Ballali aliacha mikanda ya video
Mwandishi Wetu Juni 11, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo
Ni katika asasi nyeti Marekani
TAKRIBAN mwezi mmoja tangu aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Dk. Daudi Ballali (65) afariki dunia, kile kinachoitwa wosia ama ushahidi aliouacha kinazidi kuwatesa wengi na habari zinasema aliukabidhi pia katika taasisi nyeti za fedha duniani kama Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Habari kutoka vyanzo mbalimbali vya habari zinaeleza kwamba watu kadhaa wanaohofia kuumizwa na wosia huo wamekuwa wakihaha kuhakikisha wanaupata ama kuzuia kuenea kwake na wengine kutaka kueneza propaganda za kupunguza makali yake ndani na nje ya nchi.
Wiki hii Raia Mwema imeambiwa kwamba pamoja na kuwa kuna nyaraka ambazo Dk. Ballali aliziweka katika mikono salama nchini, alipokuwa akiugulia Marekani nako alipata wasaa wa kuweka nyaraka nyingine muhimu katika mikono ya asasi kubwa za kimataifa ambako zinalindwa hadi muda utakapowadia wa kuziweka hadharani.
Ni kweli Ballali ameacha wosia na amerekodi kaseti ya video akielezea yaliyotokea BoT na maelezo mengine kayaweka kwa maandishi. Unajua alihofia familia yake kusumbuliwa kwa hiyo akaamua kuacha katika mikono ya vyombo vya kimataifa na kwa wanasheria, anasema mkongwe mmoja wa siasa za Tanzania ambaye kwa sababu za wazi Raia Mwema haitamtaja jina.
Kauli ya mzee huyo inaungwa mkono na chanzo kingine cha habari kutoka nchini Marekani kinachoeleza bayana kwamba asasi za kimataifa ambazo zimekabidhiwa video hiyo zinaweza kuanika hadharani ama kutumia ushahidi huo katika wakati mwafaka.
Imeelezwa kwamba asasi hizo zinaweza kutumia ushahidi huo kuibana Serikali ya Tanzania kuhusiana na kutowagusa kabisa wahusika wakuu wa upotevu wa fedha ndani ya BoT pamoja na kuwa wanafahamika katika duru mbalimbali serikalini, BoT kwenyewe, benki mbalimbali na katika baadhi ya kampuni za uwakili.
Raia Mwema imearifiwa kwamba Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ambako Dk. Ballali alipata kufanya kazi kwa miaka mingi, na ambako alijizolea sifa kubwa, liliwakilishwa katika mazishi yake na mmoja wa maofisa wake ambaye alimsifia Dk. Ballali kwa kazi nzuri aliyofanya akiwa ofisa wa IMF nchini Ghana, Tanzania na Zimbabwe.
Alikuwa amekuja Tanzania, yeye na aliyekuja kuwa mkewe, Anna Muganda, katika miaka ya katikati ya 1990, baada ya Rais wa wakati huo, Benjamin Mkapa, kuomba kwa IMF na Benki ya Dunia (WB) msaada wa mtaalamu wa fedha ambaye angeongoza marekebisho mbalimbali ya kiuchumi yaliyokuwa yakifanywa.
Hatimaye, mwaka 1998, Mkapa alimtangaza Dk. Ballali kuwa gavana akichukua nafasi iliyokuwa imeachwa na Mkurugenzi wa sasa wa Kampuni ya Umeme (TANESCO), Dk. Idrisa Rashid.
Pamoja na kashfa za wizi wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya BoT ambayo imetawala katika mijadala mbalimbali nchini baada ya kuibuliwa mwaka jana, na ukweli kwamba kuna maeneo aliyafumbia macho ama alikubali kuendeshwa na mashinikizo ya kisiasa, bado IMF ilikuwa ikimwona Dk. Ballali kama mmoja wa maofisa wake waliokuwa wachapa kazi vizuri na habari zinasema ni heshima hiyo iliyosababisha ofisa wake kushiriki mazishi na mawasiliano ya karibu yaliyokuwapo kwa pande hizo mbili katika siku za mwisho za uhai wake.
