Waziri Prof. Kabudi anazindua Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Machi 3, 2025

Waziri Prof. Kabudi anazindua Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Machi 3, 2025

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Joined
Apr 18, 2017
Posts
3,984
Reaction score
13,760

Waziri-Kabudi-UJzinduzi-Bodi-Ithibati.jpg
Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari imeanzishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 12 cha Sheria ya Huduma za Habari Sura ya 229, ikiwa na jukumu kuu la kutoa ithibati kwa waandishi wa habari hapa nchini.

Bodi hii ni chombo muhimu katika kusimamia viwango vya taaluma ya Uandishi wa Habari, kuhakikisha uzingatiaji wa maadili ya kitaaluma, pamoja na kuwajengea uwezo Waandishi wa Habari ili kuboresha weledi wao. Aidha, tarehe 18 Septemba, 2024 Waziri mwenye dhamana, alifanya uteuzi wa Mwenyekiti pamoja na wajumbe wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari ili ianze kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria.

Kutokana na umuhimu wa Bodi hii, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Aidan Mwaluko Kabudi (Mb) anazindua Bodi hiyo katika Ukumbi wa Mikutano uliopo katika Hoteli ya Johari Rotana, Mtaa wa Sokoine, jijini Dar es Salaam.

Balile-Uzinduzi-Bodi.jpg
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura:
Baraza la Habari Tanzania (MCT), ni chombo kilichoundwa miaka 30 iliyopita na wadau wa tasnia ya habari nchini kwa lengo la kusimamia na kukuza maadili na weledi katika taaluma ya uandishi wa habari nchini.

Na mwaka huu Mheshimiwa Mgeni Rasmi, tunatarajia kusherehekea Miaka 30 ya Sekta ya Habari kujisimamia yenyewe, yaani Self-Regulation ambapo pamoja na mambo mengine tutaangazia mafanikio na changamoto katika mfumo huo wa vyombo vya habari kujisimamia.

Maadhimisho ya miaka 30 ya kujisimamia yanaenda sambamba na mkutano mkubwa wa Mabara ya Habari Duniani yanayotarajiwa kufanyika Julai 14 hadi 17, mwaka huu, katika Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Arusha (AICC) ambapo pamoja na mambo mengine vyombo vya habari nchini na nje ya nchi vitashiriki maonesho ya kazi zao za kihabari zilizosaidia kuchagiza maendeleo ya mataifa yao na kuhamasisha ubunifu na matumizi ya teknolojia. Mawaziri wa Habari wa mataifa kadhaa wamethibitisha kuhudhuria mkutano huo.

Majukumu ambayo MCT imekua ikiyatekeleza tangu kuanzishwa kwake ni pamoja na kutengeneza na kusimamia uzingatiaji wa Kanuni za Maadili kwa Waandishi wa Habari yaani Codes of Ethics for Media Professionals.

MCT imeshirikiana na wadau na mamlaka za elimu kuandaa mitaala ya Uandishi wa Habari kwa Mfumo wa Mafunzo ya Ujuzi na Umahiri (CBET) kwa viwango vya Taifa vya Ufundi (NTA) 4, 5, na 6. Mitaala hiyo imethibitishwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE wakati huo sasa ni NACTVET) na sasa inatambulika kama mitaala rasmi ya kitaifa kwa ngazi ya Astashahada na Stashahada.

MCT kupitia Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) imesaidia kuboresha viwango vya uandishi wa habari na kuhamasisha uandishi wa habari zenye maslahi ya jamii. MCT pia imekuwa ikishiriki katika kuhamasisha upatikanaji wa Sheria nzuri ambazo zitawezesha kukuza ustawi wa sekta ya habari, hata sheria ambayo inaanzisha Bodi hii Mheshimiwa Mgeni Rasmi, pamoja na changamoto zake ni mojawapo ya zile ambazo kwa miaka mingi tumekua tukipigania uwepo wake.

Shughuli hizi ambazo siyo tu zimesaidia kustawi kwa sekta ya habari bali pia zimeboresha mwenendo wa chombo kimoja kimoja cha habari na kwa waandishi mmoja mmoja pia. Kwa msingi huo, kumewezesha vyombo vya habari kujisimamia vyenyewe.

