Na Mwandishi wetu
14th June 2010
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe
Rais Jakaya Kikwete amemjibu Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto, Kabwe kuhusu ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), kwamba ilikuwa ni hatua ya kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Ingawa hakumataja waziwazi, lakini maneno ya Rais yalionyesha wazi kwamba yalikuwa yakimlenga mbunge huyo.
Kuna mtu alikuwa anadai kwamba ujenzi wa Udom si utekelezaji wa Ilani ya CCM, lakini ni kwamba tulikaa tukazungumza kuhusu kupanua vyuo vikuu (kwa mujibu wa ilani ya CCM) ndipo tukashauriana kwamba kijengwe chuo kikuu kimoja kikubwa Dodoma, alisema.
Alisema baada ya kuafikiana, wakaamua kutoa jengo la Chimwaga lililokuwa la chama chao kwa ajili ya kufanyia mikutano kwa ajili ya chuo kikuu kinachotarajiwa kuwa kikubwa kuliko vyote Afrika Mashariki kitakapokamilika.
Kwa hatua hiyo, sasa tunafanyia vikao vyetu kwenye magodauni kule Kizota, alisema.
Rais alisema chuo hicho kimejengwa kwa pesa za Watanzania na si wafadhili.
Akichangia Bajeti ya Serikali kwa mwaka fedha 2010/11, mwishoni mwa wiki iliyopita, Zitto alisema kwamba ujenzi wa Udom ambao wabunge wa CCM wamekuwa wakijivunia hauko hata kwenye ilani ya uchaguzi ya chama chao.
Aidha alisema kwamba wazo la kubadilisha Chimwaga kuwa Chuo Kikuu lilitolewa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mwaka 1992.
Kama kuna mwana-CCM yeyote humu Bungeni basi asimame kisha atusomee ilani ya chama chake kama kuna ahadi ya kujenga Chuo Kikuu Dodoma. Ujenzi wa chuo hiki lilikuwa ni wazo la Chadema tangu mwaka 1992, alisema Zitto.
Hatua hiyo ilimfanya Mbunge wa Ukerewe, Getrude Mongela kuomba muongozo wa Spika ambapo alisema kwamba ujenzi wa Udom, uko kwenye ilani ya chama chao katika kupengele cha elimu.
CHANZO: NIPASHE