Chachu Ombara
JF-Expert Member
- Dec 11, 2012
- 6,067
- 10,938
SERIKALI imetaja sababu za kutokutumika kwa miradi ya nyumba za makazi ya maofisa na askari polisi licha ya kukamilika kwa miaka mitatu iliyopita.
Nyumba hizo ni zile za ghorofa zilizoko Mikocheni na Kunduchi mkoani Dar es Salaam, ambazo ujenzi ulianza mwaka 2014 na kukamilika mwaka 2018 chini ya usimamizi wa mkandarasi Kampuni ya Mara World Tanzania Limited.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, akizungumza na Nipashe jana kuhusu suala hilo, alisema wameshindwa kuingiza askari polisi kuishi kwenye nyumba hizo kutokana na mabadiliko ya kisera yaliyofanyika.
"Kulikuwa na mkataba kati ya serikali na kampuni iliyojenga nyumba hizi ambao mkataba huu baadaye sera zikabadilika ikawa kwamba maeneo ya jeshi yasiingie mikataba na sekta binafsi.
"Baada ya kubadilika kwa sera hiyo, ikasababisha serikali kuingia kwenye majadiliano tunafanyaje kwa sababu tayari mwekezaji alishawekeza kwenye nyumba hizi," alibainisha.
Waziri Simbachawene alisema kwa sasa majadiliano yanaendelea kati ya serikali na mwekezaji ili kupata hatima yake.
"Hatuwezi kuingia mpaka tumalize vizuri na mwekezaji, mjadala unaendelea na tupo katika hatua za mwisho, tukishamalizana tutaruhusu askari wetu waingie, hapo ndipo tulipokwama.
"Mjadala ni mkubwa kwa sababu mkataba ulikuwa wa miaka mingi ambayo ni zaidi ya miaka 50, sasa kwa mazingira kama haya ndiyo maana kumekuwa na ugumu wa kuingia kwenye nyumba.
"Unaingiaje kwenye mali ambayo bado ni ya mtu na kwenye mkataba hamjamalizana vizuri? Tukimaliza tutaweza kuingia." alisema.
Juni 19, 2019, aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, alifanya ziara kwenye nyumba hizo na kutoa mwezi mmoja kwa Shirika la Rasilimali la Jeshi la Polisi kutoa vielelezo kwa kamati ya tathmini iliyoundwa kwa ajili ya mradi wa ofisi ya polisi Oysterbay na nyumba hizo ili zikabidhiwe serikalini.
Masauni alisema miradi hiyo ipo chini ya shirika hilo na kwamba iliundwa kamati ya tathmini iliyokuwa chini ya Wizara ya Fedha na Mipango na kuhusisha wadau mbalimbali.
Katika ripoti yake ya ukaguzi mwaka wa fedha 2019/20 iliyowasilishwa bungeni mwezi uliopita, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, ananyoshea kidole kutotumika kwa miradi iliyokamilika.
Chanzo: Nipashe
Pia soma
- Polisi Watakiwa kuwasilisha Mikataba ya ujenzi eneo la Kunduchi, Mikocheni na Oysterbay jijini Dar