Ninaomba tu niwakumbushe hadhira hii kwamba tukio linaloenda kufanyika leo la kuzindua bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, miaka 30 iliyopita wadau wa habari waliwateua wafuatao kuwa wajumbe wa bodi ya baraza lao la habari ambao uanzishwaji wake haukuwa kwa mujibu wa sheria; wajumbe hao ni: Prof. Geoffrey Mmari, Gervas Moshiro, Mheshimiwa Joseph Warioba, Anthony Ngaiza, Naila Majjid Jiddawi, na Lawrence Kilimwiko, Wengine walikuwa: Edith Lucina Munuo, Dkt. Sengondo Mvungi, Jenerali Ulimwengu, Marie Shaba, Danford Mpumilwa, Masumbuko Lamwai, na Joseph Masanilo.

Malalamiko ya kwanza kuwasilishwa kwa baraza lenye wajumbe wa aina hiyo likingali changa yalitoka kwa Waziri wa Ardhi wa wakati huo, Mhe. Edward Lowassa. Alilalamikia gazeti la Heko, ambalo lilichapisha makala ikidai kwamba Tume ya Warioba kuhusu Rushwa ilikuwa imemwona "mwenye hatia" kwa vitendo vya rushwa na hata kumtaja kwa jina.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili alikuwa Warioba mwenyewe, hivyo alijitoa kwenye kusikiliza kesi hiyo na nafasi yake ikachukuliwa na Hayati Dkt. Sengondo Mvungi, ambaye alikuwa makamu wake. Lowassa alishinda kesi hiyo, na tukio hilo likawa msingi wa uaminifu ambao Baraza liliendelea kujijengea.

Ninapohitimisha, kwa niaba ya Bodi ya Wadhamini ya MCT inayoongozwa na wazee wetu, Profesa Geoffrey Mmari, Jaji mstaafu Joseph Warioba na Jaji mstaafu Augusta Bubeshi na Bodi ya Wakurugenzi wa MCT inayoongozwa na Jaji Benard Luanda, na wajumbe wake wakiwemo Yusuf Khamis, Tido Muhando, Dkt Rose Reuben, Jaji Robert Makaramba, Ali Mwamini, Sophia Komba, Dkt Joyce Bazira na CPA Nkya.

Kwa niaba yao, ninaomba niahidi ushirikiano mkubwa kwa Bodi ya Ithibati inayozinduliwa leo. Kusema ukweli ushirikiano kati ya MCT na JAB umekwishaanza mapema kwani Septemba 18, 2024, Waziri wa zamani wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Jerry Silaa, aliteua wadau sita wa vyombo vya habari kuunda Bodi ya Ithibati ya Wanahabari chini ya Wizara yake, kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016.

Kati ya wajumbe sita walioteuliwa kwenye Bodi ya Ithibati, wawili ni Wajumbe wa Bodi ya MCT, Bw. Tido Mhando ambaye ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo na Dkt. Rose Reuben kama mjumbe.

Hii ni dalili mojawapo ya taasisi hizi mbili kuwa na ushirikiano katika utendaji wa kuwahudumia waandishi wa habari. Katika vikao vya Bodi ya Wadhamini na Wakurugenzi wa MCT kati ya Desemba mwaka jana na Januari, mwaka huu tuliona umuhimu wa wajumbe hawa wawili kutoka MCT waendelee kushika nafasi walizoaminiwa na Serikali kwa faida ya tasnia huku wakiendelea pia kuwa wajumbe wa bodi ya MCT. Kwa taarifa, wajumbe hawa wawili, Ndugu Mhando na Dkt Rose wamo pia katika kamati ya bodi ya MCT inayoshughulikia maadili ya uandishi wa habari.

Mwongozo wa namna ya kuandika habari za Mahakamani, Habari za Uchaguzi, Uandishi wa Habari Vijijini, Uandishi wa Habari za Sayansi, Uandishi wa Habari za Jinsia na Watoto, Uandishi wa Habari katika Mazingira Hatarishi, bila kusahau AZIMIO LAKO PENDWA Azimio la Dar es Salaam kuhusu Uhuru wa Uhariri, Kujitegemea, na Uwajibikaji (DEFIR) kupitia Jopo la Wataalamu wa MCT kuhusu Uhuru wa Kujieleza na Masuala ya Vyombo vya Habari, wewe ukiwa mmoja wa wajumbe wa Jopo la Wajuzi hao. (Think Tank).

