ASKOFU DKT. SHOO AKOSHWA NA UTENDAJI WA MBUNGE SAASHISHA, ASEMA ANAACHA ALAMA
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT Dkt. Fedrick Shoo amesema kuwa wajibu mkubwa wa viongozi wa dini na wale wasio wa kidini kwa maana ya viongozi wa Serikali ni kuhakikisha kuwa wanatimiza yaliyo matakwa ya wanaowahudumia badala ya kujali maisha yao binafsi.
Askofu Dkt. Shoo ameyasema hayo wakati wa hafla ya kumstaafisha kwa heshima Mchungaji Anaeli Masawe ambapo amemtaja Mchungaji huyo kama mmoja wa watumishi waliosimama vyema katika maisha ya utumishi huku wakiutimiza vyema wajibu wao kwa kanisa na washarika.
"Mchungaji Masawe ulitumika ipasavyo na wakati mwingine kwa namna moja ama nyingine safari yako ya uchungaji ilikuwa na majaribu na uliweza kuyashinda kwa kumuamini Kristo, leo unastaafu kwa heshima na kwa umati huu na shangwe hii hakika ulitumika vyema" - Askofu Dkt. Shoo.
Katika hatua nyingine Askofu Shoo hakusita kugusia mambo ya kimaendeleo huku akimtaja Mbunge wa Jimbo la Hai, Mhe. Saashisha Mafuwe kuwa mzalendo katika kufanya kazi yenye kuacha alama na kuleta maendeleo katika jimbo hili.
"Namuona Mbunge wetu Saashisha Mafuwe tupo nae, hakika amefanya mengi na ambayo ni alama kwa Jimbo hili, tuzidi kumuombea afanye zaidi ili iwe alama kwa wananchi na jamii ya Hai" - Askofu Dkt. Shoo
Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa zoezi la kustaafishwa Mchungaji Anaseli Masawe, Mbunge wa Jimbo la Hai, Mhe. Saashisha Mafuwe amesema kuwa ameelekeza nguvu kubwa katika kuwasikiliza wananchi na kutii kiu ya kuwaletea maendeleo huku akisema kuwa atahakikisha anashirikiana na makundi mbalimbali ili kufikia lengo hilo.
"Niseme ukweli najaribu kukaa na kila kundi katika Jimbo hili, iwe watoto, vijana, wazee, hata wale ambao wapo kwenye vijiwe najaribu kuwafikia ili nisikie maoni yao na niweze kuwahudumia. Sitopuuzia hata wazo la mtu mmoja kwa manufaa ya Jimbo letu" - Mhe. Saashisha Mafuwe, Mbunge wa Jimbo la Hai
Ibada na hafla ya kumstaafisha Mchungaji Anaseli Masawe imefanyika katika usharika wa Hai Mjini na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kanisa na Serikali.