Taarifa za wiki hii baada ya Raia Mwema kubainisha maoni na baadhi ya vielelezo kadhaa vya eneo moja tu la wizi huo wa EPA katika toleo lake la wiki iliyopita, zinaonyesha kwamba kulikuwa na kasi ya ajabu, ambayo si ya kawaida katika jinsi maofisa wa ngazi mbalimbali ndani ya BoT walivyokuwa wakihaha kufanikisha malipo hayo.
Waraka mmoja ambao Raia Mwema imefanikiwa kuuona unaonyesha kwamba katika muda mfupi, maamuzi mengine yakifanywa ndani ya saa chache tu, kwa mfano, nyaraka za kampuni ya Kagoda Agriculture, zilipita ngazi mbalimbali katika kasi inayoashiria kwamba maofisa wa BoT walikuwa wakifukuzana na mafaili hayo kutoka ofisi moja hadi nyingine.
Mtaalamu mmoja wa masuala ya ununuzi wa madeni ya nje anasema hivi kuhusu kasi hiyo: Suala la ununuzi madeni si suala la kutafuta taarifa leo na kupata leo. Kwamba watu ndani ya BoT na hao waliokuwa wakifuatilia ununuzi wa madeni hayo waliweza kuifanya kazi hiyo ndani ya wiki, tena inaelekea kwa kampuni karibu zote 20, ni jambo ambalo linatia shaka kuhusu usahihi wa madeni yenyewe na inawezekana hata hayo madeni hayakuwapo.
Tangu kufariki dunia kwa Dk. Ballali kumezuka mawazo miongoni mwa wana jamii kwamba huo ndio utakaokuwa mwisho wa suala la wizi wa EPA. Na japo haijazungumzwa wazi, kumekuwapo na jitihada katika idara mbalimbali serikalini za kutaka suala hilo life na Dk. Ballali.
Aidha, Raia Mwema imearifiwa kwamba kumekuwapo pia na uwezekano wa Kamati ya Rais ya kuchunguza EPA inayoundwa na Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema, Mwanasheria Mkuu, Johnson Mwanyika na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Edward Hosea ikaongezewa muda katika kile kinachoelezwa kwamba ni kuchelewesha tu na kuvuta muda ili EPA isahaulike.
Sambamba na hayo, kuna maoni pia kwamba jitihada zimekuwa zikifanyika kutaka baadhi ya washiriki wa wizi wa EPA kubebewa mizigo na watu ambao wamejitoa kafara ili kuepusha muanguko wa kisiasa wa baadhi yao ambao machoni wamekuwa wakionekana kama wanasiasa na wafanyabiashara maarufu, lakini ambao wako katikati ya wizi wa EPA.
Tayari sasa imekuwa rasmi kwamba
. (anamtaja jina) ndiye mhusika mkuu wa fedha za EPA na
..(anamtaja jina) kwa sasa hayupo kabisa na hatajwi popote na wachunguzi wa timu ya Mwanyika, kinaeleza chanzo cha habari chenye mawasiliano ya karibu na watendaji serikalini.
Hata hivyo, mtoa habari huyo ameliambia Raia Mwema kwamba mkakati huo wa Serikali ni wa muda mfupi kwa kuwa kuna maelezo yenye nguvu ambayo yanamhusisha moja kwa moja mwanasiasa anayekingiwa kifua.
Kuna maandishi ya kisheria ambayo yanaeleza kwa kina yaliyotokea BoT na zaidi kuhusu fedha za EPA na kwa kina maelezo hayo yanataja ni jinsi gani mfanyabiashara huyo alivyohusika katika mchakato mzima wa malipo ya fedha hizo, anasema.
Mbali ya wosia huo ambao sasa ni gumzo la kila mtu anayejali, Ballali anaelezwa kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kabla ya kuondoka nchini kwenda Marekani, maelezo ambayo hadi sasa hayajawekwa wazi.
Habari za awali zilieleza kwamba watu mbalimbali walio karibu na Marehemu Ballali, wakiwamo wanasiasa na wanasheria wamekabidhiwa nakala ya maelezo ya gavana huyo wa zamani wa BoT.
