjadala yaani hakuzingatia matumizi mapana ya neno hilo kutoka katika jamii ya matini chanzi.
Mjadala uendelee
Hakika unastahili heshima ya kipekee kuweza kudadavua hiyo hoja ya ama NGAMIA au KAMBA kwenye mfano alioutoa Yesu.
Mchambuzi mwingine anafafanua ifuatavyo:
Je! Katika Marko 10:25 Bwana Yesu alimaanisha ngamia mnyama au kamba katika Injili Takatifu ya Marko:10:25 alipowaambia mitume wake kuwa,
ni rahisi ngamia kupenya katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu..
Mwanzilishi wa mjadala amehitimisha tafsiri yake ya aya hiyo kwa kuandika
ngamia/camel inayomaanishwa kwenye bible ni kamba.
Baada ya kupitia Biblia Takatifu na baadhi ya nyaraka zenye kutoa ufafanuzi wa aya zenye utata fulani katika Biblia; naomba kutoa mchango wangu zaidi katika mjadala huu kama ifuatavyo:
1. Mafundisho ya Bwana Yesu katika Marko 10:25 yanalingana na Luka 18: 25 na Mathayo 19:24. Katika aya hizi zote, hakubainishwi kama Bwana Yesu alikuwa anaongelea ngamia mnyama au ngamia kamba.
2.THE AFRICAN BIBLE katika ukurasa wa 1766 imelifafanua neno CAMEL kwenye safu ya ufafanuzi ( footnote) kama ifuatavyo: ( tafsiri yangu ya kawaida) " A camel: ngamia kupita kwenye tundu la sindano ni usemi wa mfano kuelezea kile kisichowezekana kibinadamu. Ni Mungu pekee anayeweza kuleta wokovu. Lakini kuacha vyote kwa ajili ya kuingia katika ufalme wa Mungu kuna maana ya kupata zawadi iliyo kuu, sasa na baadaye. Huyo NGAMIA (kwa Kiebrania "GAMAL"), anayeelezwa mara nyingi katika Biblia hutumika kubeba mizigo mizito na kwa usafiri wa watu; na mara nyingi anahusishwa na makabila ya watu wanaohama hama, wa Afrika ya Kaskazini. Huu ni ufafanuzi uliotolewa wa Injili ya Luka 18:25.
Ufafanuzi wa Mathayo 19:24 ni kama ifuatavyo: " Camel": ( Linganisha Marko 10:25; Luka 18:25; Mathayo 23:24). Ngamia ambaye Mafarisayo hummeza wakati wakimchuja mbu(?) . Baadhi ya wadadisi wa maandiko wanatilia shaka kuwa huenda maandiko ya awali yalisomeka kama "KAMILOS" katika lugha ya Kigiriki yakimaanisha KAMBA ( au waya, CABLE). Hata hivyo, sura ya ngamia ( mnyama) kupenya kwenye tundu la sindano, haielezei ugumu, bali kutowezekana". Hapa pameonyeshwa picha ya mnyama ngamia.
Ufafanuzi wa Marko10:25 kwenye footnote: " Camel: "ni kama ifuatavyo: " Jambo muhimu ambalo Bwana Yesu anataka kusema hapa ni kwamba wokovu ni zawadi kutoka kwa Mungu; nayo haipatikani kwa juhudi za kibinadamu pekee".
