Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 5,352
- 15,876
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MAOMBI YA VISA ZA CHINA KWA RAIA WA TΑΝΖΑΝΙΑ
Itakumbukwa kuwa, mnamo tarehe 16 Aprili, 2026, Wizara ilitoa taarifa kwa umma kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Ubalozi huo katika kushughulikia changamoto mbalimbali za upatikanaji wa viza ya China hapa nchini. Taarifa hiyo pamoja na mambo mengine iliwasisitiza waombaji kuambatisha nyaraka sahihi, kamili na zinazokidhi vigezo husika ili kupunguza mchakato wa uhakiki wa maombi.
Katika kuendeleza jitihada hizo, Ubalozi wa China nchini, hivi karibuni umetoa taarifa kwa umma ikisisitiza kwamba hakuna vikwazo vya kisera vinavyowazuia raia wa Tanzania kuomba visa za China na kwamba maombi ya visa yanayowasilishwa na raia wa Tanzania yanaendelea kushughulikiwa kwa utaratibu na kwa ufanisi.
Aidha, Ubalozi huo unathibitisha kuimarika kwa uhusiano kati ya watu wa China na Tanzania, na unafurahia kuona kwamba idadi ya Watanzania wanaosafiri kwenda China inaendelea kuongezeka.
Vilevile, kutokana na ongezeko la idadi ya waombaji wa visa, Ubalozi wa China nchini Tanzania unachukua hatua mbalimbali za kuongeza uwezo wa kushughulikia maombi, pamoja na kuboresha ufanisi na ubora wa huduma zinazotolewa kwa waombaji.
Hata hivyo, kwa kuzingatia uwezo wa sasa wa kushughulikia maombi na idadi kubwa ya maombi yanayopokelewa, waombaji wanashauriwa kuzingatia maelekezo yafuatayo: -
1. Kuwasilisha maombi mapema
Waombaji wanashauriwa kuwasilisha maombi yao ya visa mtandaoni angalau wiki tatu kabla ya tarehe iliyokusudiwa ya kuondoka kwenda China, ili kutoa muda wa kutosha kwa ajili ya mchakato wa kushughulikia maombi
2. Kuzingatia masharti na taratibu rasmi
Waombaji wanapaswa kuzingatia kikamilifu masharti na taratibu rasmi za maombi ya visa. Maelekezo ya kina yanapatikana kupitia tovuti rasmi ya Ubalozi wa China nchini Tanzania: 中华人民共和国驻坦桑尼亚联合共和国大使馆 1220 11777393.htm?
3. Kufuatilia mfumo wa maombi mtandaoni
Waombaji wanashauriwa kukagua mara kwa mara mfumo wa maombi ya visa mtandaoni na kujibu kwa wakati iwapo wataombwa kufanya marekebisho au kuwasilisha nyaraka za ziada. Kutofanya hivyo kunaweza kusababisha kuchelewa kwa mchakato wa kushughulikia maombi.
4. Kuepuka taarifa potofu
Waombaji wanashauriwa kutopotoshwa na taarifa zisizo sahihi zinazosambazwa na watu au mawakala wanaolenga kujipatia faida. Taarifa sahihi kuhusu maombi ya visa za China zinapatikana kupitia tovuti rasmi ya Ubalozi wa China nchini Tanzania pamoja na akaunti rasmi za Mitandao ya Ubalozi kwenye X na Facebook.
Pamoja na hayo, Wizara inasisitiza wadau wote kuheshimu na kuzingatia sheria, taratibu, mila na desturi za nchi wanazotembelea ili kuendelea kuimarisha uhusiano uliopo kwa manufaa ya pande zote mbili.
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
Pia soma:
~ Tunasota kupata Visa ya China hapa Dar, tunawahi foleni lakini siku ya tatu sasa hatupati huduma
~ Changamoto ya Visa ya China Tanzania: Tatizo ni Madalali, Sio Ubalozi
~ Kijana aliyenyimwa Visa ubalozini kwa ''fujo'' alizofanya Guangzhou -China