WAZIRI DKT. NDUMBARO AONYA MATAMKO TLS
WAZIRI wa Katiba na Sheria Dk. Damas Ndumbaro amekitaka Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) kuacha kutoa matamko yanayovunja hadhi ya serikali badala yake kutumia busara katika kuikosoa na kuielekeza kwa kukaa pamoja mezani.
Dk. Ndumbaro amesema hakuna serikali yoyote duniani ambayo itavumilia kushushiwa hadhi yake akitolea mfano wan chi za Marekani, Ulaya na China na kusema kuwa matamko ama vitendo vyovyote vyenye uashiri wa kuivunjia hadhi serikali havitakubalika.
“Kuna wakati tunaweza kuwaambia kwamba hiki sisi hatujapenda, lakini kuna wakati sisi tunaweza tukakaa kimya tu, tukasubiri, aah sawa na sisi tunawasubiri kwenye kona Fulani tutakutana tu. Kama TLS mnadhani serikali imekosea milango iko wazi badala ya kukimbilia kwenye vyombo vya habarimnatoa matamko ya ajabu ajabu njooni tuongee.” Alisema Waziri Dk. Ndumbari alipozungumza na viongozi na wanachama wa chama hicho wakati wa hafla ya kusaini makubaliano ya ushirikiano baina ya serikali na chama hicho mkoani Dodoma jana.
Katika hafla hiyo, pia wizara ilikabidhi gari jipya aina ya Toyota Landcruiser Prado kwa chama hicho kwa lengo la kusaidia utendaji kazi wa chama hicho katika kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa TLS, Laetitia Ntagazwa alisema matamko yanayotolewa na TLS yanategemea na tabia ya kiongozi aliyepo wakati huo kwa maana kila mmoja amelelewa kwenye makuzi tofauti na kwamba ndani ya chama hicho viongozi ambao ni wanaharakati na wasio wanaharakati hivyo lazima itokee wakati kuwa na mihemko kwa mtu husika.
“Kimsingi katika uongozi wetu kuna wengine ndani yetu ni wanaharakati lakini kuna wengine pia sio wanaharakati kwa hiyo ni lazima utegemee kwamba kuna wakati inawezekana kiongozi wa awamu fulani akawa na mihemko lakini mihemko ile haiondoi sifa na wajibu wa chama cha wanasheria wa Tanganyika wa kuhudumia umma wa watanzania. Kwa hiyo tuseme tu kwamba serikali inapaswa pia kutuelewa kwamba tunapokuwa tunafanya hayo wakati mwingine hatufanyi kwa nia ovu, tunafanya kwa nia ya kuwakumbusha ili kuhakikisha kwamba umma wa watanzania unafurahia maisha.” Alisema Wakili Ntagazwa.