Ya Jenerali Ulimwengu yamenigusa!
Azimio la Arusha lenyewe lilikuwa kwa kiwango kikubwa ni azimio la Nyerere, ingawaje lilipitishwa na Halmashauri Kuu ya TANU, na kwa kuungwa mkono na maelfu ya Watanzania, likawa azimio la Watanzania wote.
..Ukweli ni kwamba hakukuwa na mjadala uliowahusisha wananchi (au hata wana-TANU) katika utungaji wa azimio lenyewe wala katika mbinu za utekelezaji wake.
Nimeshawahi kuona mahali pengi mawazo kama haya ya wasomi kwamba miaka hiyo kabla ama baada ya Uhuru hakukuwa na mjadala uliowahusisha wananchi katika maamuzi ya kisiasa
. Pengine tungejiuliza kidogo, hivi wakati huo kabla ama baada ya Uhuru, wananchi wangapi walikuwa na uelewa kisiasa wa kuweza kuchangia mawazo kikamilifu katika kutunga kitu kama Azimio la Arusha ama mbinu za utekelezaji wake? Wananchi waliokuwa na uelewa wa hata namna masuala ya utawala ama mchezo wa siasa ulivyo walikuwa ni wachache mno. Baadhi ya wasomi wachache Waafrika waliokuwepo wakati huo waliogopa kujiitosa kwenye siasa kwa kuogopa kupoteza ajira zao maana Mkoloni alikuwa haruhusu waajiriwa Serikalini kujiingiza kwenye siasa. Kwa hiyo, hata hao waliokuwa viongozi wa Chama cha TANU wengi wao walikuwa hawana kisomo chochote. Kwa maana hiyo walikuwa wakisikiliza na kutegemea mawazo ya watu kama Mwalimu wawaongoze. Ndio hao walioibuka na kaulimbiu ya Zidumu Fikra
Hata humu tukianza kuimba Zidumu Fikra za Mchungaji Kishoka sidhani kwamba atatuambia ah sitaki jamani, tumeamua wenyewe hakutuomba wala kutulazimisha! Hata hivyo, Mwalimu alikuwa mwenye busara aliwahi kuikana kaulimbiu hiyo.
Nikirudi kwenye uelewa mdogo wa siasa wakati huo, ni dhahiri kwamba kama Mwalimu angeliutaka/kuupenda ubepari akaujengea hoja, akauhubiri/kuupigia debe, asingelishindwa kupata wafuasi wengi wa kumuunga mkono. Moja ya sababu za Mwalimu kulivalia njuga suala la elimu kwa wote kwa makusudi kabisa, ilikuwa ni kutaka watu waelimike ili huko mbele ya safari waweze kuwa na uwezo wa kutafakari wenyewe na kuamua mustakabali wa nchi yao. Leo hii, pamoja na elimu bado hatuoni watu wengi (ilivyokusudiwa) wanaokuja na jipya zaidi ya kujenga hoja zao kuzunguka yale yale yaliyoanzishwa na Mwalimu kwa kuunga mkono ama kuyapinga!
Mwaka 1968, tutakumbuka, walichomoza wabunge kadhaa waliotaka kufurukuta na kuihoji TANU ndani ya Bunge la chama kimoja. Alichofanya Nyerere ni kuwashitaki wabunge hao (Kaneno, Bakampenja, Choga, Masha, Anangisye, Mwakitwange) ndani ya vikao vya chama. Wakanyanganywa uwanachama wa TANU, na hivyo wakapoteza ubunge.
Pengine Mwalimu alifanya makosa katika baadhi ya hatua alizochukua. Lakini, katika kuwashughulikia hao wanaodaiwa kufurukuta kuhoji, kama aliwapeleka ama aliwashitaki kwenye vikao vya Chama ikadhihirika ndani ya kikao kwamba wana makosa, wakahukumiwa na vikao hivyo, kosa la Mwalimu ni lipi?
