UWT kupanguliwa
Kaanaeli Kaale
Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Sophia Simba, amesema ana mikakati ya kuubadilisha na kuuboresha umoja huo ili kwenda na wakati. Akizungumza katika hafla ya kumpongeza iliyofanyika jana katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, Simba alisema ataunda kamati ambayo itasaidia kuleta mabadiliko hayo na kuufanya kuwa kimbilio la wanawake.
Alifafanua kuwa tofauti na viongozi waliotangulia, viongozi wa sasa wanafanya kazi kwa kuzingatia matakwa ya karne ya 21 ambayo yametawaliwa na changamoto nyingi zinazotokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
UWT ilianzishwa mwaka 1962 lakini saa tupo karne ya 21 ... wengine wanaiita karne ya dot com, hivyo nitafungua ukurasa mpya ndani ya UWT ili tuweze kwenda na mabadiliko ya kisasa, Simba alieleza. Simba, ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), alisema kazi kubwa ya umoja huo ni kutekeleza sera za CCM na kuhakikisha maisha bora kwa kila Mtanzania.
Alisema maisha bora yanaanzia katika familia na mtendaji mkuu katika familia ni mama, hivyo umoja huo utaanzisha programu zitakazowawezesha wanawake kuboresha familia zao. Kama kila familia itakuwa na maisha bora, ni wazi kila Mtanzania atakuwa na maisha bora ... hivyo tutajipanga kuhakikisha mkakati huo unafanikiwa, alisema.
Aliwasihi wanachama wa UWT kuvunja makundi na kufanya kazi kwa pamoja ili kufikia malengo na kutekeleza sera za CCM na kuongeza kuwa Umoja huo utaendelea kuwa na ushirikiano kama kawaida, ila utaongeza kazi ya kuleta maendeleo.
Alisisitiza kuwa ili Umoja huo uweze kufanikiwa, ni lazima viongozi wakubali kufanya kazi na wasomi pamoja na kuhakikisha kuwa idadi ya wanachama wa Umoja huo inaongezeka maradufu. Wasomi watasaidia kuleta maendeleo ya haraka ndani ya chama, hivyo tusiwaogope kwani ni mabinti zetu na wamesoma kwa kutumia fedha zetu
nawasihi viongozi kuanzia ngazi ya kata kukaribisha wasomi hao, alisisitiza.
Aliahidi kufanya kazi kwa uaminifu bila kubagua mtu yeyote kwani anaamini kuwa wagombea wote waliopambana naye wana uwezo na sifa za uongozi ila aliwashinda kwa kuwa Mungu alimchagua yeye kuwa kiongozi wa umoja huo. Simba katika uchaguzi huo uliofanyika Dodoma wiki hii, aliwaangusha Janet Kahama na Joyce Masunga.
Source:
HabariLeo: Gwiji la habari Tanzania | UWT kupanguliwa