2. GRUDEN'S COMPLETE CONCORDANCE TO THE OLD AND NEW TESTAMENT katika kufafanua neno "CAMEL", imeonyesha ifuatavyo katika ukurasa wa 74: "CAMEL": ( Ngamia ndio walikuwa wanyama waliotumika kwa usafiri wa binadamu katika nchi za mashariki kwa kuwa ni wanyama wenye nguvu kuliko farasi na wenye kustahimili zaidi magumu. KWA KUWA SEHEMU KUBWA YA ULIMWENGU WA KI-BIBLIA ILIKUWA AMA JANGWA AU NCHI KAVU/ KAME KATIKA VIPINDI FULANI VYA MWAKA, uwezo wa kipekee wa mnyama ngamia wa kuhimili mazingira magumu ya jangwani, ulikuwa ni wa kipekee. Mara nyingi utajiri wa mtu ulipimwa kwa kigezo cha wanyama ngamia. Ngamia walifugwa kwa ajili ya kufanyishwa kazi au kwa ajili ya usafiri wa haraka; na singa zake zilitumika kutengenezea mavazi ( HAPA ZIKANUKULIWA AYA ZA BIBLIA IKIWAMO HIYO INAYOSEMA :
" Ni rahisi kwa ngamia kupenya katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mbinguni, zikaorodheshwa aya Marko 10:25; Mathayo 19: 24; Luka 18:25 na Mathayo 23:24).
3. THE BIBLE READER'S
ENCYCLOPAEDIA AND CONCORDANCE: Imefafanua jina "CAMEL" kama ifuatavyo: "Camel ( Hebrew: " GAMAL". "Kati ya kumbukumbu za kale kabisa za watu wa mashariki, ngamia alichukuliwa kuwa miongoni mwa vianzo muhimu vya utajiri. Ngamia walipotajwa kwa mara ya kwanza kupatikana huko Misri, Arabuni au Kanaani, wanyama hao walipatikana kwa idadi kubwa na walilinganishwa na kondoo, ng'ombe na punda. Ngamia mwenye nundu moja ndiye ngamia anayeongelewa hapa. Haikuruhusiwa kula nyama ya ngamia, ijapokuwa maziwa yake yalikuwa yakitumika kama chakula kwa kiasi kikubwa. Ngamia walifugwa katika idadi kubwa mno". ...hapa pakaorodheshwa aya za Biblia ikiwemo Mathayo19:24 inayohusu somo tunalolijadili hapa.
Kwa upande mwingine, neno kamba, au kwa Kiingereza "CABLE" au "CORD", hakuna mahali katika Biblia Takatifu ambapo limeonyeshwa kuhusishwa na mafundisho ya Bwana Yesu katika Marko 10:25; Luka 18:25; Mathayo 19:24 au Mathayo 23:24 tofauti na maelezo ya mwanzilishi wa mjadala huu. Hata pale tulipoonyeshwa neno la Kigiriki "KAMILOS" katika ufafanuzi wa The African Bible kama ilivyonukuliwa hapo juu, pameoneshwa mashaka katika usahihi wa tafsiri hiyo. Na kwa kuwa enzi hizo Biblia ilipoandikwa, lugha ya Kiswahili ilikuwa bado haijazaliwa, kwa maoni yangu, ni makosa kusema kuwa Bwana Yesu alikuwa anafundisha juu ya ugumu wa kamba kupenya katika tundu la sindano.
Kinyume chake, na kama tulivyoona katika maandiko yenye kuaminika hapo juu; ni wazi kuwa Bwana Yesu alipokuwa anawafundisha mitume wake kwa kutoa mfano wa urahisi kwa ngamia kupenya katika tundu la sindano kuliko kwa tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu kama alivyonukuliwa katika Marko 10:25; Luka 18:25 na Mathayo 19:24, alimaanisha mnyama ngamia na wala siyo "camel" kwa tafsiri ya kamba katika lugha ya Kiswahili.
Kwa hitimisho langu hilo naungana nawe kuwa
tundu la sindano lilikuwa ni lango dogo la kuingia mji wa Yerusalem. Yesu hakumaanisha "sindano ya kushonea" kwa kuwa kwa wakati ule na hata wa sasa "sindano" zina ukubwa wa aina tofauti kulingana na ukubwa wa uzi. Na hata hiyo kamba inayotumika kwenye majahazi pia hupitishwa kwenye matundu yenye ukubwa unaostahili.