Niliwahi kusikia kwamba Jenerali Ulimwengu alikuwa mmoja wa Wabunge G
waliokuwa wanataka Tanganyika wakati ule. Inasemekana walikwenda Msasani kwa Mwalimu kuelezea greaviences zao zilizowafanya watake/kudai Tanganyika yao! Je, katika mkutano wao na Mwalimu hawakuwa na majadiliano naye, aliwaburuza tu wasomi wazima? Nasikia aliwashinda kwa kuwaambia jambo jepesi sana, Jenerali anaweza kutuambia kama ni kweli ama la. Eti Mwalimu aliwaambia nyinyi ni Wabunge wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa Katiba, kama mwataka Tanganyika yenu basi vueni kwanza huo Ubunge wa Jamuhuri ya Tanzania ndipo mdai Tanganyika! Sijui kama walifanya hivyo.
Hakika ilianza kusadikika kwamba ukipata laana ya Kambarage ujue umemalizika kisiasa, imani ambayo imezidi kujengeka katika miaka ya karibuni.
Watu ambao walidhani wanaweza kumshinda Mwalimu kwa hoja, walipoona kila wakijaribu anawaweka mahali wakajiona hoja zao hazina uzito, ndio hao wanaoeneza uvumi kwamba Mwalimu alikuwa akitoa laana za kisiasa! Walikuwa wakijimaliza wenyewe. Sisi hao hao tunaodai kwamba Mwalimu alikuwa akimaliza watu kisiasa, wakati mwingine tunamsifu kwamba alikuwa anaona mbali! Muona karibu ukipeleka hoja zako zenye mwelekeo wa kuangalia mambo ya karibu karibu tuuu lazima zitapwaya tu mbele ya hoja za muona mbali. Ukweli ndio huo!
Tukubaliane kwamba Mwalimu alikuwa binadamu na aliweza kukosea kama binadamu mwingine yeyote. Lakini, mengi aliyobuni Mwalimu, akafanya na kuyasimamia yalikuwa na mantiki sana na kwa kuwa alikuwa anaelewa kwamba analolisimamia na kulivalia njuga lilikuwa na manufaa kwa Taifa alilokuwa analiongoza, hoja za kumtaka awaze vinginevyo alikuwa hazikubali kwa sababu alikuwa anaona mbali na alikuwa anajua analofanya ni kwa nia njema na lengo zuri.
Utamaduni ulioanzishwa wakati wa Nyerere umeendelea ndani ya chama-tawala kiasi kwamba majadiliano ni nadra sana, na mara nyingi mijadala huzuka ili kumshughulikia mtu fulani, na wala si kusaili hoja wala falsafa. Athari mojawapo ya utamaduni huo ni kwamba hivi sasa, Nyerere akiwa hayupo, hakuna kiongozi hata mmoja, hata wale waliokuwa safu ya mbele kabisa katika kuhubiri Ujamaa leo hii huwezi kuwatambua.
Tatizo hapa si utamaduni ulioanzishwa na Mwalimu bali ni ubinafsi na unafiki wa viongozi wengi waliojiingiza kwenye siasa. Baadhi ya viongozi walikuwa wakiimba wimbo wa Ujamaa wakati roho zao zikitamani ubepari. Kwa hali hiyo walikuwa waoga hata kuujadili Ujamaa wenyewe!
Hali hii ilianza kujitokeza hata wakati Mwalimu akiwa madarakani. Kadri umri ulivyoongezeka na nguvu za mwili kupungua ndivyo kasi ya kusimamia sera na utekelezaji wake ilivyoendelea kupungua, kiasi kwamba chama na sera zake vilianza kuonyesha uzee kadri nywele za Mwalimu zilizvyozidi kuwa nyeupe.
