• Ni kwa kuikejeli CCM kwa ujenzi wa UDOM
Na Martin Malera, Dodoma
KAULI ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA) kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeshindwa kutekeleza nusu za ahadi zake na badala yake kinajisifia na ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) imeonyesha kumkera Rais Jakaya Kikwete.
Bila kumtaja jina, Rais Kikwete alimjibu Zitto ambaye alitoa kijembe hicho wakati akichangia bajeti ya serikali ya 2010/2011kuwa licha ya ujenzi wa UDOM kutokuwa ndani ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), chuo hicho kimejengwa na serikali ya chama hicho.
Kauli hiyo ya Rais Kikwete imekuja siku tatu baada Zitto kusema kuwa CCM imeshindwa kutekeleza nusu ya ahadi zake na inajisifia kwa ujenzi wa chuo hicho ambao haukuwemo kwenye ilani yake ya uchaguzi.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana wakati akiwahutubia wanafunzi wa vyuo vikuu mkoani Dodoma, waliofanya maandamano ya kumuunga mkono kwa hatua yake ya kutaka kuchukua fomu kuwania urais kwa awamu ya pili.
Rais Kikwete, alitamba kuwa ilani ya CCM ya mwaka 2005, imezungumzia suala la upanuzi wa elimu kwa ujumla wake, lakini serikali kupitia ilani hiyo imeamua kujenga chuo hicho, ili kutekeleza ahadi hiyo kwa wananchi.
"Nasikia kuna mtu mmoja, (Zitto) eti anasema mpango wa ujenzi wa Chuo Kikuu Dodoma hauko kwenye Ilani ya CCM, hiyo ni kweli hatukuandika hivyo, lakini ilani yetu inazungumzia upanuzi wa elimu kwa ujumla kuanzia ngazi ya msingi hadi vyuo vikuu."
"Upanuzi wa elimu ni pamoja na kujenga au kuboresha baadhi ya vyuo na kuvifanya viwe na hadhi ya vyuo vikuu, kwa kuzingatia ilani hiyo, pia tumejenga vyuo vipya, mfano hiki cha Dodoma, tena kwa fedha zetu za ndani. UDOM ni chuo cha kwanza kwa ukubwa, si tu nchini, bali pia barani Afrika," alisema.
Ijumaa wakati akichangia mjadala wa hotuba ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2011/2011, Zitto aliishambulia CCM kwa kushindwa kuondoa umaskini nchini katika kipindi cha miaka minne iliyopita, licha ya serikali yake kuidhinishiwa zaidi ya sh trilioni 37.
Kuhusu ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Zitto ambaye alitumia maneno makali, alisema ujenzi wake hauko katika ahadi za CCM, huku akimtaka mbunge yeyote wa CCM asimame aonyeshe ni wapi ilani ya CCM ilipotoa ahadi itajenga UDOM.
"Kama kuna mbunge wa CCM anayeweza kuja kunionyesha ilani ya CCM ilitoa ahadi ya ujenzi wa UDOM, aje hapa, hakuna, hakuna, ‘nachallenge' kama yupo anayeweza kuonyesha aje, ujenzi wake ni wazo na ahadi ya CHADEMA ya mwaka 1992."
Kauli hiyo ya Zitto ilimfanya Mbunge wa Ukerewe, Dk. Getrude Mongella (CCM), ainuke kitini na kuomba mwongozo wa Spika.
Mongella alisema Zitto amelidanganya Bunge kwani kwenye Ilani ya CCM kuna sehemu inazungumzia mkakati wa kupanua elimu kwa ujumla wake, ikiwemo suala la ujenzi wa vyuo.
Katika mkutano wa jana, Rais Kikwete alizungumzia mafaniko yaliyofikiwa na serikali yake kwenye sekta ya elimu kwa mujibu wa Ilani ya CCM, ambapo imejenga shule nyingi za kata, kuongeza vyuo vikuu kikiwemo Chuo Kikuu cha Dodoma.
Alisema hali hiyo imefanya idadi ya wanafunzi wanaojiunga na sekondari iongezeke, huku idadi ya walimu wanaomaliza vyuo vikuu izidi kuongezeka.
"Kwa mfano mwaka 2005 idadi ya walimu waliomaliza vyuo ilikuwa 250, lakini sasa idadi yao imefikia 500,000, hayo ni mafanikio makubwa.
Rais Kikwete alizungumzia mpango mpya wa elimu nchini maarufu kwa jina la ‘Tanzania Beyond Tomorrow', alisema baada ya miaka mitano ijayo, kila wilaya itakuwa imeunganishwa na mtandao wa mawasilino ya Intaneti.
"Kuna watu wanasema ninapokuwa ziarani nje naenda kutembea, hapana, nimekutana na wamiliki wa kampuni kubwa za teknolijia ya mawasiliano (IT), wataalam wao wameshakuja nchini kufanya utafiti ili kutuunganisha Tanzania na barabara ya mawasiliano ya IT duniani na itafika mahali watoto wetu watakuwa wanasoma kwa kutumia kompyuta tu, tena wakiwa mbali na mwalimu wao," alisema.
Rais Kikwete, aliahidi kwamba serikali itaendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi na kuboresha kasoro zilizopo, huku akiwataka wanaodaiwa mikopo hiyo baada ya kumaliza masomo yao, warejeshe kuwapa nafasi wengine wakopeshwe.
Katika risala yao, wanafunzi hao waliomba waingizwe kwenye timu ya kampeni ya Rais Kikwete, ombi ambalo mwenyekiti huyo wa CCM aliridhia na kuagiza vijana 36 waingizwe kwenye kampeni zake.
Ombi hilo lilikubaliwa na Rais Kikwete, aliyeagiza vijana 36 kutoka vyuo vikuu mkoani hapa waingizwe kwenye kampeni zake za kuwania urais hasa wakati wa mchakato wa kusaka wadhamini 200 kutoka kila mkoa.