Jana nimetambua umuhimu wa Azimio kuhusu Uhuru wa Uhariri nilipomsikia Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ndugu John Mnyika akiwakumbusha wahariri kuzingatia uhuru wao wa uhariri na uwajibikaji. Yeye pamoja na viongozi wengine wa kitaaluma na kisiasa ni miongoni mwa watu zaidi ya 6,000 waliosaini kuheshimu azimio hilo.

Baraza la Habari Tanzania, halikuishia hapo tu, pia lilikuza mashirika ya kitaaluma. MCT imechangia kuanzishwa na kusajiliwa kwa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kulilea mpaka likaweza kujitegemea lenyewe, na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC).

Aidha Baraza limekuwa mstari wa mbele katika kuboresha Mazingira ya Kisheria, ambapo MCT iliwasilisha mapendekezo kwa serikali kuhusu maboresho ya sheria za vyombo vya habari. Imesaidia magazeti katika kesi za mahakamani na pale yalipopigwa marufuku, kama vile Tanzania Daima, Raia Mwema, na Mwana HALISI.

MCT pia imesaidia waandishi wa habari binafsi waliokumbwa na matatizo ya kisheria. Mfano: waandishi wa Mwanza waliotiwa hatiani kwa kifungo cha miaka 30 kwa mashtaka yaliyodaiwa kuwa ya uongo ya wizi wa kutumia silaha Christopher Gamaina, Zephania Mandia, na Manga Msalaba.

GlGt051XQAApEEz.jpeg
Msigwa: Bodi ya Ithibati haijaanzishwa ili kuzuia Watu kuwa Wanahabari
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema uwepo wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari hauna lengo la kufanya Watu wazuiwe kuingia katika tasnia ya Uandishi wa Habari bali inalenga kupatikana kwa huduma bora.

Akizungumza katika Uzinduzi wa Bodi hiyo, leo Machi 3, 2025 amesema “Utafiti tulioufanya hivi karibuni tulibaini Vyuo vyetu vinazalisha zaidi ya Waandishi wa Habari 500 kila mwaka, kusoma ni jambo moja lakini Watu hao wanahitaji kujengewa uwezo ili kuwa na ubora wakufanya kazi iliyobora.”

Ameongeza “Hiyo inaonesha kuna ongeko la Vijana wengi katika tasnia na wengi wao wana Shahada ya Habari, hawapo katika ‘mainstream’, hivyo hao watu unadani watakwenda wapi? Hivyo uwepo wa Bodi ya Ithibati utasaidia kuwafanya wawe bora na kile kinachozalishwa kiwe bora pia na sio kuwazuia kuwa Waandishi wa Habari, kama vyuo vinazalisha unadhani wakitoka hapo watakwenda wapi? Lazima tushirikiane kuwasaidia.”


Prof. Kabudi Bodi ya Ithibati itasaidia kudhibiti usambazaji wa habari za uongo
Akitaja uhumimu wa Bodi ya Ithibati, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Aidan Mwaluko Kabudi amesema katika Dunia ya sasa yenye wingi wa habari kupitia Mitandao ya Kijamii, ithibati ni njia bora ya kudhibiti usambazaji wa habari za uongo (fake news) ambapo kupitia utambulisho rasmi wa Waandishi wa Habari, Wananchi wanaweza kutambua vyanzo vya kuaminika vya habari na kuepuka upotoshaji unaoweza kuleta taharuki katika jamii.

Ametaja umuhimu mwingine ni Kuwathibitisha (accredit) Waandishi wa Habari ikiwa ni njia ya kuzingatia viwango vya kitaaluma, maadili, na uwajibikaji.

Amesema “Waandishi waliothibitishwa wanaweza kupata unafuu wa kupata habari kutoka kwa taasisi za Serikali na sekta binafsi kwa kuwa wanatambulika rasmi. Hiyo itarahisisha kazi yao ya kukusanya na kusambaza habari sahihi kwa umma na kulinda usalama wao hasa wanapofanya kazi katika mazingira hatarishi kama vile migogoro au wakati wa uchaguzi.”


