"Naomba nikuulize kuna nyumba ya kumbukumbu ya Nyerere ipo Magomeni Mikumi karibu na ofisi ya ACT Wazalendo tupe kidogo historia yake."
Jibu langu:
View attachment 2928950
Makala (Daily News) inasema kuwa nyumba hii ina historia ya kupigania uhuru.
Hii si kweli.
Nyerere kahamia nyumba hii mwaka wa 1958 na hata alipokuwa anaishi Maduka Sita nyumba ile hapakuwa na harakati zozote.
View attachment 2928954
Nyumba ya Nyerere Magomeni Maduka Sita na yeye ndiye huyo anaingia ndani.
Mipango yote na mikutano ya siri ya TANU kuanzia TAA ikifanyika nyumbani kwa Abdul Sykes.
Nyumba hii ya Mtaa wa Ifunda Nyerere alinunua kiwanja kwa fedha zake mwenyewe na akasaidiwa kuijenga na rafiki zake wa karibu: John Rupia, Dossa Aziz na Abdul na Ally Sykes.
Haya maneno alisema Makongoro Nyerere siku ya uzinduzi wa nyumba hii baada ya ukarabati mkubwa.
Mimi na Abdulrahman Ali Msham, mtoto wa Ali Msham tulialikwa kwa kuwa maofisa wa nyumba ile ya kumbukizi walifika kutuhoji historia ya Mwalimu.
Ali Msham alifungua tawi la TANU nyumbani kwake Mtaa wa Jaribu, Magomeni Mapipa na akampa Mama Maria sehemu ndogo hapo nyumbani kwake kwenye tawi la TANU kufanya biashara ya kuuza mafuta ya taa.
Mwalimu alihamia nyumba ile ya Mtaa wa Ifunda mwaka wa 1958 akitokea nyumba iliyokuwa Morogoro Road Maduka Sita ambayo alitafutiwa na TANU.
TANU walimweka Mwalimu hapo kwa kuwa walitaka awe jirani na Ramadhani Aziz mdogo wake Dossa Aziz.
Ramadhani Aziz alikuwa na duka hapo na akiishi hapo hapo.
Nyerere alihamia hapo mwaka wa 1955 akitokea nyumbani kwa Abdul Sykes Mtaa wa Stanley na Sikukuu.
Nyumba hii Nyerere hakukaa muda mrefu akapewa nyumba na serikali ya kikoloni Sea View.
View attachment 2928951
Nyumba ya Abdu Sykes ambayo Nyerere aliishi baada ya kuacha kazi.
Muonekano huu ni baada ya kufanyiwa ukarabati nyumba ya zamani katika miaka ya 1970 lakini zile nyumba mbili kubwa na ndogo aliyoishi Nyerere zilibakia kama zilivyo na ni huu upande wa kulia.
View attachment 2928953
Nyumba ya Abdul Sykes kama ilivyo hivi sasa.
Kwa kuhitimisha ningependa kusema kuwa hii ndiyo historia ambayo haikuwa inafahamika na wengi.