WANAZUONI wameshauri Katiba mpya iandaliwe kwa kushirikisha wananchi tofauti na zilivyoandaliwa Katiba zilizotangulia.
Hilo linatokana na ukweli kuwa wananchi wataridhika kuwa na Katiba ambayo wameshiriki kuielewa, kuijadili, kuiamua na kuilinda kwa maslahi yao.
Wakichangia mada katika kongamano la Katiba lililoandaliwa na Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA) jana, wanazuoni hao walisema mchakato wa Katiba mpya ni lazima ushirikishe wananchi kikamilifu kwani ndio moja ya upungufu ulio katika Katiba ya sasa na zilizotangulia.
Profesa Issa Shivji katika mada yake, alisema Mamlaka yoyote inatokana na watu kwani ndiyo dhana halisi ya Katiba, hivyo kushirikisha wananchi katika mchakato wa Katiba mpya ni muafaka kitaifa, kwani ni mali ya wananchi.
Profesa Shivji ambaye pia ni Mtaalamu wa Sheria alisema Katiba mpya inahitajika kwani kihistoria, katiba zote zilizopita nchini, wananchi hawakushirikishwa wakati uhalali wa Katiba unategemea ilivyotungwa na ushirikishwaji wa wananchi na upungufu huo hauwezi kurekebishwa kwa kupitia Bunge.
Alisema tangu uhuru zimekuwapo katiba tano; mwaka 1961, 1962, 1964, 1965 na 1977, ambazo zote alisema zilitungwa bila kushirikisha wananchi.
Katiba lazima iwe na uhalali wa kisiasa na kisheria kwa kushirikisha wananchi ili wapate Katiba wanayoielewa na kuilinda
wananchi wanapaswa kupewa nafasi ya kutosha kujadili Katiba mpya kwa maslahi yao, alisema.
Alipendekeza wakati wa mchakato wa Katiba lazima uwepo muafaka wa kitaifa, kisheria na iwepo mijadala midogo kuanzia ngazi ya chini hadi kongamano la kitaifa.
Profesa Shivji ambaye alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema mjadala
wa Katiba usipelekwe bungeni, kwani kitakuwa ndicho chanzo cha kuwagawa wananchi na kukipa nguvu ya Chama Tawala kuweka mambo ya maslahi kwake kutokana na kuwa na wabunge wengi.
Huu ni mchakato wa kisiasa, hauhitaji sheria, kwa hiyo wananchi wapewe nafasi ya kujadili, Bunge litaingia katika mjadala baada ya mchakato huo wa kisiasa
kila kundi likianzisha mjadala huu, tutakuwa na nguvu ya kumshinikiza Rais, hivyo tuhakikishe mjadala unakuwa wa wananchi, alisema.
Jenerali Ulimwengu katika mada yake, alikiri kuwa Watanzania hawajawahi kujadili wala kuandika Katiba yao, lakini sasa fursa imefika ya kuandika Katiba itakayokuwa ya maslahi kwao.
Ulimwengu alisema tabia au dhana iliyojengwa na baadhi ya watawala waliozoea kurekebisha Katiba kwa maslahi binafsi ndiyo inayofanya baadhi yao kupinga hoja ya kuanzisha mchakato wa Katiba mpya.
Alisema mtazamo huo umepitwa na wakati na viongozi wanapaswa kufahamu anayetakiwa sasa kushika hatamu ni mwananchi kupitia Katiba mpya itakayoundwa kwa kuwashirikisha.
Ulimwengu alisema hatua hii ya kutaka Katiba mpya ni nafasi ya Watanzania kujisanifu upya na serikali yenye busara itakuwa inasoma ishara za nyakati na inapaswa kufahamu wakati wa kuacha.
Kwa mujibu wa Ulimwengu, Katiba mpya itafanikiwa iwapo Watanzania watakuwa na utashi wa kitaifa na kuongeza kuwa wananchi wanapaswa kujitambua ili wawe na maadili ya kitaifa.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema suala la kutaka kuwa na Katiba mpya lisichukuliwe kama njia ya Watanzania kujiua, iwe fursa ya kisiasa na kama utakuwapo mshikamano wa kitaifa, Katiba mpya itafanikiwa, vinginevyo kila mmoja akilibeba mwenyewe itashindikana.
Profesa Gaudense Mpangala alisema sababu ya kutaka Katiba mpya ni kuepusha Taifa kuingia kwenye migogoro na umwagaji damu, mambo ambayo yametokea katika nchi zingine jirani.
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, alitoa hadhari kuwa iwapo ripoti ya Tume itakayoundwa na Rais itapelekwa kwenye vyombo vya Katiba, mambo yatakuwa yale yale, hivyo akatoa angalizo la kuhakikisha hilo halitokei na kusisitiza pia mshikamano wa kitaifa kwa alichoeleza kuwa kitasaidia kwenye mchakato wa Katiba mpya.
Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Ananilea Nkya, aliitaka Serikali kuwekeza kwa wananchi kwa kuwa na mijadala mbalimbali ya kuwaelimisha kuhusu suala zima la Katiba na mchakato wa Katiba mpya.
Aliyewahi kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Ibrahim Kaduma, alisema ili kuandika Katiba mpya ni lazima Watanzania wafahamu kwanza ni nini maadili yake ya kitaifa.
Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani, ambaye alikaribishwa kama mgeni kwenye kongamano hilo, alisema amesikia mada, maoni na michango kuhusu matakwa ya Katiba mpya na hivyo atakwenda kuyafanyia kazi.
Nimekuja kama watu wengine, nimekaribishwa kusikiliza mjadala, nimesikia, nimeyapokea nitakwenda kuyafanyia kazi, kwa hiyo kwa sasa siwezi kusema lolote zaidi, alisema.
Chanzo: Habari Leo