Prof. Kabudi: Kuna umuhimu mkubwa kwa Waandishi wa Habari kutahabari (specialization)
Amesema katika nyakati za sasa na kutokana na kukua kwa teknolojia na mahitaji ya Jamii ni muhimu kwa Waandishi wa Habari kutahabari (specialization) kwa kujikita katika eneo fulani la kuripoti na kuandika Makala au kutengeneza Makala jongefu kama vile Siasa, uchumi, afya, mazingira na mabadiliko ya tabia nchi michezo, teknolojia, au uandishi wa uchunguzi.

Amesema “Ulimwengu wa leo uliojaa taarifa nyingi na mabadiliko ya haraka katika Vyombo vya Habari, kutabahari kumekuwa na umuhimu mkubwa kwa waandishi wa habari na hasa uandishi wa kina wa uchambuzi baada ya habari.”

Ameongeza “Waandishi wa Habari waliobobea na kutabahari eneo fulani hupata uelewa wa kina, hivyo wanaweza kuchambua masuala kwa umakini na kuripoti kwa usahihi. Hii huongeza ubora wa habari na kuifanya iwe na manufaa kwa Jamii. Aidha, Waandishi wa Habari waliobobea na kutabahari hujenga uaminifu na kuwa vyanzo tegemezi vya habari.”


Maelekezo ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Aidan Mwaluko Kabudi kwa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari:

1.
Bodi hii inapaswa kuhakikisha kuwa waandishi wa habari wote wanazingatia sheria, kanuni, na miongozo inayosimamia taaluma yao. Ithibati ya wanahabari itasaidia kudhibiti uandishi usio wa kimaadili na kuongeza heshima ya taaluma hii. Katika hili tunapaswa kuanza kwa kuwalea na kuwapa miongozo mbalimbali juu ya taaluma yao.

2. Bodi inapaswa kuandaa na kusimamia utaratibu wa usajili wa waandishi wa habari kwa kuzingatia viwango vya kitaaluma. Mfumo huu unapaswa kuwa shirikishi na unaoendana na maendeleo ya teknolojia na mazingira ya sasa ya sekta ya habari.

3. Bodi ina jukumu la kuhakikisha kuwa waandishi wa habari wanazingatia maadili ya taaluma kwa kutoa miongozo na mafunzo ya mara kwa mara. Pia, ni muhimu kuwa na utaratibu wa kushughulikia malalamiko na ukiukwaji wa maadili kwa haki na uwazi.

4. ili kufanikisha majukumu yake, Bodi inapaswa kushirikiana na vyombo vya habari, vyuo vya mafunzo ya uandishi wa habari, na wadau wengine ili kuhakikisha kuwa waandishi wa habari wanapata mafunzo ya mara kwa mara na kuwa na ujuzi wa kisasa.

5. wananchi wanapaswa kuelewa umuhimu wa ithibati ya waandishi wa habari na jinsi inavyosaidia kuboresha sekta ya habari. Bodi inapaswa kuandaa programu za uelimishaji ili kuongeza uelewa wa umma kuhusu umuhimu wa taaluma hii kusimamiwa ipasavyo.

6. katika ulimwengu wa sasa wa kidijiti, Bodi hii inapaswa kusaidia kuhakikisha kuwa waandishi wa habari wanatumia teknolojia kwa manufaa ya taaluma yao bila kuvunja maadili. Hii ni pamoja na kudhibiti matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii katika utoaji wa habari.

7. Bodi inapaswa kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha kuwa waandishi wa habari wanafanya kazi zao kwa usalama bila vitisho, unyanyasaji, au vikwazo visivyo vya lazima. Usalama wa wanahabari ni msingi wa uhuru wa vyombo vya habari.
 

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi (kulia) akizindua rasmi Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (Journalists Accreditation Board-JAB) na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Tido Mhando (kulia) leo Machi 3, 2025 jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi (Mb) amesema, kuwathibitisha (accredit) waandishi wa habari ni hatua muhimu katika kuhakikisha taaluma ya uandishi wa habari inazingatia viwango vya kitaaluma, maadili, na uwajibikaji.
Akizungumza katika uzinduzi rasmi wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (Journalists Accreditation Board-JAB) jijini Dar es Salaam, tarehe 03 Machi, 2025, Profesa Kabudi amesema, moja kati ya kazi kubwa za Bodi hiyo ni kutoa ithibati kwa waandishi wa habari, na ndiyo kazi kubwa kutokana na umuhimu wake.