Hii ni kejeli isiyo ya lazima. Mwalimu alikuwa na dhamira ya kuacha uongozi tangu miaka ya 70 zaidi ya miaka 10 kabla ya kungatuka mwaka 1985. Aliamini kwa dhati kabisa kwamba walikuwepo watu ambao wametajwa humu na baadhi ya wachangiaji, watu kama Marehemu Sokoine, Marehemu Mzee Bomani, Mzee Malecela, Mzee Job Lusinde, Dr. Salim Ahmed Salim, Judge Sinde Warioba, Mzee Cleopa Msuya na wengine ambao hadi leo hii bado mishipa ya miili yao imejaa damu ya Ujamaa na roho zao zimejaa uzalendo usiotetereka kwa Taifa letu. Mwalimu aliwaelewa hivyo na aliwathamini sana. Hawa kwa namna moja ama nyingine wangeliweza kuendeleza kwa dhati kabisa Ujamaa na Kujitegemea kama ulivyoasisiwa na Mwalimu, kwa staili zao wenyewe na kwenda na wakati lakini kwa lengo lile lile! Miongoni mwa hao niliowataja yumo ambaye alikuwa ndilo chaguo haswa la Mwalimu kwa urais wa mwaka 1995, kiongozi huyo alimkatalia Mwalimu kwa sababu zake wakati huo. Mwalimu alisikitika lakini aliheshimu maamuzi ya kiongozi huyo. Rafiki yake Jenerali alikuwa ni second choice na yupo mtu aliyempigia debe kwa Mwalimu ambaye hata siku moja hajatajwa popote! Wapo wanaoamini kwamba rafikiye Jenerali alidhani anaweza kuwa na mawazo mbadala ya kuendeleza Taifa nje ya misingi aliyoiweka Mwalimu. Matokeo tumeyaona.
Katika hali ya kutokuwapo na mjadala, sera zilizolenga kumkomboa Mtanzania zikaishia kumletea matatizo ambayo yaliupa Ujamaa jina baya. Serikali ikajiingiza katika biashara isiyokuwa yake kuuza nyama na chumvi; vyama vya ushirika vikavunjwa; serikali za mitaa zikafutwa, na kadhalika.
Maandishi kama haya hayamtendei haki Mwalimu. Mara ngapi Mwalimu alikuwa akienda Chuo Kikuu kujadiliana na wasomi kuhusu mustakabali wa nchi? Mlango wa Msasani ulikuwa wazi wakati wote lakini watu kwa woga wao wakawa hawathubutu kuomba kuonana na Mwalimu ili watoe mawazo yao. Wengine wakawa wanasingizia kwamba Butiku alikuwa akiwazuia kumuona Mwalimu! Wachache waliokuwa wakijiamini, Mwalimu alikuwa akiwasikiliza kwa makini sana. Mwalimu alikuwa akiwasikiliza wazee kwa vijana, hata wahudumu, wapishi, madobi, madreva n.k. na kufanyia kazi aliyoyapata kutoka kwao, sembuse viongozi wenziwe?
Hivi ni kweli Mwalimu alikuwa akilizuia Bunge la chama kimoja kujadiliana juuya namna ya kuboresha ama kushughulikia matatizo ya ki-sera zilizolenga kumkomboa Mtanzania mpaka sera hizo zinakufa etc etc? Viongozi wa mashirika na wananchi waliopewa na Serikali majukumu ya kuuza nyama na chumvi wangelikuwa ni watendaji wazalendo wenye uchungu wa dhati ya maendeleo ya nchi yao, mashirika yote yakaendeshwa kwa ufanisi uliodhamiriwa, leo hii Tanzania tungelikuwa wapi? Mameneja wangapi walijenga nyumba na kufuja fedha za mashirika, kufanya ubadhilifu wa kila aina kwa kutumia nafasi za uongozi walizopewa? Kama Wachina wameweza kujipatia maendeleo ya kiuchumi haraka, sisi ambao tunaambiwa kiongozi wetu alikuwa akiwaiga wao na kusikiliza kila alilosema, ilikuwaje na tulishindwaje kuwa kama Wachina?
Ushauri toka kwenye masufuria jikoni: Hatujachelewa. Tutafute njia za kisasa tuwarudishe vijana kambini, tuwafunze uzalendo wa kupenda na kujali nchi yao kuliko jambo lingine lolote. Sie wazee tukae tucheze na wajukuu zetu na kutoa mawazo ya kukumbushana tulikotoka badala ya kudhani kwamba leo hii tutaweza kufanya yale tuliyoshindwa huko nyuma kwa visingizio kwamba Mwalimu (aliyekuwa na uchungu na nchi yake toka rohoni) alikuwa hawapendi ama alikuwa na nia mbaya na wale wote waliokuwa na hoja zao nyepesi na wenye kuona karibu!
Mchungaji Kishoka, ukoko upo tu. Siku ukija nyumbani nitafute kama nitakuwa bado hai tutajikumbusha ya Ferry na Bunge!