Bado kuna baadhi ya wananchi na hasa wapinzani wanaamini kama mabadiliko Tanzania yataletwa na waliokuwa viongozi wakuu waandamizi ndani ya CCM na serikali ya CCM ambao ni Edward Lowassa na Maalim Seif.
Ikumbukwe kuwa Lowassa na Maalim Seif wanalishwa, kuvalishwa na kulindwa na serikali ya CCM. Hii ina maana na mantiki kubwa sana kwenye siasa za nchi za Afrika. Yaani wanakaa kupanga mikakati ya kuiangusha serikali ya CCM huku wakilindwa na maofisa waliotumwa kufanya kazi na Rais.
Aliyewahi kusema ‘’wajinga ndio waliwao’’ hakukosea kwa sababu hata Tanzania katika uwanja wa siasa kuna wajinga wengi sana ambao ''wanaliwa'' na baadhi ya wanasiasa ambao ni political entrepreneur.
Nilikuwa ninashangaa na kucheka kila nikisoma mabandiko ya baadhi ya watu wakisema ‘’Uchaguzi mdogo wa ubunge na madiwani katika kata 20 ni kipimo cha uongozi wa Rais Magufuli’’.
Nikawa ninajiuliza, kama chaguzi ndogo ndio mizani ya kipimio cha utendaji wa Rais Magufuli kwa kutumia mawe ya mizani yanayoitwa Lowassa na Maalim Seif, basi itakuwa ni kupoteza muda kwa sababu haya mawe hayafai kutumika katika mizani. Haya ni mawe ya kugushi (fake).
Matokeo ya Uchaguzi mdogo wa Mbunge na Udiwani katika kata 20 tumeyasikia na kuyaona. Ni kipigo na kilio kwenye kambi za upinzani.
Ninafahamu kuna baadhi ya watu watakuja na nyimbo zenye chorus zinazosema uchaguzi haukuwa huru na haki kama vile wanalazimishwa kuingia kwenye chaguzi.
Mwaka 2015 wakati vyama vya upinzani vinapanga mkakati wa kukabiliana na CCM, Lowassa alijitokeza na kuwaambia kazi hiyo wamwachie yeye, wao kazi yao iwe ni kupiga kura na kurudi nyumbani. Matokeo yake tunayafahamu.
Huko Zanzibar, wakati CUF inaendelea kufanya vizuri wakati wa zoezi la kuhesabu kura, Maalim Seif alijitokeza na kuvuluga uchaguzi baada ya kujitangaza mshindi kinyume cha sheria ya uchaguzi. Yaliyojiri baadaye ni historia.
Kwa sasa Maalim Seif amewashawishi tena CUF waingie kwenye uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Dimani, Zanzibar wakati huku Bara, Lowassa akiwashawishi CHADEMA waingie tena kwenye uchaguzi wa madiwani wakati hawajajipanga ipasavyo. Matokeo yake tumeyaona. Wamepata kipigo kama cha mwizi!
Waingereza hupenda kusema, “It is difficult to see the picture when you are inside of the frame.”
Wajinga wataendelea kuimba Mabadiliko Lowassa, Lowassa Mabadiliko huku CCM ikiendelea kuwapa kipigo cha kisiasa katika chaguzi mbali mbali.