"Kupitia ithibati, itaonyesha waandishi wa habari wenye sifa stahiki na waliopata mafunzo yanayohitajika ili kufanya kazi kwa ufanisi" amesema Profesa Kabudi na kuongeza kuwa, "Hii itasaidia kuimarisha weledi katika tasnia ya habari na kudhibiti usambazaji wa habari zisizo sahihi".





Amesema, vile vile, ithibati itasaidia kulinda haki na uhuru wa waandishi wa habari wanapotekeleza majukumu yao, kwani waandishi wa habari wanaotambulika rasmi wana nafasi nzuri ya kulindwa dhidi ya vitisho, manyanyaso, na madhila wanayoweza kukutana nayo wakiwa kazini.

Profesa Kabudi amesema, katika dunia ya sasa yenye wingi wa habari kupitia mitandao ya kijamii, ithibati ni njia bora ya kudhibiti usambazaji wa habari za uongo (fake news), hivyo kupitia utambulisho rasmi wa waandishi wa habari, wananchi wanaweza kutambua vyanzo vya kuaminika vya habari na kuepuka upotoshaji unaoweza kuleta taharuki katika jamii.






Amesema, ithibati pia itachochea uwajibikaji kwani waandishi wa habari walioithibitishwa wanawajibika kwa Bodi, jambo litalorahisisha usimamizi wa maadili ya taaluma ya habari.

"Ikiwa mwandishi wa habari atakiuka maadili ya uandishi wa habari, ni rahisi kuwajibishwa kwa mujibu wa taratibu zilizopo, hivyo itasaidia kudumisha weledi na uwajibikaji katika sekta ya habari," amesisitiza Prof. Kabudi.

Amesema, kuthibitishwa au kupewa Ithibati na Bodi kunakuza hadhi na heshima ya taaluma ya uandishi wa habari, kama ilivyo kwa taaluma nyingine kama sheria na udaktari.


"Uandishi wa habari hauna budi kutambuliwa rasmi kama taaluma yenye hadhi na umuhimu mkubwa katika jamii" amesema Profesa Kabudi.

Amesema, kupitia ithibati, waandishi wa habari wanapata utambulisho rasmi unaowawezesha kufanya kazi zao kwa uadilifu, na pia itawarahisishia kupata habari kutoka taasisi za Serikali na sekta binafsi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Gerson Msigwa, amesema Bodi ya Ithibati chini ya Wizara hiyo, itakuwa na jukumu la kusimamia maadili ya taaluma na kusaidia kukuza mazingira bora ya utendaji kazi katika Sekta ya Habari hapa nchini.



Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Bodi hiyo, Msigwa ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amekazia kuwa Bodi hiyo itawajibika kuhimiza waandishi wa Habari kuandika kwa weledi, na kuzingatia ukweli, haki na maslahi ya umma.

Amebainisha kuwa Bodi ya Ithibati yenye wajumbe 7 akiwemo Mwenyekiti wake Tido Mhando, itashirikiana na Taasisis za mafunzo na wadau mbalimbali wa tasnia ya Habari kuhakikisha waandishi wa Habari wanapata elimu bora na mafunzo yanayokidhi viwango vya kitaaluma.

Akitoa shukurani zake Mhando amemhakikishia Waziri Kabudi kuwa wajumbe wa Bodi hiyo wamepokea maelekezo aliyowapa na kwamba watayatekeleza kwa moyo wa uzalendo, uadilifu na ufanisi wa hali ya juu kwa ushirikiano na wadau wa sekta ya Habari.

Amesema kwa kuonyesha utayari wa kufanya kazi, vikao vya Bodi ya ithibati vitaanza Jumanne Machi 4;2025, kwa lengo la kupanga mikakati mbalimbali ya utekelezaji wa majukumu ya Bodi hiyo yaliyoainishwa kwa mujibu wa sheria.
 
Bodi hii ni chombo muhimu katika kusimamia viwango vya taaluma ya Uandishi wa Habari, kuhakikisha uzingatiaji wa maadili ya kitaaluma, pamoja na kuwajengea uwezo Waandishi wa Habari ili kuboresha weledi wao. Aidha, tarehe 18 Septemba, 2024 Waziri mwenye dhamana, alifanya uteuzi wa Mwenyekiti pamoja na wajumbe wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari ili ianze kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria.
Acheze singeri kwanza tuamini anachokiamini
 
Back
Top Bottom