Mwanasheria aliyeuona waraka aliouandika Ballali kwa mkono wake anasema umeeleza mambo mengi ya msingi aliyotuhumiwa nayo ikiwamo sakata la fedha za EPA zilizokuwa zikisimamiwa na BoT, zinazokadiriwa kuwa zaidi ya Sh bilioni 133.
Kwa mujibu wa waliouona waraka huo wa wosia, Ballali anaeleza, kwa mfano, jinsi alivyosita kuidhinisha malipo ya Kampuni ya Kagoda Agricultural Limited, ambayo pekee ilikabidhiwa kiasi cha Dola za Marekani 30,732,658.82 (takriban Shilingi Bilioni 40/-) kwa kutumia nyaraka za kughushi.
Ballali ameeleza katika waraka ule kwamba alikataa kuidhinisha malipo hayo akielezea jinsi isivyo sahihi kutumia nyaraka za kughushi lakini aliitwa na mkubwa na kuamrishwa kuidhinisha malipo hayo mara moja. Kampuni ya Kagoda Agricultural Limited inatajwa kuchota zaidi ya Sh bilioni 40.
Kampuni hiyo, kwa mujibu wa kumbukumbu za Msajili wa Makampuni (BRELA), ina ofisi Kipawa Industrial Area Plot namba 87, Temeke, Dar es Salaam lakini eneo hilo lina makampuni tofauti jirani na namba hiyo haionekani na kinachoonekana ni viwanja kuanzia Plot 77 na hata Plot 86 na Plot 88 katika eneo hilo maarufu la viwanda.
Lakini habari zinasema, kama itabidi, maofisa wa BoT na baadhi ya wanasheria, kwa kuokoa nafsi zao, watalazimika kutaja ni nani alikuwa akifuatilia fedha hizo za EPA katika kampuni ya Kagoda; hasa kwa kuwa nyaraka za kisheria zipo za kuhusu mchakato mzima wa unununuzi huo hewa wa madeni.
Raia Mwema imearifiwa kwamba kama ulivyo wosia wa Dk. Ballali, vivuli vya hundi kadhaa, zinazoonyesha ni wapi fedha hizo zilikwenda na nyaraka nyingine zinazoonyesha nani walihusika, ziko katika hifadhi za watu mbalimbali na kwamba wakati utakapofika mambo yote yatawekwa hadharani ama Mahakamani, katika majukwaa ya kisiasa au kwenye vyombo vya habari.
Kamati ya Mwanyika imekuwa ikisema kwamba mkakati wake ni kuhakikisha fedha zote, shilingi bilioni 133, zinarejeshwa kabla ya kuchukuliwa hatua kwa wale waliofanya makosa ya kijinai katika kupata fedha hizo.
Imeelezwa kwamba tayari hata fedha ilizochukua kampuni ya Kagoda nazo zimekwishakuanza kurejeshwa japo kwa awamu, jambo linalodhihirisha kwamba wahusika wanafahamika lakini, pengine, kwa kuwa ni vigogo, wametunziwa heshima.
Uchunguzi wa awali wa mkaguzi wa nje wa BoT, Samuel Sithole, kutoka kampuni ya Kimataifa ya Deloitte & Touche ya Afrika Kusini ulionya kuhusu matendo ya kihalifu ndani ya Kagoda kabla ya kuandikiwa barua na Waziri wa Fedha, Zakia Meghji kwamba fedha hizo zilikwenda katika matumizi nyeti ya usalama wa nchi.
Lakini siku nne baada ya kuandika barua hiyo, Meghji aliifuta akielezea kupotoshwa na Gavana, Dk. Ballali, ambaye tayari wakati huo alikwisha kwenda katika matibabu Marekani. Meghji hakurejeshwa katika uwaziri baada ya mabadiliko ya Februari.
Katika mikutano yake michache na vyombo vya habari wakati wa uhai wake, Dk.Ballali, ambaye ameacha mke na familia, alikuwa akitamka wazi kwamba hakuwahi kuiba hata senti moja ya umma katika kipindi chote akiwa BoT na alikuwa akiwashutumu watu aliowakwamisha kuwa chanzo cha kuandamwa kwake na tuhuma mbalimbali kabla ya kukataliwa kujiuzulu na hatimaye uteuzi wake kutenguliwa na Rais Jakaya Kikwete Januari mwaka huu.