Licha ya umbo lake dogo, Peter Murigi mwenye umri wa miaka minane aliwavutia watazamaji huko Kiambu, katikati mwa Kenya, alipopanda jukwaani kuonesha weledi wake wa Kungfu.
Murigi alikuwa miongoni mwa washiriki mashuhuri katika Mashindano ya nne ya Kitaifa ya Wushu ya Kenya, ambayo yalishirikisha washindani 35 wenye umri wa miaka saba hadi 22.
Akifundishwa Kungfu akiwa na umri wa miaka sita na baba yake, ambaye ni mtaalamu wa muda mrefu wa mchezo huo, Murigi aliwashinda washindani wengi wakubwa na kushinda zawadi ya juu.
"Ninapenda kufanya mazoezi ya kujivingirisha kila wakati tunapokusanyika kwa ajili ya mazoezi ya Kungfu katika mtaa wetu, na leo nilikuwa nimeazimia kuwashinda washindani wangu, ambao walikuwa na nguvu sawa na mimi," alisema, akiongeza kuwa mchezo huo umeongeza uimara wake wa kimwili na kiakili katika miaka miwili iliyopita.
Tangu mashindano ya ubingwa yazinduliwe mwaka 2021, mchezo huo umepata umaarufu mkubwa miongoni mwa vijana wa Kenya. Katika mashindano ya mwaka huu, mwanafunzi wa shule ya sekondari mwenye umri wa miaka 15, Emily Wanjiku, aliwaaacha mdomo wazi watazamaji kwa usahihi na wepesi wake, akipata tuzo ya juu katika moja ya vipengele saba.
Wanjiku alianza mazoezi akiwa na umri wa miaka 10, akipata hamu ya kujifunza kutoka kwa mwalimu. Alisema Kungfu imeimarisha kujiamini kwake, maarifa ya jamii na utimamu wa mwili. "Nina furaha na ninajisikia vizuri kwa kuwa shindano lilikwenda vizuri na kutimiza hamu yangu ya kushinda tuzo ya juu. Mustakabali wa Kungfu katika nchi hii ni mzuri, hivyo ninawahimiza vijana kukumbatia mchezo huu," alisema.
Kungfu imekuwa ikikua nchini Kenya tangu 2000, ikithaminiwa kwa kuboresha afya, nidhamu na umakini wa kiakili.
"Kungfu inakua katika nchi hii. Ni kama mchezo mwingine wowote wa ushindani, ikiwa ni pamoja na kukimbia au mpira wa miguu, na imekuwa na athari zaidi kwani inahusisha kuruka, kujiviringisha na kushughulikia silaha kama vile mkuki kwa usahihi. Ni mchezo mzuri," alisema Ngaruiya Njonge, rais wa Shirikisho la Wushu Kungfu la Kenya.
Njonge alisema mchezo huo pia umeimarisha uhusiano wa kitamaduni wa China na Kenya, huku shirikisho la kitaifa likianzisha mchezo huu katika shule za msingi na sekondari pamoja na vyuo vikuu. Mwanawe, mwenye umri wa miaka 21 aliyesomea kozi ya lugha ya Kichina Collins Njonge, alisema alikubali Kungfu baada ya kuona ushawishi wake mzuri kwa vijana.
"Tangu nilipokuwa mtoto, nimeona jinsi Kungfu inavyowasaidia vijana kujiepusha na dawa za kulevya. Huo ulikuwa msukumo wangu wa kukumbatia sanaa hii ili kubadilisha maisha," alisema. Pia alipata tuzo ya juu katika mashindano hayo.
Mwalimu wa Kungfu Elvis Munyasya Mutua, ambaye amefundisha kwa muongo mmoja na kushiriki katika mashindano ya kikanda, alisema mchezo huo unawavutia vijana wanaotafuta njia mbadala ya uhalifu na matumizi mabaya ya dawa za kulevya.
Mchezo huo umeleta nidhamu, heshima na motisha miongoni mwa vijana, Mutua alisema.